Home » » Jali muda kustawisha bishara yako

Jali muda kustawisha bishara yako

Written By Koka Albert on Friday, July 13, 2012 | 12:07 AM

Staphord Kwanama
MUDA ni rasilimali muhimu katika biashara. Kwa lugha ya ujasiriamali, muda ni kipimo kizuri cha kujua kama kweli wewe ni mjasiriamali au mbabaishaji.

Fikiria chini ya jua, kila mtu bila kujali jinsia katika muda wa saa 24, kuna watu wanafanikiwa na kuna watu mambo yao hayaendi kabisa.

Kwa kuzingatia ukweli kwamba muda ni rasilimali muhimu kwako wewe mjasiriamali. Kwa kuwa muda ni muhimu,  tathimini namna unavyotumia muda wako. Kwa mfano, kama unatumia muda wa kutosha kwa shughuli za kukuingizia fedha au unatumia kwenye bla bla na porojo tu. Ainisha ni mambo gani ambayo siyo ya msingi sana kwako huingilia muda wako mara kwa mara na yanatokana na nini.

Vidokezo vya namna ya kutumia muda wako vizuri; jipangie muda maalumu wa kumaliza jambo na hakikisha unakuwa na msimamo kumaliza jambo hilo ndani ya muda ulojipangia, unaweza kujipongeza endapo umemaliza kwa wakati.

Kwa mfano, pumzika dakika kadhaa kwa kunywa kiburudisho unachokipenda.

Jipangie kipaumbele kwa shughuli ulizonazo, ipi ianze kwanza na ipi ifuate na ipi iwe ya mwisho. Hakikisha unafanya kitu kimoja kwa wakati, usichanganye mambo mara umeshika hiki mara kile, mwisho wa siku, mwezi hata mwaka utajikuta hujafanya jambo lolote.

Katika ofisi yako weka taratibu na sera kuhusu kujali muda ili eleweke kwa kila mmoja ofisini. Mathalani unaweza kuwa na daftari la kuingia kazini na kutoka ili wafanyakazi wako wafike kwa wakati na pia iwe wazi wanatoka muda gani.

Pia hakikisha una kitabu cha kumbukumbu ya mikutano. Mjasiriamali anapaswa kuandika mambo mnayokubaliana kuhusu  wafanyakazi au wateja.

Katika hatua hii, itasaidia kutorudia rudia uamuzi ambao mmekubaliana awali na badala yake, mtakuwa na mambo mapya kuweza kusonga mbele.
Kasimu madaraka au majukumu kwa mfanyakazi mwingine ambaye unaona anaweza kufanya.

Acha kabisa kufanyakazi za watu wengine, kama umemwajiri inaamana unamlipa mshahara sasa iweje ufanye majukumu yake, sisitiza kila mtu afanye majukumu yake hii itaongeza uzoefu na ubunifu katika kazi, na hatimaye tija huongezeka.

Pia ainisha na fanya kazi kidogo muhimu kwa ufanisi kwa mfano, asilimia 20 ya kazi, lakini muhimu ambayo itakuzalishia asilimia 80 ya matarajio ya biashara yako.

Wataalamu wanashauri kufanya kazi zinazohitaji ujuzi na umakini wa hali ya juu wakati wa asubuhi. Usiache au kukatiza kazi bila sababu za msingi. Fika kazini kwako mapema. Pia jipumzishe walau saa moja baada ya kazi.

Pia weka utaratibuwa mtiririko maalumu katika kazi zako,  mathalani shughuli unayofanya leo lazima iwe na uhusiano na malengo ya siku inayofuta au iwe na malengo ya muda mrefu ya biashara yako.
Weka mambo yako wazi na taratibu nzuri za namna ya kila mtu katika biashara yako atatekeleza majukumu yake.
Jaribu kuainisha au kutumia teknolojia ya kisasa katika biashara yako ili kurahisisha kazi na kupunguza muda ambao ingefanyika bila nyenzo au teknolojia.

Kwa mfano,  badala ya kutuma mtu kupeleka barua sehemu fulani na kumlipa fedha, tumia kompyuta, mtandao wa barua pepe au nukushi ambao utakusaidia kufikisha ujumbe ndani ya sekunde tu na majibu kupatikana ndani ya muda mfupi. Teknolojia pia inategemeana na ukubwa wa biashara mathalani kama biashara ni ndogo unaweza kutumia excel katika kutunza kumbukumbu za hesabu na taarifa mbalimbali za biashara kama mauzo.

Lakini biashara inapokuwa kubwa unahitaji kutumia pakeji maalumu kama ya uhasibu.

Fanya biashara yako kitaalamu, muda ni mali, pangilia mambo yako kwa mizania na toa kipaumbele kwa shughuli za kibiashara zinazokuingizia fedha.

Pia jipangie muda kwa mfano, mara moja kwa mwezi kutathimini mwenendo mzima wa biashara yako na weka mikakati ya kuboresha.
Share this article :

+ comments + 1 comments

July 16, 2012 at 5:51 AM

un caloroso saluto...ciao

Post a Comment

KARIBU KATIKA WEBSITE YA KIJANJA, KUPATA HABARI MBALIMBALI ZA NDANI NA NJE YA NCHI. PIA UTAPATA MAMBO YA ACADEMIC. KARIBU SANA
 
Support : Creating Website | Johny Template | Mas Template
Copyright © 2011. GetInformedTz - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Mas Template
Proudly powered by Blogger