BBC-Swahili

Sample Text

Habari

Labels

Labels

Social Icons

Blog Archive

About Me

My photo
I would like to welcome all the interested people to join the blog and together we help each other to reach our goals.

Featured Posts

Designed by Edservant. Powered by Blogger.

Sample Text

Latest Post

CCM sasa vurugu tupu

Written By Koka Albert on Thursday, May 31, 2012 | 12:35 AM

MUKAMA ASEMA KINA MPASUKO MKUBWA KAMA G8, NATO, MAIGE AMLIPUA NAPE, ASEMA NI GAMBA LINALOPASWA KUVULIWA
Amini Yasini, Rufiji na Ahmed Makongo, Kahama
HALI ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), si shwari na Katibu Mkuu wake, Wilson Mukama amekiri kwamba hivi sasa kina mpasuko mkubwa unaotokana na makundi yanayofanana na yale ya Umoja wa Kujihami wa Nchi za Magharibi (Nato) na Umoja wa Mataifa yenye nguvu kubwa kiuchumi duniani (G8).

Wakati mtendaji mkuu huyo wa chama tawala akitoa kauli hiyo, aliyekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Ezekiel Maige ameibuka na kumshambulia waziwazi, Katibu wa Taifa wa Itikadi na Uenezi wa chama hicho, Nape Nnauye akimtuhumu kukiharibu kwa utendaji mbovu, hivyo kutaka ang’olewe haraka akidai kuwa ni gamba.

Nchi zinazounda G8 ni Marekani, Canada, Ufaransa, Ujerumani, Italia, Japan, Russia na Uingereza ambazo pia baadhi yao, ndizo zinazounda Nato, umoja wenye wanachama 28.

Mukama alitoa kauli hiyo juzi wilayani Rufiji wakati akizungumza na umati wa wananchi na wanachama wa chama hicho waliofurika katika Viwanja vya Corecu, Kata ya Kibiti.

Alisema baadhi ya wanachama wa CCM wamekuwa ni wasaka madaraka na wanapokosa huamua kuunda makundi ya uhasama ambayo hawataki kuyavunja pindi mchakato wa kutafuta mgombea unapomalizika.

“Makundi yaliyoundwa tangu 2005 na 2010 yanaendelea kukitafuna chama, wanachama wakinyimwa uongozi wanaanza uhasama, hatufiki malizeni makundi,” alisema.

Alisema makundi hayo pia yako katika Wilaya za Mkuranga na Rufiji, ambako katika ziara yake amebaini mpasuko mkubwa unaotokana na fitina na uhasama miongoni mwa wapenzi na makada wa CCM na kusisitiza kwamba hayafai na ni hatari kwa mustakabali wa chama hicho kikongwe barani Afrika.

“Nikiwa Mkuranga nilitaarifiwa kuwa kuna makundi ya Nato na G8 na sasa nimefika Rufiji nimeyakuta makundi hayo. Jamani makundi hayo ya nini?”
Mukama ambaye aliwahi kushika nafasi mbalimbali za kiutendaji zikiwemo za Ukuu wa Wilaya ya Mafia akimrithi mtangulizi wake Hemedi Mkali, alisema aliwahi kugombea ubunge wa viti vya Taifa kupitia Juwata (iliyokuwa Jumuiya ya Wafanyakazi Tanzania), na aliposhindwa alikubali matokeo.

Alisema Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere aliwahi kusema bila CCM imara nchi yetu itayumba, akimaanisha kuwa hakuna chama mbadala cha kuongoza nchi zaidi yake.

Alitoa mfano wa Chama cha Democrat cha Marekani kwamba wanachama wake hawana kadi, bali mapenzi ya chama yako mioyoni mwao na wanapojiunga hawafanyi hivyo kwa lengo la kusaka madaraka... “Hii ni tofauti kubwa na nchi zetu ambako mtu akijiunga na chama kitu kwanza kufikiria ni kusaka madaraka,” alisema.

Alisema chama hicho kina mkakati madhubuti wa kupambana na watu wachache wanaotaka kukimiliki wakitumia nguvu ya fedha.

Alisema baadhi ya wanachama wa kawaida wamejiona kuwa hawana nafasi katika chama chao wakiamini kuwa kimetekwa na wenye fedha na kuongeza kwamba mwanachama wa kawaida hawezi kuongoza bila rushwa.

“Hapana! Chama chetu hakitakubali hali hiyo. Ni hatari sana kwa mustakabali wa chama chetu na nchi yetu,” alisema na kuongeza kuwa wanachama wa kawaida wanatakiwa kugombea hata kama hawana fedha.

Alisema chama kipo katika uchaguzi wake wa ndani na kuwataka wanachama kufanya uamuzi sahihi wa kuchagua viongozi waadilifu wasiotumia rushwa, kwani kufanya hivyo kunaweza kusababisha kuingia watu katika uongozi waliotoa rushwa.

Katika mikutano yake hiyo, Mukama alitamba kuwa chama chake hakitishwi na wapita njia akimaanisha wapinzani wanaodai kuwa hakijafanya kitu.

Alisema CCM ni chama makini na sikivu katika kusikiliza kero za wananchi akitamba kwamba kimejenga Daraja la Mkapa ambalo limekuwa kiunganishi kati ya Mikoa ya Lindi, Mtwara na Dar es Salaam na umeme wa gesi unaotoka kusini ambao wananchi wa Rufiji wananufaika nao kwa sasa.

Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Rufiji, Mrisho Matimbwa alisema katika uchaguzi uliopita wa chama hicho kulikuwa na makundi mawili, ya Bush na Al Qaeda ambayo kwa sasa yamekufa na kubakia mpasuko katika halmashauri kuu ambako aliahidi kuutatua.

Maige na Nape

Akizindua matawi mawili ya wakereketwa wajasiriamali wa CCM katika Kijiji cha Isaka, Kahama, Shinyanga, Maige ambaye ni Mbunge wa Msalala alimtaka Nape kuacha tabia yake ya kutoa kauli ambazo kwa namna moja au nyingine zinaelekea kukidhoofisha chama.

Alimtaka kupima utendaji wake tangu alipoishika nafasi hiyo ya Itikadi na Uenezi na kujiuliza ni wanachama wangapi wameingia ndani ya chama hicho.

Alisema sasa hivi kuna wimbi kubwa la wanachama wa chama hicho kuhama na kukimbilia upinzani na kusema ni wajibu wa Nape kupima na kuona kuwa kazi ya itikadi na uenezi haiwezi na kwani hajui wajibu wake akisema ni mtu wa kumhurumia.

Maige alisema mbali ya kushindwa kuzuia wimbi la wanachama kukihama CCM pia hapaswi kuvumiliwa kutokana na kauli yake kwamba hata kama wanachama watahama wote na akabaki yeye (Nape) peke yake, haitakufa. Alisema kauli hiyo haikijengi chama, bali kuchochea makundi ambayo yanaweza kukibomoa.

Alisema akiwa mwana CCM anaona kwamba sasa hivi Nape amekuwa hafanyi kazi ya uenezi na kukirejeshea haiba na mvuto ambao umepotea kwa wananchi na kwamba, kazi anayoifanya sasa ni kukuza makundi na kusema ovyo.

Aliendelea kumshambulia Nape kwa maneno akisema amejenga jeuri, kiburi, dharau na ulevi wa madaraka huku akidai kwamba kitendo cha CCM kupoteza wanachama zaidi ya 10,000 kwa wakati mmoja mkoani Arusha na sehemu nyingine wanachama 3,000 ni ishara ya hatari lakini, Nape amekuwa akiwaita wanaohama kwamba ni mzigo.

“Huyu Nape ni lazima atupishe. amekifanya chama kama mali yake, yeye ndiye mwenye jukumu la kueneza sera za chama na kutafuta wanachama wapya, lakini ndiyo kwanza anasema waachwe waondoke, Chadema wanatamba kila siku yeye hajali, huyu nasema ni gamba ni bora atupishe,” alisema.

Baada ya mashambulizi hayo, Maige alijitetea kwamba maneno yake dhidi ya Nape yasitafsiriwe kama ni kuulilia uwaziri: “Ni uchungu nilionao kwa chama changu kuona kila siku zinavyokwenda ndivyo tunavyopoteza idadi kubwa ya wanachama, tuliyemkabidhi jukumu la uenezi anasema hajali, sasa huyu si atupishe mapema kabla mambo hayajaharibika?”

Tushirikiane kuilinda AMANI yetu

KATIKA hali isiyokuwa ya kawaida tangu kuanzishwa kwa serikali ya maridhiano Zanzibar mwaka 2010, kwa siku tatu mfululizo zimetokea vurugu kubwa zilizohusisha watu wanaodaiwa kuwa wafuasi wa Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislamu (Jumiki), kwa kile kinachodaiwa kupinga Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
 
Vurugu hizo zilianza Jumamosi jioni baada ya wafuasi hao kuvamia maeneo mbalimbali, yakiwamo vituo vya polisi. Katika vurugu hizo, wafuasi hao wanadaiwa kuharibu mali, kuchoma moto magari na matairi ya magari, kurusha mawe, kuweka vizuizi katika barabara kuu za kutoka na kuingia Zanzibar.
 
Polisi wanadai pia kwamba makanisa matatu, moja la Assemblies of God na mawili ya Katoliki yalichomwa moto, huku baa tatu zikiporwa na kuchomwa moto na watu wanaodaiwa kuficha sura zao kwa vitambaa vyeupe. Habari zinasema, hadi kufikia jana jioni polisi walikuwa wamewatia mbaroni watu kadhaa.
 
Habari hizo bila shaka siyo tu zimewasikitisha wananchi wengi, bali pia zimeleta aibu na fedheha kubwa kwa nchi yetu mbele ya jumuiya ya kimataifa. Tunasema hivyo kwa sababu kwa muda mrefu sasa  taswira ya nchi yetu mbele ya jumuiya ya kimataifa imekuwa nzuri kiasi cha kuvutia watu wengi, wakiwamo watalii, wawekezaji na makundi mengine ambayo siyo tu yamevutiwa  na vivutio vingi vilivyopo, bali pia vimekoshwa na hali ya usalama, umoja na utulivu ambao tumekuwa nao tangu Tanganyika na Zanzibar ziungane mwaka 1964.
 
Ndiyo maana tunalaani vikundi vyote vilivyohusika katika kupandikiza chuki zilizosababisha vurugu hizo na uharibifu mkubwa wa mali katika visiwa hivyo na kusema kwamba lazima mamlaka husika zichukue hatua stahiki kuhakikisha wahalifu hao wanafikishwa katika vyombo vya sheria. Pamoja na kwamba vyombo vya sheria ndivyo pekee vyenye dhima ya  kusimamia sheria na kutoa adhabu kwa wahalifu, tunayo haki pia kama wananchi kusema lazima watakaotiwa hatiani kwa uhalifu huu wapewe adhabu kali ambayo hawataisahau milele.
 
Tunasema hivyo kwa kutilia maanani kwamba kuna kila dalili kuwa, nchi yetu  itaangamia iwapo watu wachache miongoni mwetu wataachiwa kutuvuruga kwa misingi ya kidini na kikabila kwa lengo la kutimiza malengo yao ya kisiasa. Pamoja na uhuru wa kuabudu na haki ya kila mwananchi kuishi mahali popote Tanzania  ambao umewekwa wazi katika Katiba, inakuwaje tunawaacha wendawazimu fulani wapokonye haki hiyo kwa kuchoma moto nyumba za ibada, baa, kubagua wananchi wenye asili ya Bara na kutishia uhai na mali zao? Mbona wananchi wa Zanzibar waishio Bara wanaishi kwa uhuru, amani na upendo?
 
Tunashangaa kuona kwamba hali ya amani visiwani imeendelea kuwa tete tangu kuanzishwa kwa vikundi vinavyohamasisha wananchi kuukataa Muungano. Lakini tunashangazwa zaidi na ukimya wa viongozi wa Serikali ya Mapinduzi (SMZ) na ya Muungano kukaa tu kama watazamaji, huku vikundi hivyo ambavyo  vinachukua sura ya kigaidi kila kukicha,  vikileta hofu kubwa kwa wananchi.
 
Ni jambo lisiloelezeka kwamba vikundi hivyo vya ubaguzi vinaweza kuachwa siyo tu viwagawe na kuwatisha wananchi, bali pia vifumbiwe macho na viongozi kiasi cha kuachwa viwadhalilishe kwa matusi ya nguoni waasisi wa Muungano wetu, yaani Mwalimu Julius Nyerere na Abeid Amani Karume. Hii ni hali isiyokubalika hata kidogo na tusione ajabu iwapo wananchi wa pande mbili za Muungano wanaoheshimu mchango wa waasisi wetu hao waseme sasa inatosha, hivyo waanzishe mapambano dhidi ya vikundi hivyo.
 
Sisi tunasema viongozi wa serikali zote mbili waache woga na wasimamie mambo ya msingi yaliyotuleta pamoja kama Watanzania. Katika kusema hivyo hatuna maana kwamba  wananchi wasiukosoe Muungano au kusema aina ya Muungano wanaoutaka. Hata kidogo. Tunachosema hapa ni kwamba tusiwaache watu wachache watumie nafasi hiyo kuisambaratisha nchi yetu kwa kisingizio chochote kile. Ndiyo maana tunasema  amani ya nchi yetu lazima tuilinde kwa nguvu zote.
  

Umbumbumbu unaliumiza taifa kwenye mikataba

Written By Koka Albert on Tuesday, May 29, 2012 | 3:12 AM

Fredy Azzah
MKUU wa Shule ya Sheria Dk Gerald Ndika, amesema ‘umbumbumbu’ kwenye suala la mikataba ya kimataifa, linachangangia kuliingiza taifa kwenye wimbi la mikataba mibovu.

Dk Ndika aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam, katika ufunguzi wa mafunzo ya mikataba yanayofanywa na wataalam kutoka kampuni ya kimataifa ya sheria ya DLA Piper na General Electric (GE).

“Mikataba kama ya kukodisha ndege, inahitaji mtu ambaye amebobea katika eneo hilo siyo kila mtu tu anaweza kufanya kila kitu,” alisema Dk Ndika na kuongeza:

“Kwa hiyo siyo rushwa tu inasababisha sisi kuwa na mikataba mibovu, hata kutokuwa na ujuzi wa kutosha katika kuandika na kujadiliana juu ya mikataba ya kimataifa ni tatizo.”

Akisisitiza kuhusu suala hilo, Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Angela Kairuki, alisema mbali na uandishi wa mikataba, suala la kuweza kujadiliana kwenye mikataba ya kimataifa ni muhimu zaidi.
“Watu wanaweza kukuzidi ujanja tu kwenye kujadili na mkataba ukawa mbovu, kwa hiyo eneo hili pia lazima tulitazame kwa makini zaidi,” alisema Kairuki.

Alisema kuwa ni vyema wafunzi hao wakapewa mafunzo zaidi juu ya mikataba ya mafuta na gesi, sekta ambayo inatarajiwa kuwa moja eneo muhimu la uchumi nchini.

Mafunzo hayo yanatarajiwa kulenga zaidi katika kujenga uwezo na mbinu za kuandika maandiko ya kisheria katika uandikaji wa mijadala ikiwa ni pamoja na majadiliano na vipengele vya kutengeneza upatanishi na mizozo.

Mwendelezo wa kesi mahakamani, mikataba ya kuuza na kununua, mikataba ya mikopo ni maeneo mengine ambayo wataalam hao kutoka nchi mbalimbali za Ulaya na Afrika watawafunza wanafunzi hao.
Mkuu wa mradi huo Simon Boon kutoka DLA Piper ya London, alisema ni jambo zuru kuwa nchini kwa mara ya tatu kutoa mafunzo hayo, tangu mpango huo ulipoanza mwaka 2010.

 “Tunafurahi kupindukia kurudi kwa mara ya tatu mfululizo kufundisha uandishi wa sheria katika chuo cha sheria Tanzania,” alisema Boon.

Wanawake wanaongoza kuwapiga waume zao Dar

Aidan Mhando
KITUO cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), kimezindua Ripoti yake ya Haki za Binadamu ya mwaka 2011 inayoonyesha pamoja na mambo mengine, wanawake visiwani Zanzibar na katika Mkoa wa Dar es Salaam, wanaongoza kuwapiga waume zao.

Mbali na ukatili huo kwa wanandoa, ripoti hiyo imeonyesha pia kuwa vitendo vya rushwa nchini vimeendelea kuwa sugu na kugusa maeneo muhimu kwa ustawi wa jamii, ikiwamo bungeni ambako imedai kuwa baadhi ya wabunge wanahongwa ili kupitisha bajeti za wizara.

Akisoma ripoti hiyo kwa waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa LHRC, Dk Hellen Kijo-Bisimba alisema asilimia 7.3 ya wanawake wa Unguja Kusini huwapiga waume zao wakifuatiwa na Mikoa ya Dar es Salaam, Mjini Magharibi na Lindi ambako asilimia 5.3 ya wanawake huwapiga waume zao.

“Hata hivyo, Dar es Salaam inashika nafasi ya pili kwa kuwa ina watu wengi ikilinganishwa na mikoa mingine. Mkoa wa mwisho ni Iringa ambako tatizo hilo liko kwa asilimia 4.7,” alisema.  Dk Bisimba alisema ripoti hiyo ni ya 10 kuzinduliwa na LHRC na ya mwaka huu imegusa maeneo mbalimbali na kuanisha yale ambayo haki za binadamu zinakiukwa kwa kiwango kikubwa.

 Alisema kulingana na tafiti zilizofanywa na waandishi wa ripoti hiyo, vitendo vya wanawake kuwapiga waume zao ni moja ya tatizo la ukatili kwa haki za binadamu.  Dk Bisimba alisema mbali na ukatili wa wanawake kuwapiga waume zao, ripoti hiyo pia inaonyesha kwamba Mkoa wa Dodoma unaongoza kwa vitendo vya ukatili kwa kina mama ukifuatiwa na Mikoa ya Mara, Ruvuma, Morogoro na Kagera.

 “Ukatili wa kijinsia kwa kina mama na kina baba umeshamiri. Takwimu zinaonyesha kuwa Mkoa wa Dodoma unaongoza kwa asilimia 70.5 katika matukio ya wanaume kuwapiga wake zao, Mkoa wa Mara kwa asilimia 66.4 na Ruvuma kwa asilimia 50.8.”

Rushwa  Dk Bisimba alisema ripoti hiyo pia imeonyesha kuwa rushwa imekuwa bado tatizo nchini na sasa imeanza kuingia bungeni ambako baadhi ya wabunge wanahongwa ili kupitisha bajeti za wizara.  “Ripoti yetu inaonyesha kwamba kumekuwa na vitendo vya rushwa hadi ndani ya Bunge jambo ambalo linachangia  kuwanyima haki Watanzania hasa watu wa kipato cha chini kwani watu wachache wanafanya uamuzi kwa maslahi yao binafsi,” alidai Dk, Bisimba na kuongeza: 

“Miongoni mwa mambo ambayo yanaonyesha wazi kwamba rushwa imeingia mpaka ndani ya Bunge ni pale tuliposikia suala ya (David) Jairo (aliyekuwa Katibu Mkuu wa Nishati na Madini, na tuhuma za baadhi ya wabunge kuomba rushwa kwa wakurugenzi wa halmashauri,” alisema. 
Bisimba alisema ripoti hiyo imeeleza kuwa licha ya kuwepo vitendo vya rushwa ndani ya Bunge, vimekuwa pia vikionekana katika maeneo mengine kadhaa ikiwamo usafirishaji wa wanyama kupitia viwanja vya ndege, kwenye chaguzi pamoja na vyombo vya usalama.  “Ripoti inaonyesha kwamba suala la usafirishaji wanyamapori kupitia viwanja vya ndege mfano, Kiwanja cha Ndege cha Kilimanjaro (Kia) ndege 120 wanaojulikana kama species walipelekwa ughaibuni mwaka 2010. Hii yote inatokana na kusahau misingi ya haki za binadamu,” alisema.  Adhabu ya Kifo  Kuhusu adhabu ya kifo, Dk Bisimba alisema bado kuna changamoto kubwa ya kuhakikisha adhabu hiyo inaondolewa kwani ni moja ya kitendo kinachowanyima wananchi haki ya kuishi.

 Alisema kila Mtanzania ana haki ya kuishi, na kwamba adhabu ya kifo ni inakiuka misingi ya haki za binadamu ya kuishi.  “Mpaka sasa, asilimia 74 ya watu 600 walioshtakiwa na kuhukumiwa kifo, wanasubiri kunyongwa,” alisema.

Aidha, ripoti hiyo inaonyesha uwepo wa watumishi wachache katika vyombo vya kutolea uamuzi kuwa ni miongoni mwa mambo ambayo yanachangia kuwanyima haki wananchi.  Dk Bisimba alisema mpaka sasa, kuna mahakama 760 kati ya 1,000 zinazohitajika na mahakama za mwanzo 500 ambazo hazina mahakimu  Ripoti hiyo pia imeonyesha kuwepo kwa upungufu wa watumishi wa sekta ya afya kwa asilimia 68 ikisema watumishi waliopo ni asilimia 32.

Akizindua ripoti hiyo, Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba alisema Serikali inapaswa kuweka wazi matumizi ya rasilimali za taifa na kodi za wananchi ili wapate fursa ya kujua uhalali wa matumizi hayo na moyo wa kuendelea kuchangia maendeleo yao. 

“Ni vyema wanaohusika katika ufujaji wa fedha za Serikali wakachukuliwa hatua kwani hiyo ni mojawapo ya kuwanyima haki wananchi kwa kukosa maendeleo kutokana na kodi zao kutumiwa na viongozi wasio waadilifu,” alisema Profesa Lipumba.
KARIBU KATIKA WEBSITE YA KIJANJA, KUPATA HABARI MBALIMBALI ZA NDANI NA NJE YA NCHI. PIA UTAPATA MAMBO YA ACADEMIC. KARIBU SANA
 
Support : Creating Website | Johny Template | Mas Template
Copyright © 2011. GetInformedTz - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Mas Template
Proudly powered by Blogger