Home » » Vituko vya familia ya ngariba

Vituko vya familia ya ngariba

Written By Koka Albert on Sunday, July 29, 2012 | 12:00 AM

Wankyo Mwikwabe akiwa na mume wake Mwikabe Mwita Magesa.
WAILALAMIKIA SERIKALI KUZUIA UKEKETAJI,WADAI KAZI ILISAIDIA KUSOMESHA WATOTO
Anthony Mayunga
MKOA wa Mara ni miongoni mwa mikoa nchini inayotajwa kuongoza kwa matukio ya vitendo vya ukeketaji wanawake, hususan watoto wadogo.
Pamoja na juhudi za Serikali na mashirika mbalimbali ya kijamii kutoa elimu dhidi ya mila hizo potofu, bado vitendo hivyo viliendelea kufanywa, ama kwa siri au wakati mwingine hadharani kabisa.

Hata hivyo, juhudi hizo sa Serikali na mashirika binafsi zimeonesha kuzaa matunda kwa baadhi ya wahusika kukiri kuacha kufanya vitendo hivyo baada ya kupata elimu ya kutosha juu ya madhara ya ukeketaji kiafya.
Katika kijiji cha Nyanchabhakenye, Kata ya Kisumwa, Wilaya Rorya, mkoani Mara nakutana na Wankyo Mwikwabe (64) maarufu kama Chunguza.
Mama huyu amekuwa Ngariba kwa zaidi ya miaka 20, na baada ya kupata elimu ya kutosha juu ya athari za ukeketaji, sasa ameamua kustaafu kazi hiyo iliyokuwa ikimuingizia kipato. Hata hivyo uamuzi wake kwa upande mwingine umekuwa mwiba kwa familia yake, hasa mume wake, Mwikwabe  Mwita Magesa(66).

Bila kuficha hisia zake Magesa anasema, “Kama si mkazo wa Serikali kupiga marufuku ukeketaji, mke wangu alitakiwa kuendelea maana kazi hiyo ilisaidia kipato cha familia, tulisomesha watoto ,chakula kizuri lakini sasa ndivyo hivyo mmeishaamua tutafanyaje.”

Anabainisha kuwa, uamzi wa Serikali wa kupiga marufuku ukeketaji umepelekea athari kiuchumi kwenye familia hiyo lakini pia imekuwa changamoto ya kujipanga kuhakikisha familia haiyumbi kiuchumi.

“Mimi nilikuwa napata vitu kutoka kwa mke wangu, kila alipokwenda tuliongozana ,kama ni pombe akipewa ananipa, chakula tulitengewa kizuri maana aliheshimiwa sana kila anakopita,” anasema Magesa.

Anabainisha kuwa, kazi ya ungariba aliyokuwa akifanya mke wake, ilichangia kupata wateja wengi na mapato kuongezeka ambapo walifanikiwa kusomesha watoto.
Hatahivyo anasema hawakuweza kufanya mambo mengi ya maendeleo kwa kuwa fedha hizo zina masharti magumu .

“Mapato yatokanayo  na ukeketaji yana masharti magumu sana ,huwezi kununua mifugo wala kufanyia biashara zaidi ya kula na kuvaa ,yalitusaidia kusomesha hata watoto wetu…,sheria hizi zimetuathiri,”anasema.

Hata hivyo, Magesa anasema anakubaliana na uamuzi uliofikiwa na mke wake wa kuachana na kazi ya ungariba na kuomba Serikali kufanya utaratibu wa kuwawezesha mangariba waliokuwa wakitegemea kazi hiyo kuendesha maisha yao.

Mtoto wao, Mwita Mwikwabe(26), anasema kazi ya mama yake iliwasaidia kupata kipato kikubwa kwani yeye alikuwa akikodiwa kupiga muziki wa asili kila mama yake alipokuwa kwenye shughuli ya ukeketaji.

“Nilikuwa napata mialiko mingi sana na ikizingatiwa kuwa mama ndiye alikuwa ameshika soko la ukeketaji,nilikuwa nalipwa kati ya Sh100,000 hadi Sh150,000,” anasema.
Hata hivyo kijana huyo anabainisha kuwa muziki wake si mahususi kwa shughuli za ukeketaji pekee, na kuongeza kuwa alikuwa akipata mialiko mingi kupitia umaarufu wa mama yake.

Ngariba anena
Wankyo mwenyewe adai hakujua kama ukeketaji una madhara na kuongeza kuwa anajisikia amani sana kuachana na kazi ya ukeketaji baada ya kupata elimu kwa kuwa aliifanya kama kudumisha mila na desturi bila kujua madhara kwa aliokuwa akiwakeketa.

“Mimi niliwakeketa kwa utalaam na walikuwa wanapona haraka na wanawahi kuolewa na hata kuzaa mapema …nilipata sifa kubwa nikabatizwa jina la Chunguza kwa kuwa niliwachunguza na kuwatengeneza vizuri,” anasema mama huyo.

Kutokana na ongezeko la wateja anasema aliweza kupata kati ya kati ya Sh200,000 hadi 300,000 kwa msimu mmoja wa ukeketaji kwani alikuwa akitoza Sh5,000 kwa kila mtu. Anaongeza kuwa wanawake walioolewa walikuwa wakitozwa bei kubwa zaidi, tofauti na wale ambao walikuwa hawajaolewa. “Wanawake walioolowa na kuzaa niliwatoza Sh10,000 hadi Sh15,000 kwani ilikuwa kazi sana kuwatahiri kwasababu walishafanya tendo la ndoa tayari.

Kuwa Ngariba
Anasema ameanza kazi ya ungariba mwaka 1990  baada ya kile alichokieleza ni kusumbuliwa na ndoto za ajabu usiku. “Baada ya kudumu kwa ndoto hizo kwa muda, nilienda kwa kwenda kwa waganga wa jadi nikapiga ramli na kuniambia marehemu bibi yangu ndiye ananitaka nianze kazi yakukeketa,”anasema.

Aliowakeketa
Ngariba huyo anasema kwa miaka 10 aliyofanya kazi hiyo, ameshakeketa watoto na wasichana zaidi ya 2000. Anafafanua kuwa ameamua kuacha kazi ya ungariba baada ya Serikali kulivalia njuga suala hilo na kupiga marufuku vitendo vya ukeketaji, pia mafundisho ya dini yalichangia kumfanya aweke vifaa vya ukeketaji chini mwaka 2010.

 “Uamuzi wa kuacha uliridhiwa na familia kwa kuhofu kukamatwa na kufungwa kwa kuwa elimu ya kupinga vitendo hivyo ikawa kila kona,nikaamua kwenda Kanisa Katoliki huko Baraki nikaanza mafundisho ili nibatizwe,”anabainisha. Hata hivyo hajawahi kubatizwa kutokana na kufuatwa na mizimu kila wakati usiku na kumfanya akate tamaa.

“Shetani ananifuata sana nakunizuia kubatizwa, ananitaka niendelee kukeketa ,naomba  aniachie lakini ananibana sana sijui anataka nifungwe,”anasema kwa unyonge.
Share this article :

Post a Comment

KARIBU KATIKA WEBSITE YA KIJANJA, KUPATA HABARI MBALIMBALI ZA NDANI NA NJE YA NCHI. PIA UTAPATA MAMBO YA ACADEMIC. KARIBU SANA
 
Support : Creating Website | Johny Template | Mas Template
Copyright © 2011. GetInformedTz - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Mas Template
Proudly powered by Blogger