Home » » Sakata la Ulimboka latikisa Bunge

Sakata la Ulimboka latikisa Bunge

Written By Koka Albert on Tuesday, July 3, 2012 | 7:15 AM

MBILINYI AFANANISHA WALIOMTEKA NA JANJAWEED, WAZIRI NAGU AINGILIA KATI
Waandishi Wetu
KITENDO cha kutekwa nyara, kuteswa na kisha kuumizwa mwili mzima, kwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari Tanzania, Dk Steven Ulimboka jana kilitikisa Bunge huku wabunge wa CCM na Chadema wakitupiana mpira kuhusu nani waliohusika na tukio hilo.

Msuguano huo ulianza baada ya Mbunge wa Mbeya Mjini (Chadema), Joseph Mbilinyi kudai kuwa waliofanya kitendo hicho ni sawa na wanamgambo hatari wa Janjaweed wa Sudan.  

Kauli hiyo ya Mbilinyi maarufu kwa jina Sugu, ilizusha tafrani ndani ya Bunge kwani Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwezeshaji), Dk Mary Nagu aliomba mwongozo wa Mwenyekiti wa Bunge, Sylivester Mabumba aliyekuwa akiendesha Bunge jana jioni akihusisha matamshi hayo na kuituhumu Serikali kutumia watu kama Janjaweed katika kumteka Dk Ulimboka jambo ambalo alisema siyo la kweli.

Akichangia Hotuba ya Ofisi ya Rais, (Utumishi, Utawala Bora, Ikulu na Mipango) Mbilinyi alisema kitendo alichofanyiwa Dk Ulimboka ni cha kinyama na baadhi ya watu wanaamini kwamba Serikali ilihusika, hatua ambayo ilimfanya Dk Nagu kusema Mbilinyi alikuwa akizungumzia jambo ambalo hana uhakika nalo na kutaka aamriwe kuthibitisha.

Mwenyekiti Mabumba alimtaka Mbilinyi athibitishe kauli yake au aifute. Wakati Mabumba akimtaka Mbilinyi kuthibitisha au kufuta kauli yake, Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu alitaka kuingilia kati suala hilo na hata kuwasha kinasa sauti, lakini Mabumba alimwamuru akae chini.
Mbilinyi alipopewa nafasi alisisitiza: “Waliomteka Dk Ulimboka walikuwa na silaha kama siyo askari, basi hawana tofauti na kikundi cha Janjaweed ambacho kilifanya mauaji makubwa na kumfanya Rais wa Sudan, Omar Al Bashir ambaye sasa anatakiwa na Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai kuhusu kufanya uhalifu dhidi ya binadamu.”

Alifafanua kwamba, hakusema kama Serikali inatumia Janjaweed, bali alizungumzia namna Al Bashir alivyotumia wapiganaji hao kufanya uhalifu badala ya jeshi.
Hali hiyo ilizidi kuzua mvutano kati ya kiti cha Spika na Mbilinyi uliodumu kwa dakika tatu, huku Lissu naye akitaka apewe nafasi atoe hoja yake.

Baadaye Mabumba alitumia busara na kuamua kumalizia suala hilo kwa kumtaka Mbilinyi aendelee kuchangia na mbunge huyo wa Mbeya akiendelea kuzungumzia zaidi hilo, alitaka Bunge liunde tume ya uchunguzi kwa sababu hana imani na Serikali kuunda tume kuchunguza ukatili huo.

Baada ya Mbilinyi kumaliza, Mabumba alimtaka Lissu atoe dukuduku lake na aliposimama alimpinga Mwenyekiti huyo wa Bunge kwa maelezo kwamba alitumia kifungu kisicho sahihi kumwamuru Mbilinyi atoe maelezo ya kuthibitisha au kufuta kauli. Hata hivyo, alimtaka akae chini akisema: “Usitafute umaarufu hapa.”

Baadaye alisimama Mbunge wa Viti Maalumu (CCM) Stella Manyanya ambaye alikituhumu Chadema kwa kuchochea mgomo huku akidai kwamba kilihusika kumteka na kumjeruhi Dk Ulimboka.

Mbunge wa Ubungo (Chadema),  alikuja juu baada ya kauli hiyo akimtaka Mwenyekiti amtake Manyanya kuthibitisha au kufuta kauli yake. Badala yake, Mabumba alimtaka Mnyika kuthibitisha kwamba chama hicho hakihusiki.

Mnyika alisema Chadema hakihusiki na suala hilo na kueleza kwamba ripoti ya Kamati ya Bunge iliyoundwa kuchunguza mgogoro wa madaktari na Serikali inathibitisha hivyo, akitaka iwasilishwe bungeni na isomwe.

Mbunge wa Iramba Magharibi (CCM), Mwigulu Nchemba alisema Chadema kinaunga mkono mgomo wa madaktari akirejea hotuba ya upinzani bungeni iliyotolewa jana ikisema inawaomba wananchi kwa kushirikiana na madaktari kuiunga mkono Chadema kuishinikiza Serikali hadi wapate haki zao.

Manyanya alisimama tena na kudai kwamba hata waliomteka daktari huyo walikuwa wamevaa magwanda ambayo yanatumiwa na makada wa Chadema kauli ambayo iliibua mzozo huku wabunge wengi wa Chadema wakisimama kutaka kuzungumza.

Mwenyekiti Mabumba alilazimika kutumia dakika kadhaa kuwataka wabunge watulie na wakae chini lakini Mbunge wa Kasulu Mjini (NCCR-Mageuzi), Moses Machali alikataa kutii amri hiyo akitaka kuzungumza hali ambayo ilimfanya Mabumba kuamuru atolewe nje ya eneo la Bunge na kumtaka Manyanya aendelee kuzungumza.

Muhimbili utata mtupu
Wakati uongozi wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili ukisema huduma katika hospitali hiyo zimerejea katika hali ya kawaida baada ya madaktari kurejea kazini jana, madaktari bingwa wa hospitali hiyo nao wametangaza kuanza mgomo.

Taarifa iliyotolewa jana na msemaji wa uongozi wa Muhimbili, Aminiel  Aligaesha imesema wagonjwa wote waliolazwa wodini jana walihudumiwa na baadhi ya kliniki za huduma ya upasuaji zilifanyika na kuongeza: “Hata hivyo, upasuaji haukufanyika kwani hakukuwa na orodha ya wagonjwa waliopangwa kufanyiwa upasuaji.”

Lakini wakati uongozi wa Muhimbili ukisema hivyo, madaktari bingwa walikutana jana katika hospitali hiyo na kutangaza kuanza mgomo. Akizungumza muda mfupi baada ya kumalizika kwa mkutano wao uliofanyika katika hospitali hiyo, msemaji wao Dk Catherine Mng’ongo alisema:
“Sisi madaktari bingwa kufanya kazi bila Interns haiwezekani. Tungeanza kufukuzwa sisi kwanza. Kuanzia sasa hatutafanya kazi hadi hapo Serikali itakapokubali kuwarejesha wote kazini na kufungua meza ya majadiliano yenye nia ya dhati ya kumaliza mgogoro.”
Dk Mng'ong'o alisema zaidi ya madaktari 200, waliokuwa kwenye mafunzo ya vitendo Muhimbili na Taasisi ya Mifupa (Moi) wamepatiwa barua za kufukuzwa kazi na idadi yao nchi nzima inafikia 300.

Tamko la Rais Kikwete

Makamu Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari Tanzania , Dk Godbles Charles ameeleza kushangazwa na kauli ya Rais Jakaya Kikwete kuwa Serikali haihusiki katika sakata hilo na akidai ameingilia kazi ya tume iliyoundwa na Polisi kuchunguza tukio hilo.
“Je, ni sahihi kwa Rais kutamka waziwazi kuwa Serikali yake haihusiki kwa namna yoyote ile hata kabla ya ripoti ya uchunguzi?” alihoji Dk Charles.
Habari zilizopatikana jana zilieleza kuwa hali ya Dk Ulimboka inaendelea vizuri anakotibiwa Afrika ya Kusini.
Hospitali nyingine
Madaktari katika Hospitali ya Rufaa ya KCMC wamekubaliana na kuendelea na mgomo wakisubiri uamuzi wa mkutano mkubwa wa madaktari utakaofanyika leo.
Jumamosi iliyopita, uongozi wa KCMC uliwatimua madaktari zaidi ya 80 walioko kwenye mafunzo kwa vitendo na kuwataka wasionekane katika eneo la hospitali wala kukusanyika hapo.

Uongozi wa Hospitali ya Mkoa wa Arusha, Mount Meru, umelazimika kuitisha kikao cha pamoja na madaktari wa hospitali hiyo kwa lengo la kuwasihi waachane na mgomo.

Vyanzo vya habari hospitalini hapo, vilidai ya kwamba katika kikao hicho uongozi wa hospitali hiyo chini ya Mganga Mkuu Mfawidhi, ulilazimika kuitisha kikao siku moja baada ya tukio la Dk Ulimboka na kuwaangukia madaktari hao waachane na mgomo.

Huko Mbeya, Mkurugenzi wa Hospitali ya Rufaa Mbeya, Dk Eliuter Samky amesema utoaji huduma kwa wagonjwa siyo wa kuridhisha  kutokana na kuathirika kwa kiasi kikubwa kwa baadhi ya sekta muhimu.

Akizungumza mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Abbas Kandoro, Samky alisema mgomo huo umesababisha kuzorota kwa huduma kwa wagonjwa licha ya kusitisha huduma nyingine za kawaida na kubaki kuendelea kutoa huduma za dharura.

Habari hii imeandikwa na Leon Bahati, Geofrey Nyang’oro Aidan Mhando,Victoria Mhagama, Godfrey Kahango, Mbeya, Daniel Mjema, Moses Mashalla, Arusha.
Share this article :

Post a Comment

KARIBU KATIKA WEBSITE YA KIJANJA, KUPATA HABARI MBALIMBALI ZA NDANI NA NJE YA NCHI. PIA UTAPATA MAMBO YA ACADEMIC. KARIBU SANA
 
Support : Creating Website | Johny Template | Mas Template
Copyright © 2011. GetInformedTz - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Mas Template
Proudly powered by Blogger