Home » » Wanaosababisha mimba watakiwa kufika kliniki

Wanaosababisha mimba watakiwa kufika kliniki

Written By Koka Albert on Tuesday, June 5, 2012 | 3:58 AM

Fredy Azzah
WANAUME wanaowapa mimba wake zao ama vimada wametakiwa kwenda kliniki pamoja na wenza wao ili pamoja na mambo mengine wote wapime maambukizi ya virusi vya Ukimwi (VVU).

Mratibu wa mradi wa kuwahamasisha wanandoa hususani wanaume kupima virusi vya Ukimwi kutoka Kiwohede, Agnes Mandwa alisema hayo jana jijini Dar es Salaam katika tamasha la kuhamasisha upimaji wa VVU.

Alisema kitendo cha kuwatenga wanaume kwenye mipango mbalimbali ya afya ya uzazi ni moja ya sababu zinazochangia kuongezeka kwa utelekezwaji wa watoto pamoja na maambukizi ya virusi vya Ukimwi.
“Unasikia siku ya wanawake, siku ya wanawake na watoto na nyingine nyingi kama hizo, lakini hakuna zinazowashirikisha wanaume, hali hii inawafanya kuwa mbali na familia zao,” alisema Mandwa.

“Wakati mwingine wanaume wakishawapa wasichana mimba wanawakimbia, wanaenda kutafuta nyumba ndogo kama ni wanandoa ama kama ni wachumba wanawaacha kabisa, matokeo yake ni kuongezeka kwa watoto wa mitaani,”alisema.

 Alisema ni vyema wanaume wakashirikishwa katika mipango ya afya ya uzazi ili waweze kuwa karibu zaidi na familia zao.Alisema wanaume wakishirikishwa hata maambukizo ya VVU yatapungua kwani, itakuwa rahisi kwao kuepukana na kuwa na wapenzi wengi.

“Tafiti mbalimbali zinaonyesha kuwa, wanaume wanaongoza kwa kuwa na wapenzi wengi, kushirikishwa kwao katika mipango hii ni dhahiri  kutasaidia kupunguza maambukizo ya Ukimwi,” alisema Mandwa.
Alisema  hata sera mbalimbali za nchi zinamtenga mwanaume, huku akitolea mfano wa wanawake kutakiwa kupima VVU wakati wakienda kliniki, lakini mwanaume halazimiki kufanya hivyo.

Kwa upande wake Muganyizi Edward ambaye ni mmoja wa watekelezaji wa mradi huo unaojulikana kwa jina la Champion, alisema wanahamasisha wanandoa ama watu walio kwenye mahusiano kupima VVU ili iwe rahisi kudhibiti maambukizo mapya.

“Tunawahamasisha wapime wawili kama ni wanandoa ama wachumba ili kuweza kudhibiti maambukizo mapya, hawa pia tuna uhakika kwamba wanakutana mara kwa mara kimwili kwa hiyo ni vyema wakajua afya zao,” alisema Edward.Alisema kufanya hivyo kunawafanya kujiamini na kuwa na uangalifu zaidi kwa wenzi wao, jambo alilosema litasaidia pia kupunguza vifafa vya mimba.
Share this article :

Post a Comment

KARIBU KATIKA WEBSITE YA KIJANJA, KUPATA HABARI MBALIMBALI ZA NDANI NA NJE YA NCHI. PIA UTAPATA MAMBO YA ACADEMIC. KARIBU SANA
 
Support : Creating Website | Johny Template | Mas Template
Copyright © 2011. GetInformedTz - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Mas Template
Proudly powered by Blogger