Home » » CUF yataja suluhisho migomo ya walimu

CUF yataja suluhisho migomo ya walimu

Written By Koka Albert on Monday, August 6, 2012 | 12:09 PM


Geofrey Nyang’oro
MWENYEKITI wa Chama cha Wananchi (CUF) Profesa Ibrahimu Lipumba amewataka  walimu kuungana na chama hicho kuendesha harakati za kuondoa   CCM madarakani kwa kuwa imeonyesha wazi haina dhamira ya  kutekeleza madai yao.
Profesa Lipumba ambaye pia kitaaluma  ni mtaalamu wa  uchumi alisema chama chake kamwe hakiungi mkono mgomo, lakini kinatambua madai ya walimu na umuhimu wa kuyatatua.

Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, alisema ingawa katika Ilani ya CCM na hata ahadi  za viongozi wake zilieleza bayana kuwa ingeboresha masilahi ya wafanyakazi, hotuba ya Rais Jakaya Kikwete ya Agosti Mosi mwaka huu inadhihirisha kuwa CCM haina nia hiyo.


“Katika hotuba ya Rais  ya mwishoni mwa mwezi Julai mwaka huu iliyosomwa mbele ya wahariri wa vyombo vya habari Agositi mosi, sehemu ya hotuba inasema madai ya safari hii ni makubwa mno,yametuzidi kimo.Athari za kuyatekeleza yalivyo yataifanya serikali kutumia asilimia 75 kwa ajili ya mishahara”alisema  Profesa Lipumba akinuuu hotuba ya Rais Kikwete na kuongeza:

“Ukiangalia nukuu hizi,zinathibitisha dhana ya serikali ya CCM katika kutekeleza madai ya walimu,Rais hataji serikali ina mpango gani na kwa kiasi gani itatekeleza mipango hiyo,serikali isiyo na mipango kwa vyovyote vile haiwezi kuwatumikia wakulima na wafanyakazi wa nchi yetu”alisema.
“Sisi (CUF) tunawashauri walimu watambua kuwa CCM haipo madarakani kutatua matatizo yao,muhimu walimu wakaungana wote ili kuhakikisha CUF inaongoza dola na kuleta mabadiliko.
Profesa Lipumba alisisitiza kuwa migogoro inayoendelea hapa nchini ni  uthibitisho wa kuwapo kwa ombwe la uongozi uliojikita katika ,usiri, uzembe, dharau na ubabe.
“Inasikitisha kwamba mvutano kati ya serikali na walimu hauishi, mazingira ya kuaminiana katika kutatua mgogoro, serikali ya CCM haiwezi kutatua kero za walimu na kuwapa motisha wa kuboresha elimu kwa watoto wetu”alisema Lipumba.
Msimamo wa CUF kuhusu mgomo
Mwenyekiti huyo wa CUF alisema chama chake ingawa hakiamini kuwa mgogoro unaweza kumalizwa kwa migomo kinaunga mkono madai ya walimu kuwa ni ya haki.
“Pamoja na kuwa (CUF) hakiamini migomo ya wafanya kazi kama suluhisho la kuisha kwa matatizo yao na bila kuingilia maamuzi ya mahakama tunasisitiza kuwa walimu wana madai sahihi na yanapaswa kupewa kipaumbele”alisema.

Alisema walimu wanafanya kazi katika mazingira mgumu wakati serikali ya CCM inayojiita sikivu haijawasikiliza na kutekeleza madai yao zaidi ya kutishia kuwafukuza kazi na kuwakamata baadhi kuhusiana na mgomo.
Alisema chama chake kilitegemea Rais Kikwete angetoa kauli mahsusi ya mpango maalumu wa kushughulikia madai yao lakini imekuwa tofauti baada ya kusema serikali yake haina uwezo wa kutekeleza.

Lipumba alisema majibu ya Rais Kikwete yalijumulisha madai ya ongezeko la mishahara ya walimu na kuwa ongezeko la wafanya kazi wote serikalin ambalo linafanya kufikia asimilia 75 aliyosema haiwezekani.
Athari za mgogoro wa walimu
Katika mkutano huo Profesa Lipumba alisema athari zitokanazo na mgogoro baina ya walimu na serikali ni kubwa zitakazoweza kudhoofisha juhudi za kujinasua kutoka katika  dimbwi la umasikini.

“Kama walimu wataendelea kulipwa namna hii,ina maana ualimu ni wito na si taaluma kama zilivyo taaluma nyingine muhimu, tusishangae kuwa walimu wetu wataendelea kuuza bagia badala ya kufundisha kwa kuwa kipato chao hakitoshi”alisema.


Alisema tayari kumekuwa na athari kuwa nchini za kuporomoka kwa elimu na kwamba hayo ni matokeo ya serikali kushindwa kuboresha mazingira ya elimu ikiwamo mishahara na vitendea kazi.


“Hivi sasa tumepiga hatua katika suala zima la uandikishaji wanafunzi ambapo tumetoka asilimia 51 mwaka 1990 na kufikia asilimia 97 mwaka 2009,lengo la kuandika watoto wote wenye umri wa kuanza darasa la kwanza limefikiwa tatizo ubora wa elimu”alisema Lipumba.


“Utafiti wa uwezo uliofanywa na Taasisi isiyo ya kiserikali umebaini kuwa watoto watano wanaomaliza darasa la saba mmoja kati yao hawezi kusoma hadithi ya ngazi ya darasa la pili, katika kipindi cha miaka saba watoto hao wanaelekea kubaki mbumbumbu (hawajui kusoma wala kuandika)maishani mwao….”alisema Lipumba.


Profesa Lipumba alisema ni muhimu kuboresha elimu ya Msingi ili wanaoingia shule iweze kuwasaidia na kwamba ikiwa hatutafanya hivyo taifa liko hatarini kurejea kwenye elimu ya watu wazima (UPE) kama ilivyokuwa miaka ya 80.


Alisema kukua kwa uchumi wa  kisasa na wenye uwezo kuboresha maisha ya wananchi kunategemea wafanya kazi wenye ujuzi na maarifa na kwamba yote yanatokana na elimu bora.

Hivi karibuni Chama cha Walimu Tanzania (CWT)kilitangaza mgomo wa walimu nchi nzima na usio na ukomo uliodumu kwa siku tatu kabla ya kubatilishwa na mahakama.
Share this article :

Post a Comment

KARIBU KATIKA WEBSITE YA KIJANJA, KUPATA HABARI MBALIMBALI ZA NDANI NA NJE YA NCHI. PIA UTAPATA MAMBO YA ACADEMIC. KARIBU SANA
 
Support : Creating Website | Johny Template | Mas Template
Copyright © 2011. GetInformedTz - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Mas Template
Proudly powered by Blogger