Home » » Malawi kutopigana na Tanzania

Malawi kutopigana na Tanzania

Written By Koka Albert on Friday, August 10, 2012 | 11:33 PM

MALAWI imesema imeondoa ndege zake zilizokuwa zikifanya utafiti wa mafuta katika Ziwa Nyasa kwa kuwa haitaki kuingia vitani, badala yake imeamua kupeleka mgogoro huo Mahakama ya Kimataifa.

Kauli hiyo ilitolewa juzi na Waziri wa Mambo ya Ndani na Uhusiano wa Kimataifa kwa Mambo ya Kiusalama wa Malawi, Uladi Mussa alipokuwa akizungumza na gazeti linalochapishwa nchini humo la Nyasa Times.

“Nawahakikishia wananchi mtaendelea kuishi kwa utulivu. Tupo kwenye mazungumzo na Serikali ya Tanzania, bila shaka mambo yataenda vizuri. Kama hali ikishindikana tutalipeleka suala hili kwenye Mahakama ya Haki ya Kimataifa,” alisema Mussa.

Kauli ya Waziri huyo imekuja wakati baadhi ya wananchi wa Malawi wanaoishi katika Vijiji vya Karonga na Chitipa vilivyopo kando ya Ziwa Nyasa upande wa Malawi wakiwa wameanza kuvihama vijiji hivyo kuhofia usalama wa maisha yao.

Baadhi ya wakazi hao wamekaririwa na Nyasa Times wakisema kuwa wameamua kuchukua hatua hiyo kunusuru maisha kutokana na kuwapo kwa dalili za kutokea vita kati ya Malawi na Tanzania.
Waziri Mussa amesema suala hilo la mgogoro wa mpaka litaamuliwa kwa njia ya amani na hivyo kuwataka wananchi kuendelea na shughuli zao bila wasiwasi.

Waziri huyo aliwahakikishia wananchi hao kuwa Serikali ya Malawi ina ushahidi wa kutosha kuwa ziwa lote la Malawi (Nyasa)ni mali ya Malawi na Tanzania haina nguvu ya kuwasimamisha kuendelea na kazi ya kutafuta mafuta.

“Kimsingi hapa hakuna hoja ya kubishania. Wote tunajua ziwa hili ni mali yetu (Malawi),” alisema.
“Kama malalamiko haya yangekuwa yametolewa na Msumbiji, hapa tungekuwa na hoja ya kubishania, lakini si Tanzania.” alisisitiza.

Alisema ushahidi wao wa mipaka ni wa tangu mwaka 1890 wakati ambako wakoloni wa Uingereza na Ujerumani walitiliana saini juu ya suala hilo.

Aliendelea kueleza kuwa umiliki huo wa ziwa  umeongezewa nguvu na maazimio ya mwaka 1963 ya Wakuu wa uliokuwa Umoja wa Nchi Huru za Kiafrika (OAU) kwamba wanachama wanapaswa kuheshimu mipaka waliyorithi kwa wakoloni.

Kauli za wananchi
Wakati Serikali ya Malawi ikitoa msimamo huo watu kadhaa waliohojiwa wameonyesha hofu ya nchi hizo kuingia katika vita.

Heckley Christopher ambaye ni raia wa Malawi anayefanya biashara eneo la Mbambabay mkoani Ruvuma anasema: " Malawi ni nchi ndogo sana kupigana na Tanzania, ni nchi yenye mikoa minne tu, kukiwa na vita itaangamia mara moja."

Raia mwingine wa Malawi ni Vilion Gordon ambaye alisema Tanzania na Malawi ni marafiki wa siku nyingi, hivyo hawana sababu za kugombania ziwa ambalo lilikuwapo tangu enzi hizo.

"Nashauri wakae chini wapatane, kwa nini tugombane sasa wakati ziwa hilo lilikuwapo tangu enzi hizo?"alisema.

Mtanzania mkazi wa Kijiji Lundo kilichoko Mbambabay mkoani Ruvuma, Zakhia Chengula ameitaka Serikali ya Tanzania kuendelea kuimarisha ulinzi na kukubali kuingia katika mazungumzo na Malawi badala ya kufikiri vita.

"Hapa sisi ni kwetu, vita ikiingia sisi tutakufa tu hakuna pa kukimbilia. Tunaiomba Serikali iimarishe ulinzi eneo hilo na ikae na Malawi kuzungumzia mgogoro huo," alisema.

Mkuu wa Wilaya mpya ya Nyasa, Ernest Kahindi alisema hakuna hofu yoyote kwa wakazi wanaoishi kando ya Ziwa Nyasa upande wa Tanzania.
Amewataka wananchi hao kuendelea na shughuli zao za uzalishaji mali kama kawaida kwani suala hilo sasa linashughukiliwa kitaifa.

"Mwanzoni kulikuwa na hofu kubwa, lakini baada ya Serikali ya Tanzania kutoa tamko la kutaka ndege za Malawi ziondoke na zenyewe kutii amri hiyo, hakuna tatizo lolote," alisema na kuendelea;
"Shughuli katika eneo hili zinaendelea kama kawaida. hakuna mwananchi aliyepigwa risasi wala ndege iliyotunguliwa, mambo yako shwari."
Jeshi laimarisha ulinzi

Katika hatua nyingine Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), limeimarisha ulinzi katika mwambao wa Ziwa Nyasa na kupiga marufuku wananchi kukatisha eneo lao la jeshi.
Share this article :

Post a Comment

KARIBU KATIKA WEBSITE YA KIJANJA, KUPATA HABARI MBALIMBALI ZA NDANI NA NJE YA NCHI. PIA UTAPATA MAMBO YA ACADEMIC. KARIBU SANA
 
Support : Creating Website | Johny Template | Mas Template
Copyright © 2011. GetInformedTz - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Mas Template
Proudly powered by Blogger