Home » » Mahakama yapiga ‘stop’ mgomo wa walimu

Mahakama yapiga ‘stop’ mgomo wa walimu

Written By Koka Albert on Friday, August 3, 2012 | 2:52 AM


Rais wa Chama cha Walimu Tanania (CWT), Gratian Mukoba akiwa ameambatana na baadhi ya walimu wakati wakitoka Mahakama kuu, kitengo cha kazi jijini Dar es Salaam jana kusikiliza maamuzi ya mahakama hiyo kuhusu kesi yao dhidi ya Serikali. Mahakamama ilisitisha mgomo wa walimu ikidaiwa kuwa ni batili. Picha na Venance Nestory
MAHAKAMA Kuu ya Tanzania, Kitengo cha Kazi imesitisha mgomo wa walimu na kuwataka kurudi kazini mara moja.
Mahakama hiyo pia imeuagiza uongozi wa Chama cha Walimu (CWT) kuandaa taarifa kwa umma, kutangaza kusitishwa kwa mgomo huo kama walivyowatangazia wanachama wake wakati ulipoanza.

Mahakama hiyo ilisitisha mgomo huo jana wakati ilipotoa uamuzi wa maombi yaliyowasilishwa mahakamani na Serikali. Jaji Sophia Wambura aliyekuwa akisikiliza maombi hayo, alisema mgomo huo ni batili kwa kuwa haukukidhi masharti ya Sheria ya Ajira na Uhusiano Kazini.

Katika uamuzi wake, mahakama hiyo pia imekitaka CWT kulipa hasara za kifedha au kuwafidia wanafunzi vipindi vya masomo walivyovikosa, hususan wale wa darasa la saba. Mahakama hiyo ilikwenda mbali zaidi na kuwaonya walimu na Serikali kwa kitendo cha kuzungumzia suala hilo wakati tayari lilikuwa mahakamani.

Jaji Wambura alisema kitendo hicho ni uvunjaji wa Ibara ya 4 na ya 107 A ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya  mwaka 1977 kama ilivyokwisha kurekebishwa mara kadhaa.

“Vinginevyo, hakukuwa na haja ya kuja hapa mahakamani kabisa. Kama kila mmoja ataachwa awe jaji, itakuwa ni kero na uvunjaji wa utawala wa sheria,” alisema Jaji Wambura.

Jaji huyo alizitaka pande zote kurudi kwenye meza ya mazungumzo na kushauri kuwa, ikiwezekana zialike watu wenye ujuzi wa masuala ya sheria za kazi na uhusiano kazini kuwasaidia ili kufikia makubaliano kwa  amani.

“Chini ya Masharti ya Kifungu cha 81 (1) (2) cha Sheria ya Ajira na Uhusiano Kazini, natamka kuwa mgomo ambao umekuwa ukiendelea kwa siku tatu sasa ni kinyume cha sheria. Ninaamuru usitishwe na walimu wote warudi kazini mara moja,” aliagiza Jaji Wambura.

Msingi wa uamuzi
Jaji Wambura alirejea hoja zilizowasilishwa na pande zote, waombaji wakiwakilishwa na Mawakili wa Serikali Wakuu, Obadia Kameya na Pius Mboya na wajibu maombi (CWT) wakiwakilishwa na Wakili Gabriel Mnyele.

Alisema baada ya kupitia hoja zote na vielelezo vilivyoambatanishwa kwenye hati za viapo pamoja na majibu husika, amebaini kuwa na kuridhika kuwa mgomo huo haukufuata sheria.

Alisema CWT hawakufuata masharti ya kifungu cha 80 (1), cha Sheria ya Ajira na Uhusiano Kazini na kwamba kulikuwa na dosari kwani kura zilizopigwa zilipotosha wanachama , kwa sababu hazikuwa za kuunga mkono mgomo, bali madai ya walimu.

Jaji huyo alisema upigaji kura ulikuwa ni batili kwani walimu hawakufahamishwa matokeo ya mgomo huo na kwamba haukuzingatia taratibu.

Pia alisema taarifa ya mgomo iliyowasilishwa kwa Katibu Mkuu Kiongozi Julai 27, 2012 saa 9:00 alasiri wakati mchakato wa upigaji kura ukiwa unaendelea, pia ilikuwa ni batili.

Dosari nyingine ni kutoeleza kikomo cha mgomo na kutokubainisha kama watawalipa wanachama wake wakati wa mgomo.

Aliongeza kwamba, CWT kwa kushindwa kutimiza masharti ya kanuni ya 42 na 43 za sheria husika, kulisababisha kero zisizo za lazima.

Alisisitiza kuwa kitendo cha CWT kuwasilisha taarifa ya mgomo Ijumaa saa 9:00  wakidai  mgomo unaanza Jumatatu, hali wakijua kuwa Jumamosi na Jumapili hazikuwa siku za kazi, ni kinyume cha kanuni na kilifanywa kwa nia mbaya.

Wakili wa CWT, Mnyele alisema anasubiri maelekezo ya wateja wake, lakini Rais wa CWT, Gratian Mukoba alisema watatoa tamko leo.

Mgomo waendelea
Katika baadhi ya shule za Dar es Salaam jana mgomo uliendelea na kusababisha wanafunzi kadhaa kuonekana wakizurura mitaani.

Shule hizo zimo za sekondari na  msingi ambazo ni Mchangani, Mwananyamala Kisiwani, Kunduchi, Pius Msekwa, Pwazo, Pwani, Mtakuja, Mtongani na Kisauke katika manispaa ya Kinondoni.

Walimu walioonekana maeneo ya shule hizo walikuwa wachache huku wanafunzi nao wakionekana wakisambaa hovyo katika maeneo ya shule.

Baadhi ya wanafunzi walikiri kwamba mahudhurio yao pia yamezorota.

Mwalimu Mkuu Msaizi wa Shule ya Msingi Mwananyamala Kisiwani, Abwalib Mfinanga alisema; “Kama unavyoona, walimu hawaingii madarasani kufundisha kutokana na mgomo unao endelea.”

Katika Manispaa ya Temeke baadhi ya wanafunzi wa darasa la saba walisikika wakilalamika kutotendewa haki.

“Walimu wetu wamesoma na sisi tunataka tuwe kama wao, tunawaomba  watufundishe  ili tuweze kufikia kiwango kama chao,” alisema mwalimu Alfred Mwinuka.

Katika shule ya Msingi Amani wanafunzi walionekana wakicheza katika viwanja vya michezo na  wakati katika shule ya Msingi ya Dovya, baadhi ya madarasa yalikuwa yamefungwa huku baadhi ya  wanafunzi wakiwa wamezagaa nje.

Mwanafunzi Saleh Juma alisema kuwa jana ni mwalimu mmoja tu aliyeingia darasani, na baada ya muda mfupi aliondoka. Mwalimu Mkuu peke yake ndio tunamuona akipita madarasani,” alisema Saleh.
Share this article :

Post a Comment

KARIBU KATIKA WEBSITE YA KIJANJA, KUPATA HABARI MBALIMBALI ZA NDANI NA NJE YA NCHI. PIA UTAPATA MAMBO YA ACADEMIC. KARIBU SANA
 
Support : Creating Website | Johny Template | Mas Template
Copyright © 2011. GetInformedTz - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Mas Template
Proudly powered by Blogger