Home » » SUNZU AWAPIKU TWITE, OKWI KUCHAFUKA PESA

SUNZU AWAPIKU TWITE, OKWI KUCHAFUKA PESA

Written By Koka Albert on Monday, October 15, 2012 | 2:21 AM
MICHAEL MOMBURI
FELIX Sunzu wa Simba anaongoza katika Ukanda wa Afrika Mashariki kuwa mchezaji wa kigeni anayelipwa mshahara mkubwa zaidi, huku straika mwenzake Emmanuel Okwi akishika mkia miongoni mwa wageni wa klabu hiyo.

Wakati ukiendelea kushangaa, unapaswa kutambua kuwa Mbuyu Twite wa Yanga anaongoza katika klabu ya Yanga, huku Hamisi Kiiza ambaye ni raia wa Uganda kama Okwi akishika mkia kwa wageni wa klabu hiyo ya Jangwani.

Mwanaspoti imefanya uchunguzi kwa wachezaji wa kigeni walioko klabu kubwa za Tanzania (Simba na Yanga), Rwanda (APR na Rayon) na Kenya (AFC, Gor Mahia na Sofapaka).

SIMBA
Uchunguzi ndani ya Simba umebaini kuwa straika Mzambia Felix Sunzu analipwa Dola 3,500 (Sh.5.5 milioni) akifuatiwa na beki Komanbilli Keita wa Mali na mshambuliaji Daniel Akuffo wa Ghana ambao kila mmoja analipwa Dola 1,000 ambazo ni sawa na Sh.1.6 milioni..

Beki Mkenya, Paschal Ochieng analipwa Sh.1.2 milioni sawa na straika mpambanaji Okwi anayelipwa Dola 800 ambazo ni sawa na Sh. 1.2 milioni.

Mishahara hiyo ukiondoa wa Ochieng anayelipwa kwa fedha ya Kitanzania inaweza kuongezeka kidogo kulingana na thamani ya Dola ya Marekani kwa mwezi husika lakini bado Okwi anabaki chini miongoni mwa wachezaji wa kigeni wa Simba.

Kwa mujibu wa makubaliano ya mkataba, mshahara ni maelewano baina ya pande mbili. Ochieng, Akuffo na Keita wana deni kubwa kwa Simba kuliko ilivyo kwa Okwi na Sunzu ambao wanatisha katika kikosi cha kwanza cha Kocha Milovan Cirkovic.

Keita, Akuffo na Ochieng hawana namba kwenye kikosi cha kwanza baada ya kupokwa na wazalendo walionyesha kujiamini na uwezo mkubwa wa kuisaidia timu.

Ingawa Milovan ana siri kubwa moyoni kwa atakachofanya kwenye dirisha dogo, amesisitiza kuwa bado atawapa nafasi wachezaji hao kulingana na juhudi zao.

Kwa mujibu wa hesabu hizo kwa mwezi Simba inalazimika kulipa Dola 7,300 kama mishahara peke yake kwa wachezaji wa kigeni ambazo ukizidisha kwa mwaka mzima klabu hiyo italipa fedha za Kitanzania Sh 136 milioni. Hizo hazihusishi posho za wachezaji hao timu inaposhinda pamoja na gharama nyingine za papo kwa hapo ikiwamo usafiri na nyumba.

YANGA
Mkongomani, mwenye uraia wa Rwanda, Mbuyu Twite anaongoza orodha kwa kulipwa Dola 2,500 sawa na Sh.3.8 milioni akifuatiwa na Mnyarwanda Haruna Niyonzima na Yaw Berko wa Ghana wanaokinga Dola 1,500 kila mmoja ambazo ni sawa na Sh.2.4 milioni.

Straika wa Burundi, Didier Kavumbagu analipwa Dola 1,200 sawa na Sh.1.9 milioni huku Kiiza wa Uganda akishikilia nafasi ya mwisho kwa wageni kwa kulipwa Dola 1,000 ambazo ni Sh.1.6 milioni.

Tofauti na ilivyo kwa Simba, mastaa wa kigeni wa Yanga wamekuwa wakicheza karibu kila mechi na mara kadhaa wamejikuta wote wakianza ingawa bado mashabiki hawajavutiwa na kiwango cha soka kuendana na majina na uzoefu wa wachezaji hao wa kigeni.

Yanga kwa wageni watano inalazimika kuwalipa Dola 7,700 kwa mwezi ambazo ukipiga hesabu ya mwaka mzima ni Dola 92,400 ambazo ukizibadili kwa fedha za Tanzania ni Sh 145 milioni.

Gharama hizo hazihusishi pia posho, usafiri gharama ndogondogo ikiwamo tiketi za kwenda na kurudi na familia zao.

Kenya na Rwanda
APR ya Rwanda ndiyo iliyokuwa ikilipa mishahara mikubwa lakini imetimua wachezaji wote wa kigeni na kujipanga upya kwa kutumia wazalendo. Klabu nyingine zenye mashabiki wengi nchini humo za Rayon na Kiyovu zimesajili wachezaji kutoka DR Congo na Burundi lakini zinawalipa mishahara ya kawaida kama wazalendo.

Nchini Kenya, Mnyarwanda Jonas Nahimana wa AFC Leopard analipwa Ksh.80,000 sawa na Sh. 1.4 milioni ambazo ni mshahara sawa na wa Mkongomani Robert Binja wa Sofapaka.

Ivan Anguyo na Danny Serunkuma ambao ni raia wa Uganda wote wakiichezea Gor Mahia ndio wanaolipwa Ksh.70,000 ambazo ni Sh. 1.3 milioni.

Kipa Mtanzania Ivo Mapunda anayeichezea Gor Mahia naye ameongezewa mshahara na kufikia Ksh.60,000 ambazo ni Sh 1.1 milioni.
Share this article :

Post a Comment

KARIBU KATIKA WEBSITE YA KIJANJA, KUPATA HABARI MBALIMBALI ZA NDANI NA NJE YA NCHI. PIA UTAPATA MAMBO YA ACADEMIC. KARIBU SANA
 
Support : Creating Website | Johny Template | Mas Template
Copyright © 2011. GetInformedTz - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Mas Template
Proudly powered by Blogger