Mh Peter Kallaghe akiwa katika picha ya pamoja na timu nzima ya
TWENDE PAMOJA. Kutoka kushoto Lee Patterson, Mike Knox (Director)
Wilfred Moshi, Mary Iannarelli, Fiona Macpherson na Veronica Avinou
Mike Knox mwanzilishi wa Twende Pamoja akifanya mazungumzo na Urban Pulse
Mwanzilishi wa Twende Pamoja Mike Knox akila pozi na Frank Eyembe wa Urban Pulse Edinburgh, Scotland
Wilfred Moshi akipeperusha bendera ya Tanzania kileleni Mlima Everest
Wilfred Moshi safarini kuelekea kileleni.Picha
zote hisani ya Wilfred Moshi na Urban Pulse
Imeandikwa
na Freddy Macha kwa ushirikiano na Urban Pulse
Kwa mara ya kwanza kabisa katika historia ya nchi yetu
kijana Wilfred Moshi, Mbongo wa kawaida tu (anayefanya kazi ya upagazi kuwahudumia
watalii wanaopanda mlima Kilimanjaro), ameweka rekodi mpya ya kuwa Mtanzania wa
kwanza kupanda Everest - mlima mrefu kushinda yote duniani.
Hivi karibuni, Moshi, alialikwa majuma matano nchini Uingereza
kutembelea shule mbalimbali za Scotland akakutana na takribani wanafunzi 5,000
.
Wanafunzi walitaka kufahamu namna alivyopanda
mlima Everest wenye mita 8,848 (futi 29, 029). Mlima huu mgumu kuukwea kuliko
yote ulimwenguni umewahi kupandwa na na watu 4,000 toka ulipoanza kufikiwa
kileleni na Edmund Hillary na Sherpa Tenzig Norgay mwaka 1953. Kati ya hao 200
walifariki. Mwaka huu wanne wameshafariki wakiijaribu shughuli hii
inayochukua miezi miwili na kugharimu
Dola 100,000 (Shilingi milion 157,500,000) Linganisha na mlima Kilimanjaro unaodai siku tano na gharama (ikiwepo vifaa husika) Dola
2,000 (Shilingi milioni 3, 161).
Wilfred Moshi ni Mtanzania wa kwanza na Mwafrika
wa tatu kufikia kilele cha kitendawili hiki Mei 19 2012 (kilichoitwa “Chomolungma” na
wenyeji kabla ya kubatizwa jina la Everest na Waingereza enzi za ukoloni)
Wilfred aliyezaliwa mwaka 1979 na kumaliza kidato
cha sita shule ya Kilimanjaro Boys, amekuwa akipanda mlima Kilimanjaro tangu
angali bado shuleni na miaka 19.
Mara baada ya kuwasili Edinburgh, Scotland
alikaribishwa bungeni akakutana na Waziri wa Sheria mheshimiwa Kenneth
MacAskill na viongozi wengine. Safari ilikirimiwa na shirika la “Twende Pamoja”
lililoanzishwa na Mike Knox miaka 30 iliyopita. “Twende Pamoja” imejenga
ushirikiano kati ya wanafunzi wa Scotland na shule 34 za Kitanzania. Ni moja ya mashirika,
watu binafsi na wafadhili mbalimbali ulimwenguni waliochangia fedha za
kumwezesha Moshi kupanda mlima Everest.
Balozi wetu Uingereza, Mheshimiwa Peter Kallaghe
vile vile alisafiri toka London kumtembelea Wilfred Moshi na kumpa heko. Umbali
wa London had Scotland ni kama Dar es Salaam hadi Kigoma!
Kwanini Moshi anahusudu kupanda milima?
Ukweli sisi bado hatuoni umaana (au umuhimu) wa
kupanda milima. Anasema lengo lake lilikuwa kutimiza ndoto ya Mtanzania wa
kwanza kupanda Everest. Pili, upandaji milima ni moja ya njia zinazoweza
kusaidia kujenga jamii kwa misaada na fadhila za mashirika yasiyo ya kiserikali
(NGO). Tujiulize vipi alisaidiwa na watu wengi namna hiyo kuchangia fedha
takikana? Tatu, Moshi amethibitisha ukiwa na moyo na jitihada unaweza kufanya
lolote. Ushujaa na ushupavu wake utasaidia kuwahamasisha Watanzania kuwa
ukitaka kufanya jambo lolote lile unaweza ili mradi uwe na moyo na nidhamu.
Mpanda milima mashuhuri, Mike Hamill, aliyeshakwea
milima yote mikubwa saba duniani anasema
katika kitabu chake kipya (“Climbing Seven Summits”) wapanda milima ni watu
wenye moyo wa kufikia malengo na kufanikiwa katika maisha yao.
Akiwa Uingereza Moshi alipanda mlima wa Ben Nevis
mrefu kuzidi nchi hii-
wenye mita 1,344 (futi 4, 409). Baada ya kuimudu milima mitatu
sasa , Wilfred Moshi ameazimia kupanda milima katika mabara yote 7 duniani.
Anasema amebakisha milima mitano: Aconcagua ( Marekani ya Kusini ), Kosciuszko
(Australia), Vinson Massif ( Antarctica) McKinley(Alaska) na Elbrus(Urusi).
Mungu ambariki Mtanzania huyu mwenye jazba na
hamasa anayetuletea sifa.
+ comments + 1 comments
safi sana
Post a Comment