Home » » Bomoabomoa ya Magufuli yazua vurugu Dar

Bomoabomoa ya Magufuli yazua vurugu Dar

Written By Koka Albert on Wednesday, April 4, 2012 | 2:14 AM

Dotto Kahindi
POLISI wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU), jana walitumia mabomu ya machozi kutawanya mamia ya wafanyabiashara ndogondogo maarufu kama Wamachinga, waliofunga Barabara ya Mandela kwa mawe na kuchoma matairi ya magari kupinga utekelezaji wa agizo la Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli la kuwaondoa kwenye hifadhi ya barabara.

Mwezi uliopita akizundua Kituo cha Mabasi cha Mbezi mwisho, Dk Magufuli alitangaza operesheni safisha jiji iliyolenga kuwaondoa wote waliovamia hifadhi ya barabara na akisisitiza: "Hata mkikuta milingoti ya bendera za CCM ng'oeni."

Jana, utekelezaji wa agizo hilo ulizua vurugu katika eneo la Ubungo ikiwamo Kituo Kikuu cha Mabasi yaendayo mikoani (UBT) na kusambaa katika maneo jirani na makutano ya Barabara za Morogoro, Mandela na Sam Nujoma.

Vurugu hizo zilizodumu kwa saa kadhaa, zilizua taharuki, msongamano wa magari na kuvuruga kwa muda mfumo wa usafiri katika vituo vya mabasi vya Mwenge, Magomeni, Buguruni na Tazara.

Katika vurugu hizo, ofisi 10 katika eneo la Ubungo nazo zilijikuta katika msukosuko ambapo zililazimika kuongeza ulinzi kutokana na hofu ya Wamachinga hao kuvamia na kuingia ndani ya ofisi hizo.

Taasisi zilizolazimika kuongeza ulinzi ni Kampuni ya Kuzalisha na Kusambaza Gesi Asilia (Songas), Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), Kituo cha Mabasi Ubungo (UBT), Shirika la Viwango Tanzania (TBS), benki za NMB na NBC, Kiwanda cha Kibuku na Wizara ya Maji.

Operesheni hiyo ya kuwahamisha kwa nguvu wafanyabiashara hao ilianza mapema asubuhi lakini, kadri muda ulivyokuwa ukienda, vurugu ziliongezeka.

Hatua ya polisi kutumia mabomu ya machozi ilikuja muda mfupi baada ya wafanyabiashara hao kukaidi kuondolewa na kuamua kufunga Barabara ya Mandela kwa kuweka mawe eneo la Riverside na kuzuia magari yasipite.

Baada ya tukio hilo, askari wa FFU walilazimika kutumia nguvu za zaidi kwa kufyatua mabomu ya machozi kuwatawanya wafanyabiashara hao waliokuwa wakisema hawako tayari kuhama.

Kurushwa kwa mabomu hayo ya machozi kuliwasambaratisha wamachinga hao walioanza kukimbia huku na kule, baadhi wakibeba bidhaa zao, wengine kuzitelekeza na kuwafanya askari wa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni waliokwemo kwenye operesheni hiyo, kuzichukua kirahisi.

Baada ya wafanyabiashara hao kusambaratika, polisi walifika katika eneo hilo na kuanza kuondoa mawe hayo na kufanikiwa kuwakamata watu 15 waliodaiwa kuhusika na vurugu hizo.

Hata hivyo, wakati polisi wakifikiri kwamba vurugu zimetulia, mchana wamachinga hao waliibuka ghafla na kuanza kuchoma matairi hovyo barabarani.
Share this article :

Post a Comment

KARIBU KATIKA WEBSITE YA KIJANJA, KUPATA HABARI MBALIMBALI ZA NDANI NA NJE YA NCHI. PIA UTAPATA MAMBO YA ACADEMIC. KARIBU SANA
 
Support : Creating Website | Johny Template | Mas Template
Copyright © 2011. GetInformedTz - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Mas Template
Proudly powered by Blogger