Home » » Sabodo akiahidi Chadema jengo la kisasa

Sabodo akiahidi Chadema jengo la kisasa

Written By Koka Albert on Monday, April 30, 2012 | 4:15 AM

Mfanyabiashara, Mustafa Jaffer Sabodo akizungumza na wajumbe wa Mkutano wa Baraza Kuu la Chadema jijini Dar es Salaam jana.kulia ni Mwekiti wa Taifa wa chama hicho, Freeman Mbowe.
Raymond Kaminyoge
MFANYABIASHARA maarufu nchini, Mustafa Sabodo jana alihudhuria Mkutano wa Baraza Kuu la Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na kuahidi kukijengea chama hicho jengo la kisasa la makao yake makuu.

Sabodo ambaye ni kada mkongwe wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) amesema atafanya hivyo kwa kuwa Chadema kimeonyesha shukrani kwa yale ambayo amekuwa akikifanyia.

“Nitaishawishi familia yangu ili tuijengee Chadema ofisi kubwa na ya kisasa ambayo itatumika kama makao makuu ili waweze kuhama katika ofisi ndogo iliyopo Kinondoni,” alisema Sabodo.

Sabodo ambaye amekuwa akikisaidia chama hicho, alikuwa mgeni rasmi kwenye ufunguzi wa mkutano huo unaoendelea Dar es Salaam.

“Kwa kweli nimefurahi sana kunialika kwenye mkutano wenu, nimeshawahi kuisaidia CCM, lakini hawajawahi kunishukuru kama mlivyofanya ninyi,” alisema Sabodo ambaye kitaaluma ni mchumi na kuongeza:

“Nimeisaidia sana CCM, nilichowapa Chadema ni asilimia moja tu ya makubwa niliyowasaidia CCM, lakini hawajawahi kuniita kwenye vikao vyao. Leo nimefarijika sana kuwepo kwenye mkutano wenu.”

Sabodo ambaye ni mzaliwa wa Mkoa wa Lindi alisema ni jambo la ustaarabu kushukuru kwa kila ambacho unapewa na mwenzako.

Alisema CCM si chama kibaya, lakini Chadema kimeelekeza nguvu zake katika kusaidia wanyonge kitendo ambacho kinampa faraja kuendelea kukisaidia.

“Nitawaambia marafiki zangu waisaidie Chadema, lakini nitawaambia pia marafiki zangu kina Joseph Warioba waiangalie sana Chadema kwani inafanya vizuri,” alisema Sabodo.

Alisema hali inatisha hivi sasa kwa sababu wananchi wengi wanyonge wanashindwa hata kununua unga na sukari.
“Wanyonge wanateseka wanashindwa kupata mahitaji yao ya muhimu, naomba Chadema muendelee na juhudi zenu za kusaidia wanyonge wa nchi hii,” alisema.

Alisema yeye ni mfanyabiashara ambaye alikutana na Rais wa Awamu ya Kwanza, Mwalimu Julius Nyerere ambaye katika kukisaidia chama, alimwahidi nafasi mbalimbali serikalini lakini alikataa na kuendelea kuwa mfanyabiashara.

Alisema propaganda zinazoenezwa kuwa Chadema kina udini hazina ukweli wowote akisema zinafanywa na maadui wa chama hicho kwa lengo la kuwakatisha tamaa.“Mimi naitwa Mustafa Sabodo nakisaidia chama viongozi na wanachama wana dini tofauti sasa udini hapo uko wapi?” alisema Sabodo.
Share this article :

Post a Comment

KARIBU KATIKA WEBSITE YA KIJANJA, KUPATA HABARI MBALIMBALI ZA NDANI NA NJE YA NCHI. PIA UTAPATA MAMBO YA ACADEMIC. KARIBU SANA
 
Support : Creating Website | Johny Template | Mas Template
Copyright © 2011. GetInformedTz - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Mas Template
Proudly powered by Blogger