Home » » Wanafunzi 5,000 waliofaulu hawajui kusoma, kuandika

Wanafunzi 5,000 waliofaulu hawajui kusoma, kuandika

Written By Koka Albert on Tuesday, April 10, 2012 | 2:47 AM

IMEBAINIKA kwamba wanafunzi 5,200 waliofaulu na kuchaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza mwaka huu, hawajui kusoma wala kuandika.

Kutokana na sababu hiyo, habari kutoka Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi zinasema kwamba wanafunzi hao wataachishwa masomo na Serikali inaangalia uwezekano wa kuchukua hatua za kisheria wanafunzi hao na wakuu wa shule wanazotoka ili kukomesha tatizo hilo.

Wanafunzi hao wanatoka katika mikoa yote ya Tanzania bara, isipokuwa Kigoma ambao taarifa zake hazijafika katika wizara hiyo.

Wanafunzi hao wamebanika kutojua kusoma wala kuandika baada ya kupewa majaribio ya kupima uwezo wao wa Kusoma, Kuandika na Kuhesabu (KKK) baada ya kuripoti shuleni kama ilivyoagizwa na Serikali.

Desemba 14, mwaka jana wakati akitangaza matokeo ya Mitihani ya Darasa la Saba, Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Philipo Mulugo aliagiza wanafunzi wote watakaoingia kidato cha kwanza mwaka huu wapimwe kwanza uwezo wao wa Kusoma na Kuandika.

Agizo hilo lilitokana na udanganyifu uliojitokeza kwenye mtihani huo na kusababisha watoto 9,736 kufutiwa matokeo.

Wanafunzi waliofanya mtihani huo walikuwa 983,545 na waliofaulu ni 567,567. Kati yao wasichana walikuwa 278,377 sawa na asilimia 54.48 na wavulana walikuwa 289,190 sawa na asilimia 62.49.

Akizungumza na wafanyakazi wa Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) mwishoni mwa wiki, Mulugo alisema tathmini inaonyesha kuwa Mkoa wa Kilimanjaro umeongoza kwa kuwa na wanafunzi wengi wasiojua kusoma na kuandika.

"Mkoa wa Kilimanjaro una wanafunzi wasiojua kusoma na kuandika wapatao 660, Tanga 490 na Dar es Salaam 208," alisema Mulugo bila kutaja matokeo ya mikoa mengine.

“Hili ndilo janga la kitaifa sasa. Siyo hayo mengine ambayo watu wanasema ni majanga ya kitaifa. Lazima tujiulize kwa nini watoto wanamaliza darasa la saba wakiwa hawajui kusoma wala kuandika na halafu wanafaulu?” alihoji kuongeza:

“Je, siku hizi hakuna tena somo la kusoma na kuandika? Kwa nini mtoto amalize shule bila kuwa na maarifa ya KKK? Mitaala (mitalaa) mnayoandika kwa nini hamsaidii mtoto katika hili? Nataka leo nijue tatizo liko wapi, mengine (matatizo) ya Serikali; walimu, vitabu, miundombinu na majibu yake sisi tunayo.”

“Jambo la kusikitisha kuna mpaka baadhi ya wanafunzi wa kidato cha tatu, ambao hawajui kusoma wala kuandika. Tulipofikia siyo pazuri hata kidogo, lazima tuwe makini jamani. Tuheshimu Baraza la Mitihani (Necta) tupate ufumbuzi wa mambo haya taifa hili ni letu sote, lazima tuhakikishe linasimama imara.”

Alisema Serikali kwa upande wake, imejipanga kufanya utafiti na kujua chanzo cha tatizo na kuwa imepata Sh150bilioni kutoka Global Partnership for Education (GPE), kwa ajili hiyo.

Kaimu Mkurugenzi wa TET, Habib Fentu alisema mitalaa waliyoandika imesisitiza mwalimu kufanya tathmini ya kile alichofundisha kila baada ya mada husika kumalizikia.

“Kwa hiyo hapa sasa suala la uwajibikaji linakuja, inakuwaje mtoto amalize darasa la saba akiwa hajui kusoma, kuandika wala kuhesabu na mwalimu wa darasa yupo, mwalimu wa taaluma, mwalimu mkuu na kamati ya shule vipo?”

Katika matokeo ya darasa la saba yaliyotangazwa mwaka jana, Mkoa wa Manyara uliongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya wanafunzi waliofutiwa matokeo ukifuatiwa na Arusha.
Share this article :

Post a Comment

KARIBU KATIKA WEBSITE YA KIJANJA, KUPATA HABARI MBALIMBALI ZA NDANI NA NJE YA NCHI. PIA UTAPATA MAMBO YA ACADEMIC. KARIBU SANA
 
Support : Creating Website | Johny Template | Mas Template
Copyright © 2011. GetInformedTz - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Mas Template
Proudly powered by Blogger