Home » » Ripoti ya CAG yamweka njiapanda Waziri Mkulo

Ripoti ya CAG yamweka njiapanda Waziri Mkulo

Written By Koka Albert on Tuesday, April 17, 2012 | 2:50 AM


Ramadhan Semtawa
KASHFA ya uuzwaji wa kiwanja cha Serikali namba 10 kilichoko Barabara ya Nyerere, Dar es Salaam kwa Kampuni ya Mohamed Enterprises (MeTL), imemuweka njiapanda Waziri wa Fedha na Uchumi, Mustafa Mkulo baada ya Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kuonyesha kuwa uuzwaji wa kiwanja hicho, uliihusisha wizara yake na Ofisi ya Msajili wa Hazina.

Mkulo aliwahi kuingia kwenye mvutano na Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC), Zitto Kabwe baada ya kuituhumu kamati hiyo kuhongwa ili kutetea nyongeza ya muda ya Shirika Hodhi la Mashirika ya Umma (CHC).

Katika Mkutano wa Nne wa Bunge ambao ulishuhudia mvutano huo bungeni, Zitto aliapa kuwa kama ingebainika alihongwa yeye au wajumbe wake wa POAC, angejiuzulu na kumtaka Mkulo naye ale kiapo kama hicho ikibainika kuwa maelekezo yake kwenda CHC yalisababisha ufisadi huo, lakini waziri huyo aligoma.
Hata hivyo, taarifa ya mwaka huu ya CAG iliyowasilishwa bungeni wiki iliyopita, inaonyesha kuwa Wizara ya Fedha na Ofisi ya Msajili zilihusika moja kwa moja katika uuzaji wa kiwanja hicho.

Sehemu ya ripoti hiyo ya CAG inasema: “Matokeo ya ukaguzi maalumu yalibaini mambo yafuatayo: Ilionekana kuwa Ofisi ya Msajili wa Hazina na Wizara ya Fedha zilihusika moja kwa moja katika uuzwaji wa Kiwanja Na.10 kilichopo kando ya Barabara ya Nyerere kilichouzwa kwa kampuni ya Mohamed Enterprises Tanzania Ltd, bila kuishirikisha Bodi ya Wakurugenzi ya CHC.”

CAG alifafanua kwamba ripoti pia inaonyesha ubinafsishaji wa mashirika yaliyosalia kwa ajili ya ubinafsishaji, ufuatiliaji na tathmini ya mashirika yaliyokwisha binafsishwa mpaka muda wa kuandaa ripoti hiyo ni 34 ambayo yalishatengwa kwa ajili ya ubinafsishwaji na yalikuwa bado yapo kwenye hatua mbalimbali za ubinafsishaji.

“Kimsingi mashirika haya yako kwenye hatua zilezile yalipokuwa wakati wa kuandika ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ya mwaka jana 2009/2010. Hii inaashiria ama ufanyajikazi usioridhisha wa Shirika Hodhi la Mali za Umma au matatizo kwenye sehemu nyingine zinazohusika kwenye mchakato wa ubinafsishaji.”

Pia CAG aliitaka Serikali iamue ama kuharakisha kukamilisha ubinafsishaji kwa mashirika yaliyosalia ili kuepusha kuharibika kwa rasilimali zilizopo au ibadilishe uamuzi wake na kuyapa mashirika hayo mtaji yaweze kufanya kazi kwa ufanisi.

“Nilibaini kuwepo kwa sintofahamu katika Hati ya madai ya Sh2.4bilioni kutoka katika Kampuni ya DRTC kama gharama za ulinzi na tozo la matumizi ya barabara ya kuingia kwenye Kiwanja Na.192 kando ya Barabara ya Nyerere,” imesema taarifa hiyo.

Katika ripoti yake, CAG alionyesha upungufu ulioonekana pia kwenye uuzwaji wa jengo la Kampuni ya Tanzania Motors (TMC), lililopo Kiwanja Na.24 kando ya Barabara ya Ali Hassan Mwinyi.
Pia, menejimenti ya CHC haikuwa makini kwenye uuzaji wa Kiwanja Na. 33 kilichopo katika eneo la viwanda la Chang’ombe kwa Maungu Seed.

Mkulo na CHC
Mwishoni mwa mwaka jana, wakati CAG akiendelea na ukaguzi huo maalumu wa uuzwaji wa kiwanja hicho na tuhuma nyingine za ufisadi, Mkulo aliivunja Bodi ya Wakurugenzi ya CHC, ambayo ilikuwa ikisubiri kupokea ripoti hiyo ya ukaguzi.

Msingi wa uchunguzi ndani ya CHC ulitokana na maombi ya Bodi ya shirika hilo baada ya kuwapo tuhuma kwamba menejimenti yake ilihusika na vitendo vya ufisadi hivyo kusababisha kusimamishwa kwa Kaimu Mkurugenzi wake, Methusela Mbajo.

Ofisi ya CAG ilifanya uchunguzi kwa kutumia kampuni ya kimataifa ya ukaguzi wa hesabu ya Ernst&Young, ukaguzi ambao pia ulilenga kubaini tuhuma dhidi ya POAC.
Awali, Bodi ya CHC ilikuwa imalize muda wake Juni 30 mwaka jana lakini Mkulo aliiongezea muda hadi Desemba 31, mwaka huo na barua ya hatua hiyo ilitumwa kwa wajumbe wa bodi hiyo kuwajulisha hatua hiyo.

Hata hivyo, ghafla Mkulo alibadili uamuzi wake huo wa Oktoba 10, 2011 kwa kumwandikia Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa CHC kwamba awaarifu wajumbe wa bodi kuhusu ukomo wa bodi yao kwamba ni Juni 30 mwaka huo.

Sehemu ya barua kutoka Wizara ya Fedha kwenda CHC ilisema: “Nimeelekezwa nikuarifu kwamba Waziri wa Fedha, Mh. Mustafa H. Mkulo (Mb), ametengua uamuzi wake wa kuongeza muda wa Bodi ya CHC hadi tarehe 31 Desemba, 2011 au hapo Rais atakapoteua Mwenyekiti wa Bodi hiyo kuanzia tarehe ya barua hii (10, Oktoba, 2011).”

Barua hiyo iliyosainiwa Geoffrey Msella kutoka Ofisi wa Msajili wa Hazina, ilisema: “Kwa barua hii unatakiwa kuwaandikia barua waliokuwa Wajumbe wa Bodi ukiwashukuru kwa michango yao kwa Shirika hili katika kipindi walichotumikia CHC.”

Kwa barua hiyo, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa CHC, Dome Malosha siku hiyohiyo ya Oktoba 10, 2011 aliwaandikia barua wajumbe hao wa Bodi akiwaarifu kuhusu uamuzi wa Waziri Mkulo kuvunja bodi hiyo.

Jana, Waziri Mkulo hakupatikana kuzungumzia ripoti hiyo ya CAG baada ya simu yake mkononi kutopatikana muda mwingi.
http://www.mwananchi.co.tz/biashara/-/22093-ripoti-ya-cag-yamweka-njiapanda-waziri-mkulo
Share this article :

Post a Comment

KARIBU KATIKA WEBSITE YA KIJANJA, KUPATA HABARI MBALIMBALI ZA NDANI NA NJE YA NCHI. PIA UTAPATA MAMBO YA ACADEMIC. KARIBU SANA
 
Support : Creating Website | Johny Template | Mas Template
Copyright © 2011. GetInformedTz - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Mas Template
Proudly powered by Blogger