Home » » Maugo aendeleza uteja kwa Cheka

Maugo aendeleza uteja kwa Cheka

Written By Koka Albert on Monday, April 30, 2012 | 4:20 AM

Imani Makongoro
BAADA ya kupokea kipigo kizito juzi usiku bondia  Mada 'King' Maugo amedai alianza kukata 'network' raundi ya nne ya pambano lake dhidi ya Francis 'SMG' Cheka lililofanyika kwenye ukumbi wa PTA, Sabasaba jijini Dar es Salaam.

Maugo alisalimu amri raundi ya saba ya pambano hilo lililokuwa la raundi 12, na kumpa ushindi wa Technical Knock Out (TKO) mpinzani wake Cheka aliyetangazwa kuwa bingwa wa Afrika wa mkanda wa IBF wa uzani wa Super Middle.

Maugo aliyeanza pambano hilo kwa kasi katika  raundi tatu za mwanzo alisema hakuelewa nini kilimtokea hadi kujikuta ametoka ulingoni raundi ya saba na kunyoosha mikono kusalimu amri kwani alifanya hivyo pasipo kujitambua.

Mashabiki wa Maugo waliokuwa wakipiga kelele za kushangilia mwanzoni,  walijikuta sauti zao zikimezwa na zile za mashabiki wa Cheka ambao walianza kumshangilia bondia wao kwa nguvu zote kuanzia raundi ya nne.

Katika raundi ya nne, tano na sita mashabiki hao walipaza sauti wakishangilia 'Cheka, Cheka, Cheka, maliza kazi tuondoke, pigaaa, ua huyo' na nyingine za kushangilia ambazo zilizidi kuongeza hamasa kwa bondia huyo kufanya kile mashabiki wake walichokuwa wanataka.

Kabla ya mabondia hao kupanda ulingoni mashabiki wa pande zote mbili waliokuwa wamefurika ukumbini hapo walikuwa wakitambiana kwa majigambo ya hapa na pale na baadhi yao wakiwekeana 'dau' endapo mmoja kati yao atashinda.

Cheka alikuwa wa kwanza kupanda ulingoni saa  9:49 usiku aliwasalimia mashabiki wake kabla ya kuanza kuzunguka kila pande ya ulingo na dakika mbili baadae Maugo alipanda ulingoni hapo akiwa kona ya blue alishangiliwa kwa nguvu zote na mashabiki wake.

Mabondia hao walianza kupimana mabavu saa nne kamili usiku ikiwa ni baada ya wimbo wa taifa kupigwa, Cheka alikuwa wa kwanza kupiga konde lililompa sawia Maugo akubaki nyuma na kujibu mashambulizi hayo kwa kasi ya ajabu iliyosabababisha mashabiki wa Cheka kuwa kimya kwa dakika kadhaa wakishuhudia bondia wao anavyosulubiwa.

Kasi hiyo ya Maugo iliendelea hadi raundi ya tatu ambapo dakika ya kwanza ya raundi hiyo alimpeleka Cheka chini kabla ya kumpeleka tena chini dakika ya tatu ya raundi hiyo ambayo jaji wa pambano, John Shipanuka alifuta makonde hayo baada ya Maugo kuonekana kucheza rafu kwa kumsukuma Cheka huku akiendelea kurusha makonde wakati mpinzani wake akiwa chini.

Raundi ya nne Maugo aligeuziwa kibao baada ya kuporomoshewa makonde mfululizo hali iliyoamsha furaha kwa mashabiki wa Cheka ambao hawakunyamaza hadi raundi ya sita baada ya Maugo kushambulia dakika ya kwanza ya raundi, lakini hakuweza kumaliza na kasi aliyoanza nayo hivyo kumpa mpinzani wake nafasi ya kushambulia zaidi.

Mashabiki wa Maugo waliokuwa wakiongozwa na Karama Nyirawila walipata wakati mgumu baada ya kengele ya kuashiria kuanza kwa raundi ya saba ambapo bondia wao alishindwa kuendelea na pambano na kujisalimisha kwa kunyoosha mikono.

Baada ya kujisalimisha Maugo alipoteza fahamu kwa dakika kadhaa hivyo kuwapata wakati mgumu wapambe wake kumpepea zoezi lilifanyika pembezoni mwa ukumbi huo huku wale wa Cheka wakiendelea kusherehekea ubingwa ukumbini hapo.

Kwa ushindi wa juzi Cheka anaendeleza rekodi yake ya kumkung'uta Maugo mara tatu mfululizo ambapo mapambano mawili yaliyotangulia Maugo alipigwa kwa pointi.
Share this article :

Post a Comment

KARIBU KATIKA WEBSITE YA KIJANJA, KUPATA HABARI MBALIMBALI ZA NDANI NA NJE YA NCHI. PIA UTAPATA MAMBO YA ACADEMIC. KARIBU SANA
 
Support : Creating Website | Johny Template | Mas Template
Copyright © 2011. GetInformedTz - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Mas Template
Proudly powered by Blogger