Home » » Mawaziri wagoma

Mawaziri wagoma

Written By Koka Albert on Monday, April 30, 2012 | 2:31 AM

MKULO ASEMA HAWAJIBIKI KAMATI KUU CCM, NUNDU ATOA MANENO MAKALI, MAIGE, "NIACHENI"
Ramadhan Semtawa na Boniface Meena
SIKU chache baada ya Kamati Kuu (CC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), kubariki uamuzi wa Rais Jakaya Kikwete wa kulisuka upya Baraza la Mawaziri kwa kuwaondoa waliotajwa katika Ripoti Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), mawaziri wanaotakiwa kujiuzulu wamekataa kuchukua hatua hiyo huku mmoja wao, Waziri wa Fedha, Mustafa Mkulo akisema hawajibiki kwa chombo hicho cha chama.

Kwa wiki mbili sasa, kumekuwa na shinikizo la kutaka mawaziri wanane wajiuzulu nyadhifa zao kutokana na wizara zao kutajwa na CAG kwamba zimehusika na ufisadi huku wengine wakitajwa moja kwa moja kufanya uamuzi wenye maslahi binafsi.

Wakizungumza na waandishi wetu kwa nyakati tofauti jana, baadhi ya mawaziri hao walisema wanaacha hatima yao mikononi mwa Rais ambaye ndiye mamlaka ya uteuzi na kutengua nafasi zao.

Mkulo
Mwandishi: Asalaam alaykum ndugu yangu Waziri Mkulo.
Mkulo: Walaykum Salaam.
Mwandishi: Habari ya mapumziko?
Mkulo: Aaah salama.
Mwandishi: Nimekupigia kutaka kujua msimamo wako kuhusu uamuzi wa CC.
Mkulo: Nakusikiliza endelea.
Mwandishi: CC imebariki Rais Kikwete afumue Baraza la Mawaziri ni kwa nini usijiuzulu kabla?
Mkulo: No comment, (sina la kusema).
Mwandishi: Lakini, CC ina nafasi kubwa katika utendaji wa Serikali, kwa nini huoni uzito wa agizo lake?
Mkulo: Mimi sijaona muhtasari wa vikao vya CC lakini, pia siwajibiki kwa CC.
Mwandishi: Kwa maana nyingine huwezi kujiuzulu?
Mkulo: No comment katika hilo.

Mkulo amekuwa akitajwa kutaka kuvunja Shirika Hodhi la Mashirika ya Umma (CHC) kwa madai ya kuficha kile kilichoitwa baadhi ya tuhuma za ufisadi katika uuzaji mali za umma ikiwemo Kiwanja Namba 10 kilichopo Barabara ya Nyerere, kwa Kampuni ya Mohamed Enterpises (MeTL).

Mkuchika
Mwandishi: Salaam ndugu yangu Waziri Mkuchika.
Mkuchika: Nzuri ndugu yangu
Mwandishi: Mimi ni...(jina la mwandishi) kutoka gazeti la ...(jina la Gazeti).
Mkuchika: Sawa nakusikiliza.
Mwandishi: Ndugu waziri, natambua rekodi yako nzuri ya utendaji wako serikalini, lakini nina swali.
Mkuchika: Sawa, uliza tu.
Mwandishi: Umewahi kuwa Naibu Katibu Mkuu wa CCM Bara, hivyo unajua nafasi chama serikalini.
Mkuchika: Ndiyo.
Mwandishi: Sasa, CC imebariki kuvunjwa Baraza la Mawaziri, je, huoni ni vyema ukakaa pembeni kabla?
Mkuchika: No comment.
Mwandishi: Lakini, unafahamu CC ni chombo kizito uliwahi kuwa mjumbe, kwa nini usubiri kufukuzwa na Rais?
Mkuchuka: Wewe bwana vipi? Uliniuliza nizungumzie uamuzi wa CC sasa nakwambia No comment huelewi?
Mwandishi: Nashukuru sana ndugu waziri
Mkuchika: Ahsante na wewe pia.

Waziri Mkuchuka anatakiwa kujiuzulu kutokana na tuhuma za ubadhirifu katika wizara yake kwa kipindi cha miaka miwili mfululizo, ambazo ni pamoja na mtandao mpana wa wizi katika wizara hiyo huku Halmashauri ya Wilaya Kishapu pekee ikiwa imepoteza Sh6 bilioni.

Nundu
Mwandishi: Asalaam Alaykum Waziri Nundu.
Nundu: Walaykum Salaam.
Mwandishi: Pole na misukosuko ambayo ni kawaida katika siasa.
Nundu: Nashukuru sana ndugu yangu.
Mwandishi: Mimi fulani (jina) Nimekupigia, moja kukwambia tuko pamoja kwani sote ni ndugu, lakini nitakuwa na la pili.
Nundu: Nashukuru sana.
Mwandishi: Kwa hiyo, la kwanza, ndiyo hilo nakupa nguvu na ukubaliane na hali halisi.
Nundu: Sawa.
Mwandishi: La pili, juzi CC ya CCM ilibariki Rais  avunje Baraza, je, huoni ni vyema ukajiuzulu kabla?
Nundu: Sikiliza wewe usijidai mjanja , hili ndilo la kwanza ulilotaka kuniuliza ukajidai unaanza kunipa pole. 
Mwandishi: Hapana. Lakini huoni kujiuzulu unajijengea heshima kuliko kufukuzwa na Rais?
Nundu: Sikiliza kwanza, wacha kupapatika maana hunipi nafasi.
Mwandishi: Sawa endelea, lakini swali langu la msingi ni kuhusu agizo la CC ya chama unachotoka.
Nundu: Hayo ya CC sitaki kuyazungumzia. Lakini pia sitaki kuongea na ninyi Mwananchi mnapotosha ukweli.
Mwandishi: Sawa, kama tulipotosha ndo nakupa nafasi ueleze kwa usahihi.
Nundu: Ninyi sijui mnatumiwa na ..... kuandika uongo halafu mnajidai kutetea maslahi ya taifa.
Mwandishi: Ndugu Waziri, huoni kwa nafasi yako hutakiwi kusema maneno kama hayo?
Nundu: Ndiyo nimekwambia hivyo uandike sasa. Mnatumiwa na ... kunichafua.   

Waziri Nundu anatuhumiwa kuipigia kifua Kampuni ya Chinese Merchants kwa ajili ya ujenzi wa gati Na13 na 14 katika Bandari ya Dar es Salaam huku akienda mbali na kumtuhumu Naibu wake, Athuman Mfutakamba kwamba amekuwa akishinikiza Kampuni ya China Communication Construction Company (CCCC), ipewe kazi ya kujenga magati hayo.

Maige
Swali: Mheshimiwa unaonaje uamuzi wa Kamati Kuu na msimamo wa Rais kuwawajibisha mawaziri waliotuhumiwa, kwa nini usiwajibike?
Maige: Siwezi kuzungumzia mambo hayo kwa sasa, nashukuru.

Wizara yake imekumbwa na tuhuma mbalimbali ikiwemo uuzaji wa mazao ya misitu, ujangili na kusafirishwa wanyamapori nje ya nchi.

Nyalandu
Mwandishi: Habari yako ndugu Nyalandu?
Nyalandu: Safi kaka. Nani wewe?
Mwandishi: Mimi fulani (jina)...kutoka... (jina la gazeti).
Nyalandu: Sawa kaka nakusilikiliza.
Mwandishi: CC ya CCM imeamua Rais Kikwete avunje Baraza, je, huoni umuhimu kujizulu kabla hujaondolewa?
Nyalandu: Kwanza, nimpongeze CAG na vyombo vya habari, lakini, nasema hebu tuache mamlaka ziamue.
Mwandishi: Sawa, lakini uwajibikaji kisiasa ni jambo la heshima. Hili unalionaje?
Nyalandu: Mimi nadhani, kwa jambo hili lilipofikia, ni vyema waliotajwa moja kwa moja wawajibike. Ni jambo jema.

Waziri Nyalandu ameingia katika malumbano na Waziri wake, Dk Cyril Chami wakitupiana mpira kuhusu kashfa ya Shirika la Viwango Tanzania (TBS), inayomkabili Mkurugenzi wake Mkuu, Charles Ekelege baada ya kudaiwa kuiingizia Serikali hasara ya karibu Sh30bilioni kutokana na ukaguzi hewa wa magari nje ya nchi.

Shikizo la mawaziri hao lilianzia bungeni baada ya wabunge wengi kutaka wawajibishwe kwa kuondolewa katika nyadhifa zao.

Katika kuongezea nguvu shinikizo lao, wabunge hao waliamua kuanzisha mchakato wa kumpiga kura ya kutokuwa na imani na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.

Mchakato huo ambao ulikuwa ukisimamiwa na Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe hadi Bunge linaahirishwa, wabunge 76 wakiwamo wa CCM walikuwa wameshasaini katika orodha hiyo.
Uamuzi huo wa wabunge pia uliridhiwa na kikao cha faragha cha wabunge wa CCM kilichofanyika Dodoma wakati Bunge likiendelea.
Share this article :

Post a Comment

KARIBU KATIKA WEBSITE YA KIJANJA, KUPATA HABARI MBALIMBALI ZA NDANI NA NJE YA NCHI. PIA UTAPATA MAMBO YA ACADEMIC. KARIBU SANA
 
Support : Creating Website | Johny Template | Mas Template
Copyright © 2011. GetInformedTz - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Mas Template
Proudly powered by Blogger