Home » » Nyama ya mamba yageuka lulu Bagamoyo

Nyama ya mamba yageuka lulu Bagamoyo

Written By Koka Albert on Monday, April 30, 2012 | 4:07 AM

Na Joseph Kapinga
MWENDO wa kilomita tatu kutoka Bagamoyo mjini kuelekea mji wa Kaole, wenye  utajiri mkubwa wa vivutio vya asili vinavyoaminika kuwapo eneo hilo kwa zaidi ya miaka 500  iliyopita, unafika eneo maarufu kwa ufugaji wa mambalinalojulikana kama Kaole Mamba Ranch.

Hapa kuna Mamba wengi wa saizi mbalimbali wanaofugwa. Kinachovutia zaidi ni kwamba, eneo hilo pia kuna machinjio maalumu ya mamba kwa ajili ya kitoweo kwa mtu yeyote unayehitaji.

Shamba hili linalomilikiwa na wazawa, lilianzishwa mwaka 1992 kwa madhumuni ya kufuga na kuuza ngozi za viumbe hao hatari kwa maisha ya binadamu, ambao uchunguzi unaonyesha watu zaidi ya 500 huuawa kila mwaka duniani kutokana na kushambuliwa na mamba.

Hata hivyo, kupanuka kwa mahitaji ya binadamu na kubadilika kwa mifumo ya maisha, kulifungua milango ya uuzwaji nyama ya mamba baada ya kuongezeka kwa walaji wake.

Ingawa mamba ni hatari kwa maisha ya binadamu kutokana na kumfanya kama sehemu ya chakula chake, upande wa pili naye binadamu amemfanya kitoweo.


Jinsi mamba wanavyochinjwa


Katika shamba hili, kwa mlaji wa nyama hiyo anachofanya ni kutembelea kwenye mabanda wanayofugwa, kisha kuchagua unayehitaji na baada ya mapatano ya bei, unachinjiwa hapohapo na kuondoka na nyama yako.

Peter Mamba, Msimamizi wa shamba hilo anasema kazi ya kumchinja mamba ni rahisi kama kuchinja kuku ili mradi tu awe amefungwa mdomo, miguu na mkia sehemu ambazo ni hatari.

"Mamba hata kama ni mkubwa kiasi gani, anaweza kuchinjwa kirahisi lakini kwanza kwa kuhakikisha amefungwa mdomo na mkia kwani ndiyo maeneo hatari anayoweza kumjeruhi binadamu," anasema.

Katika shamba hilo, kuna sehemu maalumu imetengezwa kwa sementi na kwa muonekana sehemu hiyo inafafana na kibaraza kidogo, ambapo mamba baada ya kukamatwa toka kwenye banda hupelekwa hapo kuchinjwa na kuchunwa ngozi.

Anasema mamba hukamatwa kwa mitego maalumu na kuondolewa bandani kwa kufungwa sehemu hizo na kulazwa eneo la kuchinjwa, ambapo zoezi zima linaweza kuwa chini ya dakika 10.

Utafiti wa kitaalamu unaonyesha kuwa, nyama ya mamba ina ladha kama kuku na ina madini mengi ya joto ambayo binadamu huhitaji zaidi kwa ajili ya ustawi wa afya yake.

Nyama ya mamba ina proteni nyingi, kama vitamini B 12, haina mafuta (cholesterol) na ina ladha kama nyama ya Kuku. Inaelezwa kuwa, ni bora zaidi kula nyama ya mamba kuliko ng'ombe au nguruwe.

Walaji

Peter anasema walaji wakubwa wa mamba ni raia kutoka China na wazungu wachache, na ameshangazwa na utamaduni wa Waafrika kutopenda kujaribu kuonja vyakula vingine kama nyama ya mamba.

"Mimi binafsi nimewahi kula Mamba, ana nyama nzuri na tamu haswa. Mamba ana nyama nyeupe, haina damu kama alivyo kuku, hakuna tofauti kati ya nyama ya Mamba na Kuku,"anasema Peter.

Peter anasema watu wengi wanashangaa kusikia mamba analiwa na hii ni kwa sababu ya utamaduni wa kutopenda kujaribu mambo mapya miongoni mwa watu wengi.

"Hapa wanakuja watu wengi kutembelea kwa lengo la kuona ufugaji huu, lakini tukiwaeleza kwamba tunauza pia viumbe kwa ajili ya kitoweo, wengi hushangaa kwa kumuona mamba kama kiumbe aliyekosa sifa za kuliwa," anasema Peter.

Anasema kutokana na watu wengi kutopenda nyama ya mamba, kumefanya soko lao kuwa gumu kwani wanalazimika kuwategemea wateja wao wa siku zote ambao ni wachache na wakati mwingine huja mara moja baada ya zaidi ya mwaka.
Share this article :

Post a Comment

KARIBU KATIKA WEBSITE YA KIJANJA, KUPATA HABARI MBALIMBALI ZA NDANI NA NJE YA NCHI. PIA UTAPATA MAMBO YA ACADEMIC. KARIBU SANA
 
Support : Creating Website | Johny Template | Mas Template
Copyright © 2011. GetInformedTz - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Mas Template
Proudly powered by Blogger