Home » » Tatizo la ajira kwa vijana ni kubwa nchini, lisifanyiwe masihara

Tatizo la ajira kwa vijana ni kubwa nchini, lisifanyiwe masihara

Written By Koka Albert on Monday, April 2, 2012 | 12:20 AM

KATIKA siku za hivi karibuni mjadala wa tatizo sugu la ajira kwa vijana umekuwa ukichukua nafasi kubwa kwenye vyombo vya habari, warsha na maeneo ya makazi ya watu.

Mjadala huu umepamba moto kutokana na idadi kubwa ya vijana ambao wako mitaani bila kazi na hivyo hawana kipato cha aina yoyote cha kuendeleza miasha yao.

Kutokana na hali hii, vijana wa Tanzania ambao ni nguvu kazi ya taifa ni zaidi ya milioni ishirikini wanaishi maisha ya dhiki na kubahatisha kwani hata sekta ya viwanda ambayo haswa ilitakiwa kuwa mkombozi imeajiri vijana 60,000 kati ya mamilioni ambao wangependa kupata shughuli ya kufanya kwenye sekta hiyo.

Tunasema kwamba idadi hii kubwa ya vijana ambao wamemaliza darasala la saba, vyuo vya ufundi hadi vyuo vikuu nchini hawajui mustakabali wa maisha yao ya sasa na yajayo.

Sote ni shahidi kwamba kasi ya ukosefu wa ajira nchini inazidi kukua kutokana na wahitimu zaidi ya milioni moja wanaohitimu katika shule na vyuo mbalimbali nchini.

Takwimu za kwamba zaidi ya wahitimu milioni moja wanamaliza shule na vyuo mbalimbali nchini ni za mwaka 2006, hivyo tunaamini kwamba huenda idadi ya vijana wanaoingia katika soko la ajira ni kubwa  zaidi ya milioni moja kwa kuwa miaka zaidi ya sita imepita tangu utafiti huo uliofanywa na Taasisi ya Takwimu Nchini (NBS).

Ndio maana tunatoa wito kwa taasisi husika kufanya utafiti mpya ili kuweza kubaini ukubwa tatizo kwa lengo la kukabiliana nalo baladala ya kuanza kurushiana maneno binafsi kwa wale ambao wameliongelea.
Tunasema kwamba suala la ajira ni suala nyeti ambalo halipaswi kujibiwa kwa masihara bali linahitaji majibu fasaha ambayo yatasaidia kutafuta uvumbuzi.

Katika miezi ya hivi karibuni, tulishuhudia vijana wa Kigoma Kaskazini, wakimzonga mbunge wao Zitto Kabwe kwamba awatafutie ajira kwa kuwa wamechoka kukaa vijiweni kila kukicha. Vijana hawa wa Kigoma Kaskazini wanatoa taswira moja ambayo si vijana wote wanaokaa vijiweni wanapenda kufanya hivyo bali ni kutokana na mazingira magumu ya kupata shughuli ya kufanya.

Leo hii makampunui yakitangaza nafasi ya kazi moja, waombaji ambao wana viwango vikubwa vya elimu wanaomba zaidi ya 500 katika nafasi moja na hii ni ishara kwamba kuna watu wengi sana ambao wamesoma na kushindwa kupata ajira kwenye sekta binafsi na serikalini.

Changamoto ambayo Serikali na taasisi mbalimbali zinapaswa kukabiliana nayo ni kuweza kuanzisha viwanda vingi ambavyo vinachukua idadi kubwa ya wafanyakazi, pamoja na kuweka mazingira mazuri ya kukuza kilimo ambacho pia kinaweza kupunguza idadi kubwa ya vijana ambao hawana ajira.

Leo hii vijana ambao wanamaliza kozi zao katika vyuo vya kilimo hawana kazi kwa kuwa sekta hiyo haijapewa kipaumbele kikubwa na Serikali, hivyo wahitimu hao wameamua kutafuta kazi nyingine ambazo hawajasomea na si tu kwa kupenda, lakini kutokana na hali halisi ya sekta ya kilimo.

Ndio maana tusema kwamba bila sekta ya kilimo na viwanda kupata msukumo mpya wa vitendo, ukosefu wa ajira kwa vijana ni bomu linalosubiri kupasuka na ni wakati muafaka sasa kuanza mjadala mkubwa wa kifaifa wa ukosefu wa ajira kwa vijana kwa lengo la kupata suluhisho.

Kwa maoni yetu, tatizo la ajira nchini ni kubwa na hivyo watu waijadili hoja hiyo kwa kina badala ya kuanza kujadili nani kasema kwani yote hayo bado hayamsaidii kijana anayeshinda siku nzima bila mlo kwa kuwa hana ajira
Share this article :

Post a Comment

KARIBU KATIKA WEBSITE YA KIJANJA, KUPATA HABARI MBALIMBALI ZA NDANI NA NJE YA NCHI. PIA UTAPATA MAMBO YA ACADEMIC. KARIBU SANA
 
Support : Creating Website | Johny Template | Mas Template
Copyright © 2011. GetInformedTz - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Mas Template
Proudly powered by Blogger