Home » » Magufuli akwama nyumbani kwake

Magufuli akwama nyumbani kwake

Written By Koka Albert on Tuesday, April 3, 2012 | 7:50 AM

Dk John Magufuli
Salum Maige, Chato
SAKATA la watumishi wakiwamo watendaji wa kata na vijiji wanaotuhumiwa kufanya ubadhirifu Halmashauri ya Wilaya ya Chato, mkoani Geita, limechukua sura mpya kutokana na Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli, kushangazwa na kitendo cha Mkurugenzi wa halmashauri, Hamida Kwikwega, kushindwa kuwasimamisha kazi licha ya kufikishwa mahakamani.

Watendaji hao walifikishwa mahakamani kwa tuhuma za ubadhirifu wa pembejeo za kilimo zilizotolewa na Serikali.
Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika ilitoa pembejeo ya ruzuku halmashauri hiyo zenye thamani ya Sh1.5 bilioni, lakini katika hali isiyo ya kwaida zaidi ya Sh1.3 bilioni zinadaiwa kuishia mifukoni mwa baadhi ya watendaji hao.

Kufuatia hali hiyo, baadhi ya viongozi wa vyama vya siasa, asasi za kiraia kwa kushirikiana na wananchi walipaza sauti kuelezea ubadhirifu huo, Serikali ilionekana kuchukua hatua za makusudi ili kubaini wahusika na kuwafikisha kortini.
Mbali na kufikishwa kortini watuhumiwa hao wakiwamo watendaji wa vijiji 30, halmashauri imeshindwa kuwasimamisha kazi kupisha uchunguzi zaidi wakati kesi zao zikiendelea, huku wakituhumiwa kuwatishia maisha wananchi.

Hatua hiyo juzi ilipelekea Dk Magufuli kuishtumu ofisi ya mkurugenzi kwa kushindwa kuwasimamisha kazi watendaji hao, huku baadhi ya viongozi wa halmashauri hiyo akiwamo Ofisa Kilimo wa Wilaya, Dk Phales Tongora, akisimamishwa kazi baada ya kufikishwa mahakamani.

 “Ubadhirifu wa fedha za pembejeo za kilimo umeisababishia Wilaya ya Chato kuwa na jina baya sana kutokana na tamaa ya watu wachache ambao wamekuwa wakikuzunguka wewe mkurugenzi na kuhujumu uchumi wa wilaya yetu,”  alisema.
Pia, Dk Magufuli aliwanyoshea kidole madiwani kwa kushindwa kuwadhibiti watendaji ambao wamekuwa wakishindwa kusimamia miradi ya maendeleo.

Kwa upande wake, Kikwega alikiri kuwapo kwa baadhi ya watendaji wa vijiji wanaoendelea na kazi, kwa madai anasubiri uamuzi wa mahakama.
Share this article :

Post a Comment

KARIBU KATIKA WEBSITE YA KIJANJA, KUPATA HABARI MBALIMBALI ZA NDANI NA NJE YA NCHI. PIA UTAPATA MAMBO YA ACADEMIC. KARIBU SANA
 
Support : Creating Website | Johny Template | Mas Template
Copyright © 2011. GetInformedTz - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Mas Template
Proudly powered by Blogger