Home » » Tume Katiba kutangazwa wiki hii

Tume Katiba kutangazwa wiki hii

Written By Koka Albert on Wednesday, April 4, 2012 | 2:03 AM

 
Mwandishi Wetu
RAIS Jakaya Kikwete anatarajiwa kutangaza majina 30 ya wajumbe wa Tume ya Kuratibu na Kukusanya Maoni kuhusu Katiba Mpya, wakati wowote ndani ya wiki hii.

Vyanzo vya habari kutoka serikalini vinasema kwamba Rais Kikwete atatangaza majina hayo kabla ya Sikukuu ya Pasaka.Hata hivyo, Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Salva Rweyemamu alipoulizwa jana, hakuwa tayari kuzungumzia suala hilo kwa undani na badala yake alijibu: “Rais atakuwa tayari kutangaza atakapoona inafaa.”

Lakini vyanzo hivyo vya habari vilisema kwamba miongoni mwa watakatangazwa na Rais ni mwenyekiti na makamu wake ambao wataiongoza tume hiyo inayopaswa kuwa na idadi sawa ya wajumbe kutoka Tanzania Bara na Zanzibar.
Miongoni mwa majina yanayotarajiwa kuwemo ni yale yaliyopendekezwa na vyama mbalimbali vya siasa na wadau wengine ambayo yalipaswa kuwasilishwa kwa Rais kufikia Machi 16, mwaka huu.

Tangazo la Serikali
Katika kuhakikisha tume hiyo inaundwa na watu huru na wanaotokana na maoni ya wadau, Februari 29, mwaka huu Rais Kikwete alivitaka vyama vya siasa na wadau wengine kumpelekea majina matatu ya watu wanaodhani wanafaa kuingia kwenye tume hiyo.

Rais Kikwete mbali na kuhamasisha mchakato huo kwa vyama vyenye usajili wa kudumu, pia aliwataka wadau wengine ikiwa ni pamoja na jumuiya za kidini, asasi za kiraia na makundi mengine yenye malengo yanayofanana, kushiriki kwa namna moja au nyingine.

Rais Kikwete alisema ametoa mwaliko huo kwa mujibu wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba iliyopitishwa Februari 10, mwaka huu na Bunge ambao aliurudhia kwa kuutia saini siku 10 badaaye.
Hata hivyo, kabla ya kupitishwa na Bunge, wabunge wa Chadema waligoma kushiriki kwenye mjadala kwa kile walichosema ni kutoridhishwa na mchakato wake.

Mbali na Chadema, baadhi ya wanaharakati nao walipinga muswada huo na kutaka mchakato wa kuutangaza urejewe.Hata hivyo, Rais Kikwete aliwakaribisha wadau wenye malalamiko kukutana naye Ikulu ili achukue maoni yao na kuhakikisha yanafanyiwa kazi kabla Tume haijaundwa.
Baada ya kukutana na wadau hao, alirejesha tena sheria hiyo mbele ya Bunge ili ifanyiwe marekebisho madogo kuingiza maoni hayo.

Baada ya hapo ndipo alipiotoa tena mwaliko kwa wadau hao kumpelekea majina matatu ya watu wanaoamini kwamba wakiiunda tume hiyo itafanikisha kazi hiyo kwa uhuru na haki.

Watu hao walipaswa kuwa wanaokidhi sifa zilizotamkwa katika Kifungu cha Sita cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba. Miongoni mwa sifa hizo ni uzoefu katika kufanya mapitio ya Katiba na sifa za kitaaluma za wajumbe kwenye mambo ya Katiba, Sheria, Utawala, Uchumi, Fedha na Sayansi ya Jamii.

Sifa nyingine ni kuwa na uelewa wa jiografia na mtawanyiko wa watu nchini, pamoja na kuzingatia vigezo vya umri, jinsia na uwakilishi wa makundi mbalimbali ya kijamii.

Waliokuwa wanakusanya majina hayo kwa niaba ya Rais Kikwete ni Katibu Mkuu Kiongozi na Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Share this article :

Post a Comment

KARIBU KATIKA WEBSITE YA KIJANJA, KUPATA HABARI MBALIMBALI ZA NDANI NA NJE YA NCHI. PIA UTAPATA MAMBO YA ACADEMIC. KARIBU SANA
 
Support : Creating Website | Johny Template | Mas Template
Copyright © 2011. GetInformedTz - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Mas Template
Proudly powered by Blogger