Home » » Tushirikiane kuilinda AMANI yetu

Tushirikiane kuilinda AMANI yetu

Written By Koka Albert on Thursday, May 31, 2012 | 12:25 AM

KATIKA hali isiyokuwa ya kawaida tangu kuanzishwa kwa serikali ya maridhiano Zanzibar mwaka 2010, kwa siku tatu mfululizo zimetokea vurugu kubwa zilizohusisha watu wanaodaiwa kuwa wafuasi wa Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislamu (Jumiki), kwa kile kinachodaiwa kupinga Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
 
Vurugu hizo zilianza Jumamosi jioni baada ya wafuasi hao kuvamia maeneo mbalimbali, yakiwamo vituo vya polisi. Katika vurugu hizo, wafuasi hao wanadaiwa kuharibu mali, kuchoma moto magari na matairi ya magari, kurusha mawe, kuweka vizuizi katika barabara kuu za kutoka na kuingia Zanzibar.
 
Polisi wanadai pia kwamba makanisa matatu, moja la Assemblies of God na mawili ya Katoliki yalichomwa moto, huku baa tatu zikiporwa na kuchomwa moto na watu wanaodaiwa kuficha sura zao kwa vitambaa vyeupe. Habari zinasema, hadi kufikia jana jioni polisi walikuwa wamewatia mbaroni watu kadhaa.
 
Habari hizo bila shaka siyo tu zimewasikitisha wananchi wengi, bali pia zimeleta aibu na fedheha kubwa kwa nchi yetu mbele ya jumuiya ya kimataifa. Tunasema hivyo kwa sababu kwa muda mrefu sasa  taswira ya nchi yetu mbele ya jumuiya ya kimataifa imekuwa nzuri kiasi cha kuvutia watu wengi, wakiwamo watalii, wawekezaji na makundi mengine ambayo siyo tu yamevutiwa  na vivutio vingi vilivyopo, bali pia vimekoshwa na hali ya usalama, umoja na utulivu ambao tumekuwa nao tangu Tanganyika na Zanzibar ziungane mwaka 1964.
 
Ndiyo maana tunalaani vikundi vyote vilivyohusika katika kupandikiza chuki zilizosababisha vurugu hizo na uharibifu mkubwa wa mali katika visiwa hivyo na kusema kwamba lazima mamlaka husika zichukue hatua stahiki kuhakikisha wahalifu hao wanafikishwa katika vyombo vya sheria. Pamoja na kwamba vyombo vya sheria ndivyo pekee vyenye dhima ya  kusimamia sheria na kutoa adhabu kwa wahalifu, tunayo haki pia kama wananchi kusema lazima watakaotiwa hatiani kwa uhalifu huu wapewe adhabu kali ambayo hawataisahau milele.
 
Tunasema hivyo kwa kutilia maanani kwamba kuna kila dalili kuwa, nchi yetu  itaangamia iwapo watu wachache miongoni mwetu wataachiwa kutuvuruga kwa misingi ya kidini na kikabila kwa lengo la kutimiza malengo yao ya kisiasa. Pamoja na uhuru wa kuabudu na haki ya kila mwananchi kuishi mahali popote Tanzania  ambao umewekwa wazi katika Katiba, inakuwaje tunawaacha wendawazimu fulani wapokonye haki hiyo kwa kuchoma moto nyumba za ibada, baa, kubagua wananchi wenye asili ya Bara na kutishia uhai na mali zao? Mbona wananchi wa Zanzibar waishio Bara wanaishi kwa uhuru, amani na upendo?
 
Tunashangaa kuona kwamba hali ya amani visiwani imeendelea kuwa tete tangu kuanzishwa kwa vikundi vinavyohamasisha wananchi kuukataa Muungano. Lakini tunashangazwa zaidi na ukimya wa viongozi wa Serikali ya Mapinduzi (SMZ) na ya Muungano kukaa tu kama watazamaji, huku vikundi hivyo ambavyo  vinachukua sura ya kigaidi kila kukicha,  vikileta hofu kubwa kwa wananchi.
 
Ni jambo lisiloelezeka kwamba vikundi hivyo vya ubaguzi vinaweza kuachwa siyo tu viwagawe na kuwatisha wananchi, bali pia vifumbiwe macho na viongozi kiasi cha kuachwa viwadhalilishe kwa matusi ya nguoni waasisi wa Muungano wetu, yaani Mwalimu Julius Nyerere na Abeid Amani Karume. Hii ni hali isiyokubalika hata kidogo na tusione ajabu iwapo wananchi wa pande mbili za Muungano wanaoheshimu mchango wa waasisi wetu hao waseme sasa inatosha, hivyo waanzishe mapambano dhidi ya vikundi hivyo.
 
Sisi tunasema viongozi wa serikali zote mbili waache woga na wasimamie mambo ya msingi yaliyotuleta pamoja kama Watanzania. Katika kusema hivyo hatuna maana kwamba  wananchi wasiukosoe Muungano au kusema aina ya Muungano wanaoutaka. Hata kidogo. Tunachosema hapa ni kwamba tusiwaache watu wachache watumie nafasi hiyo kuisambaratisha nchi yetu kwa kisingizio chochote kile. Ndiyo maana tunasema  amani ya nchi yetu lazima tuilinde kwa nguvu zote.
  
Share this article :

+ comments + 1 comments

Anonymous
June 1, 2012 at 12:40 AM

Together we can go far

Post a Comment

KARIBU KATIKA WEBSITE YA KIJANJA, KUPATA HABARI MBALIMBALI ZA NDANI NA NJE YA NCHI. PIA UTAPATA MAMBO YA ACADEMIC. KARIBU SANA
 
Support : Creating Website | Johny Template | Mas Template
Copyright © 2011. GetInformedTz - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Mas Template
Proudly powered by Blogger