Home » » Vigogo Uhamiaji wana utajiri wa kutisha

Vigogo Uhamiaji wana utajiri wa kutisha

Written By Koka Albert on Monday, May 21, 2012 | 2:19 AM

TUME YA KUWACHUNGUZA YAANZA KAZI LEO, WAHAMISHIWA MIKOANI KIAINA
Mwandishi Wetu
KASHFA nyingine imeibuliwa katika Idara ya Uhamiaji.Taarifa mpya yenye kurasa tano, imewataja vigogo hao saba wakidaiwa kuwa na utajiri wa kutisha.Taarifa hiyo ambayo tunayo nakala yake, imedai kuwa vigogo hao wanamiliki mali na mamilioni ya shilingi katika akaunti zao binafsi.

Maofisa saba wametajwa kwa majina na vituo vyao vya kazi ambavyo ni Lindi, Dar es Salaam, Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (Kia) na Moshi.

Tuhuma hizo zimekuja wakati Tume Maalumu iliyoundwa kuchunguza tuhuma za ufisadi na utoaji wa vibali bandia kwa wageni, ikitajwa kuanza kazi juzi. Hata hivyo, habari kutoka wizarani zinaeleza kuwa timu hiyo itaanza rasmi kazi zake leo.

Habari za uhakika kutoka ndani ya Uhamiaji, zimedai kuwa baadhi ya wajumbe wa tume hiyo wamemhoji meneja wa benki moja kubwa ya Moshi ili kupata ukweli wa madai kuwa kigogo mmoja wa Uhamiaji mwenye cheo cha Naibu Kamishna (DCI), anamiliki akaunti ya fedha za kigeni.

Kigogo huyo anahusishwa pia na mtandao wa utoaji vibali bandia kwa raia wa kigeni wanaofanya kazi mkoani Kilimanjaro au kufanya kazi za kujitolea.
Ripoti hiyo imetaja taasisi 13, zikiwamo zisizo za kiserikali (NGO), hospitali na hoteli za kitalii zinazodaiwa wageni wake walipewa vibali bandia.

Mbali na kumhoji meneja huyo, inadaiwa pia walifanya mahojiano na uongozi wa kiwanda kimoja kinachodaiwa kukutwa na vibali bandia vya wageni 84.

Taarifa hizo zilidai kuwa maofisa wengine waandamizi wa Uhamiaji kutoka Makao Makuu, Dar es Salaam walitarajiwa kuwasili Moshi juzi kuungana na wenzao.

Baadhi ya maofisa waliotajwa katika ripoti hiyo kwamba wana utajiri ni wale waliokumbwa na uhamisho katika idara hiyo, Kia miezi mitatu iliyopita.

Katika ripoti hiyo, kigogo mmoja mwenye cheo cha DCI anadaiwa kukutwa na Sh700 milioni katika akaunti yake, achilia mbali kumiliki mali za mamilioni.

Mbali na maofisa hao kumiliki mamilioni ya fedha taslimu, pia wanadaiwa ‘kufanya kufuru’ ya kununua magari ya kifahari, nyumba na viwanja.

Ripoti hiyo inayodaiwa kuandikwa na Maofisa Uhamiaji wazalendo, imepinga hatua ya kuhamishwa kutoka kituo kimoja kwenda kingine, maofisa wanaotuhumiwa kukutwa na utajiri ambao haulingani na vipato vyao.
“Tunataka ufanyike ukaguzi wa kina wa vibali vyote vilivyotolewa kati ya 2009/2010, 2010/2011 hadi 2012 na taasisi zote zionyeshe nakala za vibali,” imedai.

Pia taarifa hiyo imependekeza wenzao wote wanaotuhumiwa kuwa na utajiri wa kutisha wachunguzwe na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru).
“Haikuwa sahihi kuwahamisha na kuishia hapo, walipaswa wapelekwe Takukuru wachunguzwe chanzo cha utajiri wao.”

Pia wametaka kigogo anayemiliki akaunti ya Dola, achunguzwe ili kujua alikuwa akifanya biashara gani nje ya utumishi wa umma na kama alilipa kodi kiasi gani.

Baadhi ya maofisa Uhamiaji wamependekeza kusimamishwa kazi kwa kigogo huyo katika kipindi hiki kwa hofu ya kuingilia na kuvuruga uchunguzi.

Wiki iliyopita, Kamishna Mkuu wa Uhamiaji, Magnus Ulungi aliwaambia waandishi wa habari kuwa imeundwa kwa tume ya kumchunguza kigogo huyo.
Hata hivyo, taarifa zilizopatikana jana zilisema tume hiyo imepanua wigo wa uchunguzi juu ya kuwapo kwa vibali bandia katika taasisi mbalimbali.

Kabla ya kuhamishiwa Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Shamsi Vuai Naodha alikaririwa akisema Kilimanjaro ni moja kati ya mikoa minane inayomtia kichefuchefu nchini.
Waziri huyo alisema baadhi ya watumishi wamekuwa wakijihusisha na mtandao wa uingiaji wahamiaji haramu nchini pia kutoa vibali bandia kwa wageni.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk Emmanuel Nchimbi alipoulizwa juzi kuhusu sakata hilo alisema ni vyema Uhamiaji ikapewa nafasi ya kuchunguza suala hilo kwa kuwa tayari imeshateua tume ya uchunguzi.

“Kamishna Mkuu wa Uhamiaji tayari amelifanyia kazi jambo hilo kwa uzito unaostahili. Tuwape nafasi walichunguze si vyema kuanza kuingilia katika hatua hii ya mwanzo,” alisema.

Wahamiaji haramu
Serikali, bila mafanikio, imekuwa ikichukua hatua mbalimbali kukomesha tatizo la wahamiaji haramu linalotajwa kuwa chanzo cha utajiri wa baadhi ya vigogo wa Idara ya Uhamiaji.
Miongoni mwa mikakati iliyowahi kutangazwa na Wizara ya Mambo ya Ndani ni pamoja na idara hiyo kufanya utafiti kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Mzumbe kubaini chanzo cha ongezeko la wahamiaji haramu nchini.
Akiwasilisha Bajeti ya Wizara yake bungeni mwaka 2007/2008 , aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi wakati huo, Joseph Mungai alisema matokeo ya utafiti huo ni kuisaidia Serikali kujua chanzo cha tatizo hilo na jinsi ya kupambana nalo kwa ufanisi zaidi.
Hatua nyingine zinazochukuliwa ni pamoja na maofisa Uhamiaji kushiriki katika vikao mbalimbali kuanzia ngazi ya vijiji, ili kuwapa wananchi elimu juu ya masuala yanayohusu uraia na jinsi ya kukabiliana na wahamiaji haramu; Kutoa elimu kwa umma kupitia vyombo vya habari; Kuweka mtandao wa kompyuta katika vituo vyote vya Uhamiaji ili kuviunganisha na makao makuu.

Pamoja na Serikali kutangaza mkakati huo miaka mitano iliyopita, wahamiaji haramu limeendelea kuwa tatizo sugu linalotia doa utendaji wa idara hiyo.
Share this article :

Post a Comment

KARIBU KATIKA WEBSITE YA KIJANJA, KUPATA HABARI MBALIMBALI ZA NDANI NA NJE YA NCHI. PIA UTAPATA MAMBO YA ACADEMIC. KARIBU SANA
 
Support : Creating Website | Johny Template | Mas Template
Copyright © 2011. GetInformedTz - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Mas Template
Proudly powered by Blogger