Home » » Ngaisi Islamoi: Sitaki ndoa, nisaidieni nisome kwanza

Ngaisi Islamoi: Sitaki ndoa, nisaidieni nisome kwanza

Written By Koka Albert on Friday, May 11, 2012 | 2:12 AM

Ngaisi Islamoi
Na Burhani Yakub, Tanga

“NINAOMBA jamii inisaide  nisome, niokoeni na ukatili huu wa wazazi wangu wanaotaka kuniozesha tena kwa nguvu kwa mwanaume asiye chaguo langu.

"Wazazi wangu wamesahau kwamba mimi bado ni mwanafunzi, najisikia vibaya  kweli nikose kusoma kwa sababu tu ya ndoa, mimi siwezi kukubali kuolewa.”

Hiyo ni kauli  na malalamiko  ya mwanafunzi wa darasa la saba katika Shule ya Msingi Kingo, Kata ya Masagaru Wilayani Kilindi, Ngaisi Islamoi (13) ambaye anaishi kama mkimbizi kwa diwani wa Kata ya Masaguru, Mohammed Makengwa kwa muda mrefu sasa.

Binti huyo anakizungumzia kwa huzuni kisa cha baba yake mzazi kujaribu kumwozesha kwa mwanaume kwa mahari ya ng’ombe watano.

Akiwa mafichoni nyumbani kwa Diwani Abubakari Makengwa, mwanafunzi huyo anaeleza historia yake kuwa alizaliwa mwaka 1999 mkoani Manyara akiwa mtoto wa pili katika familia ya Islamoi Kuresoi  na  mama Helena Lolamatu.

Anasema baadaye wazazi wake walihamia  Kilindi kwa ajili ya kutafuta ardhi ya mifugo pamoja na kilimo ndipo wakafikia kitongoji cha Chang’ombe, Kijiji cha Kwamba Kata ya Masagaru.

Wakiwa kijijini hapo wazazi wake walimwandikisha yeye na kaka yake Memarut Islamoi katika Shule ya Msingi Kingo na mwaka juzi mdogo wake aitwaye Loynyake pia aliandikishwa shuleni hapo.

“Miaka yote nilikuwa nahudhuria masomo bila matatizo na nashukuru Mungu maendeleo yangu darasani yalikuwa yakienda vizuri na walimu walinisifu kwa kujitahidi,” anaeleza.

Anaongeza kuwa mwanzo wa mateso yake ulikuwa mwaka jana wakati akiwa darasa la sita ambapo mwezi Oktoba baba yake  alimwamuru aache shule na kumjulisha kwamba anatakiwa kuolewa wakati wowote kwani tayari ameshaanza kutolewa mahari ya ng’ombe.

“Baba aliniambia wazi wazibila kificho kwamba lazima niache shule ili niolewe na kijana wa kutoka familia ya mzee mmoja mfugaji wa asili ya Kimasai kama sisi ambaye amepangiwa kulipa ng’ombe watano kama mahari na kwamba tayari ng’ombe dume mmoja alishakuwa ametolewa,”anasema.

Binti huyo mwanafunzi huyo anasema alipoelezwa kuhusu suala hilo la kuolewa hakumjibu chochote baba yake kwa kuwa kwa mujibu wa mila na desturi za kabila lao msichana au hata mwanamke haruhusiwi kujibishana na mwanaume.

Hata hivyo, anasema suala la kuolewa lilimshtua sana , likamnyima raha sana  na kumtoa machozi. Anaeleza kuwa alitafakari na kuanza kusaka mbinu za kujiokoa kwa kumfuata mama yake mzazi na kumwambia kuwa hataki kuolewa na badala yake anataka kuendelea na masomo na ndipo alipohakikishwa na mama yake kuwa atafanya kila njia ili kuhakikisha anasoma.

Anasema wiki moja baadaye wakati akijiandaa kwenda shule asubuhi alibaini kwamba  sare zake na daftari zilikuwa zimefichwa na alipomwuliza mama yake alimwambia kuwa baba yake ndiye aliyezificha kwa sababu hataki kusikia yeye akiendelea kusoma.

“Nilishindwa hata  kufanya mtihani wa darasa la sita wa kwenda la saba kwa sababu sare zangu zilifichwa , nikaenda kutoa taarifa kwa mwalimu mkuu,lakini baadaye baba akaniambia kuwa hata mwalimu hatanisaidia lolote kwani  ameshamalizana naye,” anasimulia.

Anaeleza kuwa jambo hilo lilimumiza sana kichwa akaamu kumfuata ofisa elimu wa Wilaya ya Kilindi na kumshitaki mzazi wake, lakini kwa sababu likizo ilikuwa imeanza alimtaka afanye subira hadi zifunguliwe shule mwezi Januari mwaka huu.

“Ilipofika Januari  na shule zilipofunguliwa nilimfuata tena ofisa elimu, kisha nikaenda kituo cha polisi,  lakini baba alipoitwa na kuhojiwa, hali kwangu ilikuwa mbaya  zaidi nyumbani kwani alisema nitamkoma kwa sababu nataka kumfunga na kwamba sitafanikiwa, nitaolewa tu.”

Anasema kuwa mambo yalipozidi kuwa magumu kwake aliamua kukimbilia kwa diwani wa Kata ya Masagaru kuomba maskani kwani alihisi maisha yake yalikuwa hatarini.

Binti huyo anaongeza kuwa hayuko tayari kuolewa kwa sasa bali kiu yake ni kusoma hadi kiwango cha chuo kikuu ili apate kazi itakayomsaidia kuwalea wazazi wake pamoja na wadogo zake kwa sababu familia yake inaishi maisha duni.

Anaongeza kuwa haamini kama kweli mahari ya ng’ombe watano iliyotolewa ili aolewe kama itawaweza kuwakwamua wazazi wake kwenye maisha duni bali anachoamini yeye ni kuwa kwa wakati huu elimu pekee ndiyo mkombozi.

“Nimeapa! Siko tayari kuolewa nataka kusoma hadi chuo kikuu ili nipate kazi nzuri ambayo itaniwezesha kuisaidia familia yangu ambayo inaishi maisha duni na siamini kama ng’ombe watano watasaidia,kama ni ng’ombe nitanunua nikianza kujitegemea nikiwa na kazi yangu,”anasema.
Share this article :

Post a Comment

KARIBU KATIKA WEBSITE YA KIJANJA, KUPATA HABARI MBALIMBALI ZA NDANI NA NJE YA NCHI. PIA UTAPATA MAMBO YA ACADEMIC. KARIBU SANA
 
Support : Creating Website | Johny Template | Mas Template
Copyright © 2011. GetInformedTz - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Mas Template
Proudly powered by Blogger