Home » » KTM yaagizwa kupunguza uzalishaji

KTM yaagizwa kupunguza uzalishaji

Written By Koka Albert on Tuesday, May 22, 2012 | 1:24 AM

Hulda Estomihi
BARAZA la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limekiagiza kiwanda cha nguo cha KTM kufanya uzalishaji chini ya asilimia 50.
Hatua hiyo imefuatia baada ya baraza hilo kubaini kuwa maji yanayotiririshwa kutoka kiwandani hapo bado yana kemikali.

Akizungumza jijini Dar es Salaam juzi, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa NEMC , Dk Robert Nitakamulenga alisema kiwanda hicho bado kinaendelea kufanya utafiti ili kubaini namna ya kuondoa kemikali hizo.

“Walituomba wakati bado wanaendelea na utafiti wapunguze uzalishaji kwasababu ilionekana maji yanayotiririshwa kutoka kiwandani hapo bado yana rangi,”alisema Dk Nitakamulenga.
Alisema tatizo lililopo sasa ni rangi na kwamba kulingana na viwango vinatakiwa viwe chini ya 300 lakini KTM wako kwenye 500.

Alisema kama utafiti huo utafanikiwa kuondoa rangi yote inayoonekana kwenye maji basi kiwanda hicho kitaruhusiwa kuendelea na uzalishaji wake kama ilivyokuwa  awali.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi huyo, kabla ya utafiti huo kiwanda hicho kilikuwa kikitiririsha maji yenye kemikali ambayo yalikuwa yakiingia katika mto Kizinga na hivyo kuhatarisha usalama wa watumiaji wa maji ya mto huo.

Alisema tangu mwaka 2006 kiwanda hicho kilikuwa kinatiririsha uchafu kwenye mkondo wa maji wa mto Kizinga na kwamba utafiti unaoendelea sasa unafanywa ili kuweza kutiririsha maji salama kwenye mto huo.

Alisema pia bado wanaendelea kutembelea viwanda mbalimbali ili kubaini viwanda ambavyo havikidhi sheria ya mazingira ili vichukuliwe hatua.
Share this article :

Post a Comment

KARIBU KATIKA WEBSITE YA KIJANJA, KUPATA HABARI MBALIMBALI ZA NDANI NA NJE YA NCHI. PIA UTAPATA MAMBO YA ACADEMIC. KARIBU SANA
 
Support : Creating Website | Johny Template | Mas Template
Copyright © 2011. GetInformedTz - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Mas Template
Proudly powered by Blogger