Home » » Serikali iangamize mtandao huu wa vyeti bandia

Serikali iangamize mtandao huu wa vyeti bandia

Written By Koka Albert on Friday, May 18, 2012 | 12:25 AM

HABARI  kwamba Jeshi la Polisi mkoani Kilimanjaro linamhoji mhadhiri mmoja wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Ushirika na Biashara kilichopo Moshi (Muccos), kwa tuhuma za kukutwa na vyeti vya kughushi vya vyuo vikuu kadhaa hapa nchini kwenye kompyuta yake,  bila shaka zitakuwa hazikuwashangaza  wengi.
 
Tunasema habari hizo hazikuwashangaza wengi kwa sababu kukamatwa kwa mhadhiri huyo ambaye hatutamtaja jina kwa sasa, kumekuja siku chache tu baada ya Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida), kuibua kashfa ya kuwapo askari 948 katika Jeshi la Polisi na Jeshi la Wananchi wa Tanzania wenye vyeti bandia vya elimu.
 
Mkurugenzi Mkuu wa Nida, Dickson Maimu alisema jijini Dar es Salaam mwanzoni mwa wiki kwamba mamlaka hiyo iligundua  watumishi hao kutumia cheti kimoja cha elimu na watu wengine wakati zoezi la uandikishaji  watumishi wa Serikali lilipoanza. Alikuwa akitoa taarifa ya utekelezaji wa Mradi wa Vitambulisho vya Taifa kwa waandishi wa habari.
 
Tunaposema habari za kashfa hiyo zitakuwa hazikuwashangaza wengi hatuna maana kwamba hazikuwa za kughadhabisha, kufedhehesha wala kufadhaisha. La hasha. Tunachosema ni kwamba kukamatwa kwa mhadhiri huyo kumekuja wakati kukiwapo kwa taarifa za kuzagaa kwa vyeti bandia vya chuo hicho cha Muccos vinavyosemekana kuuzwa kama njugu mitaani, ikiwa ni kazi ya mtandao mmoja ndani ya chuo hicho.
 
Uongozi wa Muccos umekiri kuwa, kwa muda mrefu sasa zimekuwapo tetesi nyingi juu ya kuwapo kwa watu walioajiriwa katika taasisi mbalimbali nchini wakitumia vyeti vya chuo hicho, ingawa hawakuwahi kusomea hapo. Lakini  tamko la Nida lililotolewa mwanzoni mwa wiki la kugundulika kwa askari hao 948 walioajiriwa kwa kutumia vyeti bandia pamoja na  kukamatwa kwa mhadhiri wa Muccos kwa tuhuma za kukutwa na vyeti vya kughushi vya vyuo vikuu mbalimbali kwenye kompyuta yake ndiyo hasa  matukio yaliyofumbua macho ya watu wengi.
  
Tunachoshindwa kuelewa ni jinsi usalama wa nchi yetu unavyoweza kuwekwa rehani kirahisi namna hiyo. Inakuwaje askari wote hao 948 wapewe ajira katika vyombo vyetu vya ulinzi na usalama pasipo kupitia katika mchakato mkali wa kuchunguza kila hatua ya maisha ya askari hao, kuanzia siku  ya kuzaliwa hadi siku wanayoomba ajira katika jeshi husika. Mchakato huo ungepaswa pia ubainishe na uthibitishe pasipo shaka kwamba vyeti vya elimu na nyaraka za utambulisho za askari hao ni halisi.
 
Vinginevyo utatoaje ajira kwa askari mwenye hati na nyaraka zilizochakachuliwa na utegemee ufanisi wa kiweledi siyo tu wakati wa mazoezi ya kijeshi, bali pia wakati wa vita? Ni kitu gani kitamzuia askari huyo kuelekeza silaha yake kwa askari wenzake badala ya adui? Hali hiyo haina tofauti na kutoa ajira kwa injinia kihiyo anayejenga madaraja na majengo kwa kiwango cha chini na kuhatarisha maisha ya watu. Hivyohivyo kwa daktari kihiyo anayefanyia wagonjwa operesheni kwa kubahatisha na kuwasababishia vifo au vilema vya maisha.
 
Waziri mpya wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Shamsi Vuai Nahodha, ambaye hadi majuzi alikuwa pia Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi akilisimamia Jeshi la Polisi nchini, amesema hana taarifa za kuwapo askari walioajiriwa katika majeshi yetu kwa kutumia vyeti bandia. Kauli hiyo imeibua hasira na wasiwasi wa wananchi ambao wamewataka wakuu wa JWTZ  na Jeshi la Polisi wajiuzulu kwa kile walichokiita kuhatarisha usalama wa nchi yetu.
 
Sasa tumeelewa kwa nini baadhi ya shule zetu zinatoa wanafunzi wasiojua kusoma au kuandika kwa sababu wanafundishwa na baadhi ya walimu walioajiriwa kwa kutumia vyeti bandia. Kumbe watumishi wengi walioajiriwa katika sekta ya umma na pengine hata ya binafsi waliajiriwa kwa kutumia vyeti bandia. Serikali inatakiwa kuusambaratisha mtandao unaochapisha vyeti hivyo sasa, vinginevyo vizazi vijavyo vitakuwa  vihiyo.
   
Share this article :

+ comments + 1 comments

May 21, 2012 at 2:50 AM

Bila ivyo kiwango cha elimu kitakuwa kibovu

Post a Comment

KARIBU KATIKA WEBSITE YA KIJANJA, KUPATA HABARI MBALIMBALI ZA NDANI NA NJE YA NCHI. PIA UTAPATA MAMBO YA ACADEMIC. KARIBU SANA
 
Support : Creating Website | Johny Template | Mas Template
Copyright © 2011. GetInformedTz - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Mas Template
Proudly powered by Blogger