Home » » Sitta, Lowassa wazungumzia kujiunga na Chadema

Sitta, Lowassa wazungumzia kujiunga na Chadema

Written By Koka Albert on Wednesday, May 23, 2012 | 2:48 AM

*SITTA ADAI WANAOKIMBILIA HUKO NI MAGAMBA YEYE SI MMOJA WAO, LOWASSA AMSHANGAA LEMA, ASEMA KUHAMIA CHADEMA SI SIRI, 

Waandishi Wetu

SIKU chache baada ya aliyekuwa Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema kuwataja mawaziri wawili na mmoja aliyewahi kuwa Waziri Mkuu kwamba, wameomba kujiunga na chama hicho cha upinzani, wawili kati yao wamejitokeza na kuzungumzia madai hayo.

Waziri Mkuu aliyejiuzulu, Edward Lowassa na Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta ambao walitajwa na Lema, jana kwa nyakati tofauti walibeza madai hayo.

Jumamosi iliyopita, Lema akiwa wilayani Sengerema, Mwanza alisema mawaziri watatu, akiwamo mmoja aliyewahi kuwa waziri mkuu wameiomba kujiunga na Chadema lakini mmoja kati yao amekataliwa na wengine mchakato wa kuyakubali maombi yao unaendelea.

Katika mkutano huo, Lema aliwataja mawaziri hao kwa jina moja kuwa ni Sitta, Lowassa na waziri mwingine ambaye tunahifadhi jina lake kwa kuwa hakupatikana jana kuzungumzia madai hayo.

Msimamo wa Sitta
Sitta alipuuza madai hayo akiyaita ya kitoto na kueleza kuwa kwa hadhi yake, hawezi kuomba kujiunga Chadema na kusubiri majibu kama amekubaliwa au la.

“Yaani mimi niombe kwenda Chadema halafu nikae kabisa huku nikisubiri wanijibu! Huo ni upuuzi na jambo hili haliwezekani na si kweli hata kidogo. Kama Lema kasema hivyo, basi huo ni utoto na siasa za kihuni,” alisema Sitta.

Sitta huku akicheka aliongeza: “Sasa nimeomba kwa nani na kwa njia ipi ya mdomo au maandishi? Mimi siyo gamba. Ni mtu mwadilifu siwezi kujiunga katika utaratibu wa kuchukua magamba ndani ya CCM.”

“Wao Chadema wanachukua tu kila mtu. Wakienda kwenye mikutano pia wanachukua tu watu, sasa hivi wanachukua magamba CCM. Mimi nawatakia kila heri katika kuchukua magamba CCM.”

Sitta alisema yeye ni mwanasiasa makini na mwadilifu hawezi kukaa chungu kimoja na magamba... Wanalofanya kuchukua magamba ya CCM ni faraja hata kwa Katibu Mkuu Wilson Mukama.”

Mbunge huyo wa Urambo Mashariki, alisema kuchukua magamba CCM ni sawa na mtu ambaye anakwenda kwa jirani ambaye nyumba yake imezungukwa na takataka kisha akamsaidia kuzisomba kwenda kuzitupa... Hapo si lazima ufurahie bwana?

Alisema kama angekuwa anajiunga na Chadema wangemkumbatia akisema: “Kama wanakwenda watu wadogo wanaandaa sherehe kubwa, nikienda mimi...?

Majibu ya Lowassa
Jana, Lowassa naye alipuuza madai hayo ya Lema akisema hajawahi kuomba kujiunga na Chadema huku akisisitiza: “Kama ingekuwa hivyo isingekuwa siri. Ningetangaza uamuzi wangu kupitia vyombo vya habari.”

Lowassa alitoa kauli hiyo baada ya gazeti hili kumtaka azungumzie madai ya Lema kwamba aliomba kujiunga na chama hicho cha upinzani lakini akakataliwa.

“Kama ningeomba kuingia Chadema ningetangaza kwenye vyombo vya habari. Sijasikia hayo na sitaki kusema chochote zaidi,” alisema  Lowassa na kisha kukata simu.

Slaa amshangaa Lema

Alipoulizwa kuhusu madai hayo ya Lema, Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willbrod Slaa alisema hawezi kuzungumzia kauli ya mtu.

“Tabia yangu huwa sipendi kuzungumzia kauli aliyoitoa mtu hivyo alichokisema Lema mtafuteni yeye mwenyewe afafanue kwani atakuwa anajua alichokisema kina maana gani,” alisema Dk Slaa.

Dk Slaa alisema: “Badala ya kukaa na kuzungumzia kauli ya mtu, kinachotakiwa ni kujadili jinsi gani ya kuhakikisha tunapunguza ugumu wa maisha kwa mwananchi wa hali ya chini.”

“Tuache kuzungumza kauli za watu hapa sasa kinachotakiwa kila mmoja wetu kwa nafasi yake  atizame ni jinsi gani atahakikisha anamkomboa mwananchi kwa kupunguza gharama za maisha.”

Lema ang’ang’ana

Hata hivyo, jana alipotakiwa kufafanua kauli yake baada ya kuelezwa kwamba aliowataja wabeza madai yake, Lema aliendelea kusisitiza kwamba alichosema ni cha kweli.

“Wanakataa tu kisiasa, lakini nilichosema ni cha kweli na (kesho), leo katika mkutano wangu wa Singida, pamoja na kuwarudia hawa niliowataja nitawataja wengine pamoja na wabunge wa CCM ambao wapo tayari kujiunga na Chadema.”

Katika madai yake ya kwanza aliyotoa Jumamosi iliyopita katika mkutano uliofanyika kwenye Viwanja vya Mnadani, Lema alisema viongozi wenye uchungu na taifa hili ndani ya CCM na ambao wamekuwa hawafurahishwi na ubadhirifu wa mali za nchi, wamekuwa wakifanya mazungumzo kutaka kujiunga na Chadema.

Alisema kwa vile chama chake kimejiandaa kuingia madarakani kwa kutumia nguvu ya umma, ndiyo maana mawaziri wa Serikali ya CCM wameomba kujiunga nacho ili kusaidiana kwa pamoja kwenda kuingia madarakani mwaka 2015.

“Lakini, Lowassa tumemkataa. Tunataka wachapa kazi na wenye mioyo ya kweli katika mapambano ya kupigania haki na kuondoa dhuluma kwa Watanzania,” alisema Lema.

Lema alidai kuwa mawaziri hao (waliokubaliwa) wanasubiri muda muafaka ufike waweze kutangaza rasmi kujiunga na chama hicho, kutokana na kile kilichodaiwa kuchoshwa na mwenendo mzima wa uongozi na utendaji serikalini na ndani ya CCM, hususan suala la kuwalinda watu wanaotuhumiwa kwa ubadhilifu.
Share this article :

Post a Comment

KARIBU KATIKA WEBSITE YA KIJANJA, KUPATA HABARI MBALIMBALI ZA NDANI NA NJE YA NCHI. PIA UTAPATA MAMBO YA ACADEMIC. KARIBU SANA
 
Support : Creating Website | Johny Template | Mas Template
Copyright © 2011. GetInformedTz - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Mas Template
Proudly powered by Blogger