Home » » Kesi ya Mahalu:Mkapa Kortini Mei 8

Kesi ya Mahalu:Mkapa Kortini Mei 8

Written By Koka Albert on Tuesday, May 1, 2012 | 2:21 AM

WAKILI MARANDO ASEMA NI SHAHIDI MUHIMU,WATAMLETA KUTOA USHAHIDI WA MANENO
Tausi Ally
RAIS Mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa, anatarajiwa kupanda kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Mei 8, mwaka huu kumtetea aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Italia, Profesa Costa Mahalu.Wakili  anayemtetea Balozi Mahalu, Mabere Marando alisema jana kwamba Mkapa atapanda kizimbani siku moja baada ya Profesa Mahalu kumaliza kutoa utetezi wake.

Awali, akizungumza mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Ilvin Mgeta Wakili Marando alisema Mei 8, kutakuwa na shahidi mwingine wa mwisho muhimu ambaye hata hivyo, hakumtaja.
Alipoulizwa kuhusu shahidi huyo nje ya Mahakama, Marando alimtaja kuwa ni Rais Mstaafu Mkapa na baadaye alipopigiwa simu kutoa ufafanuzi zaidi alisema: “Mkapa ni shahidi wa Mahalu hivyo atafika mahakamani kutoa ushahidi wake kwa maneno.”

Alipoulizwa kwamba atatoa ushahidi gani mwingine mbali ya ule alioutoa kwa maandishi alisema: “Safari hii atafika mahakamani kutoa kile anachokifahamu kwa maneno.”

Kuhusu kama kiongozi huyo mstaafu wa taifa amekubali kufika mahakamani, Marando alisema: “Kwani kuna nini? Yeye ni shahidi wa Mahalu. Si kuja kutoa ushahidi tu!”

Profesa Mahalu na aliyekuwa Ofisa Utawala wa ubalozi huo, Grace Martin wanakabiliwa na shtaka la uhujumu uchumi na kuisababishia Serikali hasara ya Euro 2,065,827.60.

Akihojiwa na Wakili Mwandamizi wa Serikali, Ponziano Lukos dhidi ya mashtaka hayo yanayomkabili, Profesa Mahalu alidai kuwa Serikali ilitengua ubalozi wake Februari, 2006 bila ya kupeleka barua ya uamuzi huo kwa  Serikali ya Italia ambayo iliendelea kumtambua kama balozi na kumpa heshima zote ikiwamo kualikwa kwenye hafla mbalimbali, kuagwa na kupewa tuzo mbalimbali.

Balozi Mahalu alidai kuwa mwishoni mwa Aprili, 2006 alirejea nchini na Agosti mwaka huohuo aliitwa kwenye Ubalozi wa Italia na kupewa tuzo.

Akihojiwa kuhusu mikataba miwili iliyotumika kununua jengo la Ubalozi wa Tanzania nchini Italia alidai kuwa kulikuwepo na mikataba miwili ya ununuzi wa jengo hilo ambayo yote aliiwasilisha serikalini.

Alidai  kuwa aliiarifu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa kwamba wanategemea kununua jengo kwa mikataba miwili na aliinunua nyumba hiyo kwa faida ya Serikali na yeye hakupata kitu chochote.

Kuhusu madai kwamba aliingia mikataba miwili kwa ajili ya kununua jengo hilo bila ya kuwepo mtu mwingine wa kushuhudia, Balozi Mahali alidai kuwa yeye alikuwa  mwakilishi wa Tanzania nchini Italia na alipata maelekezo ya kununua jengo hilo baada ya Wizara ya Ujenzi kujiridhisha kutokana na tathmini waliyokuwa wameifanya.

“Hakukuwa na mtu mwingine aliyeshuhudia lakini, nilipata mamlaka kisheria ya kufanya hivyo kutoka kwa aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Jakaya Kikwete,” alidai.

Alidai kuwa suala la kununua jengo la ofisi ya ubalozi kwa kutumia mikataba miwili, Kikwete ambaye sasa ni Rais wa Tanzania, alikuwa akilifahamu na hata alipotembelea Italia hilo lilikuwa jambo la kwanza kutaka kulifahamu kutoka kwa aliyekuwa akiliuza.

“Rais Kikwete akiwa Waziri, alitembelea Italia na suala la mikataba miwili lilikuwa jambo la kwanza alilouliza kutaka ufafanuzi. Wakati tunafanya mazungumzo alimwuliza, muuzaji na alimjibu kwamba ndiyo utaratibu wa Italia wanapouza jengo kwa nchi kwa gharama ya chini huingia mikataba miwili, mmoja wa kiofisi na mwingine wa kibiashara,” alidai na kuongeza kuwa baada ya Kikwete kupata ufafanuzi huo alicheka.

Profesa Mahalu alidai kwa sifa alizokuwa nazo na kwa ucha Mungu wake, hawezi kutenda makosa yanayomkabili mahakamani.
Februari 29, mwaka huu Profesa Mahalu akijitetea, alidai kuwa Kikwete akiwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, alimpa nguvu ya kisheria ya uwakilishi wa ununuzi wa jengo hilo.

Akiongozwa na Wakili  Marando kutoa utetezi huo, Profesa Mahalu alidai kuwa Septemba 2001, alipewa Nguvu ya Kisheria ya Uwakilishi (Special Power of Attorney) ya ununuzi wa jengo hilo Kikwete.

“Aliniagiza kununua jengo hilo la ubalozi. Machi 24, 2004 nilimwandikia barua Rais Kikwete na kwenye barua hiyo niliambatanisha nyaraka za ununuzi wa jengo hilo baada ya kulinunua.”

Alidai kuwa pia alipeleka barua hiyo kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Naibu Waziri wa wizara hiyo,  Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Mhasibu Mkuu wa Serikali, Waziri wa Ujenzi, pamoja na Waziri wa Fedha.

Alidai kuwa baada ya kuandika barua hiyo na kuiambatanisha na nyaraka hizo za ununuzi wa jengo hilo, hakuwahi kuhojiwa juu ya ununuzi huo.

Alisema ushahidi uliotolewa na shahidi wa tatu wa upande wa mashtaka, Steward Migwano Aprili 23, 2008 pamoja na vielelezo vya ushahidi kuhusu ununuzi wa jengo hilo unalingana na wa kwake.

Lakini akasema ushahidi wa shahidi wa tano wa upande wa mashtaka, Isdory Kyando  kuhusu gharama za bei ya ununuzi wa jengo hilo unatofautiana na wa kwake kwenye bei rasmi na kwamba kulikuwepo na mikataba miwili ambayo Serikali iliiridhia. Alidai kuwa mikataba yote ipo mikononi mwa Serikali kwa muda mrefu.

Profesa Mahalu alisema pia kwamba Agosti 3, 2004 katika majadiliano ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, katika Mkutano wa 16, kikao cha 39, Rais Kikwete akiwa Waziri wa Mambo ya Nje alitoa hotuba  iliyoonyesha kuwa ununuzi wa jengo hilo ulifuata taratibu zote za kisheria  na kwa makubaliano ya Euro 3 milioni.

Alidai kuwa kauli yake na ya Rais Kikwete juu ya ununuzi wa jengo hilo bei zinalinga na kwamba hakuwahi kupata malalamiko yoyote wala kuhojiwa juu ya uhalali wa matumizi hayo ya fedha.
Pia alidai kuwa hakuwahi kuona upande wa mashtaka ukipeleka kesi mahakamani hapo kama mama mwenye jengo hilo la ubalozi alikuwa amelipwa fedha pungufu ya bei  iliyokubaliwa na kwamba katika mgogoro huo pia hakuwahi kuona mama huyo akipeleka malalamiko kuwa hakuwahi kulipwa.
Share this article :

Post a Comment

KARIBU KATIKA WEBSITE YA KIJANJA, KUPATA HABARI MBALIMBALI ZA NDANI NA NJE YA NCHI. PIA UTAPATA MAMBO YA ACADEMIC. KARIBU SANA
 
Support : Creating Website | Johny Template | Mas Template
Copyright © 2011. GetInformedTz - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Mas Template
Proudly powered by Blogger