Home » » Vikongwe wanne wauwawa Geita

Vikongwe wanne wauwawa Geita

Written By Koka Albert on Friday, May 11, 2012 | 2:08 AM

 
Salum Maige,Geita
WANAWAKE wanne ambao ni vikongwe wameuawa kwa kupigwa kwa mawe kisha miili yao kuteketezwa kwa moto na wananchi katika Kijiji cha Lwezera wilayani Geita, mkoani Geita kutokana na imani za kishirikina.

Habari zilizopatikana mjini Geita jana na kuthibitishwa na Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Deusidedit Nsimike zilisema vikongwe hao wameuawa baada ya kutuhumiwa kuwa wanafuga fisi kwenye makazi yao ambao ni tishio kwa maisha ya watu na mifugo kijijini hapo.

Mbali na mauaji hayo, familia za vikongwe hao zimeachwa bila makazi, baada ya nyumba zao zaidi ya 15 kuteketezwa kwa moto na wananchi hao ambao ni zaidi ya 1,000  waliokuwa wamekusanyika na  kuanzisha msako mkali wa kila kaya ambako vikongwe hao walikuwa wakiishi.

Mauaji ya vikongwe hao yametokea siku moja baada ya juzi mtoto Diana Salu (5), mwanafunzi wa darasa la awali, mkazi wa kijijini hapo kunyakuliwa na fisi akiwa na wenzake wakati wakitokea kibandani kununua mafuta ya taa aliyoagizwa na wazazi wake mnamo  saa 2:30 usiku.

Baada ya mtoto huyo kunyakuliwa na fisi, watoto wenzake walienda kutoa taarifa nyumbani na kijihada za kumtafuta mtoto huyo  kwa kushirikia na wananchi wa kijiji hicho hazikufanikiwa hadi maiti yake ilipoonekana kesho yake, ikiwa kwenye uwanja wa shule ya msingi Lwezera huku ikiwa imenyofolewa utumbo na mguu wa kushoto.

Ofisa Mtendaji wa Kata ya Lwezera ambaye pia ni mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya kata hiyo, Fransice Kadilo alisema tukio hilo la mtoto kuliwa na fisi lilitokea Mei 7, mwaka huu na ndipo wananchi walipoanza kuwatuhumu vikongwe hao kufuga fisi hao waliosababishaa kifo cha mtoto Diana.

‘’Walipokuta maiti ya mtoto huyo ikiwa kwenye uwanja huo, walikuwa wengi ndipo walianza kufanya vurugu hizo za kuwapiga vikongwe na miili yao kuichoma moto. Baadaye nilipiga simu polisi, wakawa wamefika eneo la tukio na kuthibiti vurugu hizo,’’alisema mtendaji huyo.

Ilivyokuwa
Baada ya kundi hilo la wananchi kutoka uwanjani kushuhudia maiti ya mtoto huyo, lilianza msako wa kila nyumba na  kufanya mauaji hayo kwa kutumia mawe na silaha za jadi yakiwemo mapanga na marungu huku nyumba 15 za vikongwe hao na wengine, zikiketezwa kwa moto.

Ofisa mtendaji huyo aliwataja vikongwe waliouawa katika tukio kuwa ni Kulwa Mashana (65), Laurencia Bangili (62), Ester Konya (55) na Rose Mabeshi (42), ambao wote ni wakazi wa kijiji cha Lwezera.

Aliyekuwa Mkuu wa wilaya ya Geita, Philemon Shelutete (ambaye ameachwa katika mabadiliko ya juzi ya wakuu wa wilaya) aliyefika eneo la tukio hilo, mbali na kuwaonya wananchi kuacha tabia ya kujichukulia sheria mkononi, alilitaka Jeshi la Polisi lililokuwa katika eneo hilo kuzuia vurugu hizo, kufuatilia kwa kina chanzo chake kuwachukulia hatua waliohusika katika mauaji hayo.

Kaimu Kamanda Nsimike alithibitisha kutokea kwa vifo vya kina mama hao na kwamba polisi wanaendesha oparesheni ndogo ili kuwakamata watu waliohusika na mauaji hayo.

Kaimu Kamanda huyo alifafanua kuwa marehemu waliuawa kwa awamu mbili. “Ni kwamba kundi hilo la watu waliwaua wanawake wawili kwa tuhuma za ushirikiana na baada ya muda mfupi waliwauwa watu wengine wawili na kuchoma nyumba kadhaa,”alisema.

Alisema katika awamu ya kwanza ya msako huo, watu wawili wamekamatwa na kuthibtisha taarifa kwamba idadi kubwa ya watu wameyakimbia makazi yao wakihofia kukamatwa na polisi.

“Itakuwa ni kama opareshini ndogo maana mauaji ya aina hii yanapofanyika yanahusisha watu wengi, tunakwenda kwa awamu ya pili na baada ya hapo tunaweza kutoa taarifa ya kina,”alisema Nsimike.

Hili ni tukio la pili kutokea wilayani Geita, kwani  tukio kama hilo liliwahi kutokea katika Kijiji cha Rwamgasa baada ya vikongwe watatu kuuawa kwa kupigwa kwa mawe na miili yao kuteketezwa kwa moto huku nyumba zao zikiharibiwa kwa kuchomwa moto kwa tuhuma za ushirikina.
Share this article :

Post a Comment

KARIBU KATIKA WEBSITE YA KIJANJA, KUPATA HABARI MBALIMBALI ZA NDANI NA NJE YA NCHI. PIA UTAPATA MAMBO YA ACADEMIC. KARIBU SANA
 
Support : Creating Website | Johny Template | Mas Template
Copyright © 2011. GetInformedTz - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Mas Template
Proudly powered by Blogger