Home » » Uhuru na fedha vinavyochangia kuwaharibu wanafunzi wa vyuo vikuu

Uhuru na fedha vinavyochangia kuwaharibu wanafunzi wa vyuo vikuu

Written By Koka Albert on Tuesday, June 5, 2012 | 4:20 AM

Fredy Azzah
JENGA taswira kichwani ya kijana wa Kitanzania, mtoto wa mkulima ama mfugaji kutoka kijijini ambaye tangu azaliwe hakuwahi siyo tu kumiliki, lakini hata kushika noti ya Sh 10,000!

Maisha yake yote  hajawahi kuishi katika nyumba ya umeme ama kuangalia runinga, ukitoa shuleni alikosoma kwa miaka minne (sekondari ya kawaida) ama miaka miwili (sekondari ya juu). Burudani, starehe na anasa havikuwa sehemu ya maisha yake.

Leo kijana huyo anabahatika kuchaguliwa kujiunga na elimu ya juu ambapo Serikali inampa mkopo wa fedha.Anashika fedha kwa malaki, huku akiishi  mjini kwenye starehe na anasa za kila aina.
Kama kijana huyu limbukeni hakutayarishwa kisaikolojia mara tu baada ya kudahiliwa chuoni, kwa nini asighilibike kwa kutenda mambo ambayo hata hayawani hawezi kuyatenda?

Hivi ndivyo ilivyo sasa katika vyuo mbalimbali vya elimu ya juu nchini, kumekuwapo na uporomokaji mkubwa wa maadili miongoni mwa wanafunzi wa vyuo vikuu, kiasi kwamba matendo ya ulevi, uasherati na anasa yamekuwa sehemu ya maisha yao ya kila siku.

Mfano mzuri ni taarifa ya hivi karibuni iliyoonyesha kuongezeka kwa maambukizi ya ugonjwa wa Ukimwi kwa wanafunzi wa vyuo vikuu vya Dar es Salaam na Mzumbe.

Katika taarifa iliyotolewa mbele ya Kamati ya Bunge inayoshughulikia Ukimwi mwishoni mwa Mei mwaka huu, kiwango cha maambukizi ya VVU katika chuo Kikuu cha Mzumbe na maeneo yanayokizunguka chuo kimefikia asilimia 6.5 ambacho ni zaidi ya kiwango cha maambukizi kitaifa ambacho ni asilimia 5.7.

Kwa chuo Kikuu cha Dar es Salaam, mwaka 2001 kulifanyika zoezi la kuwapima wanafunzi ambapo asilimia 2.3 ya waliopima walibainika kuwa na maambukizi ya ugonjwa huo.

Kwa nini hali hii imefikia hatua hiyo? Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Taaluma) Profesa Makenya Maboko, anasema kwa kiasi kikubwa hali hiyo inachangiwa na  wanafunzi wengi  kujiona sasa wako huru na wana fedha zao wenyewe.

“Pamoja na hayo siwezi kusema moja kwa moja kuwa wengi wanakuja kuharibikia chuoni, wengi nadhani huwa wanatoka huko wakiwa tayari wameshaharibika. Ni vema labda watu wa elimu na saikolojia wakafanya utafiti, ili kuona kama kweli  wanaharibikia chuoni ama la,” anasema.

Kwa upande wake,  Mkuu wa Idara ya Saikolojia ya Elimu na Masomo ya Mitalaa ya Shule Kuu ya Elimu  katika chuo hicho,  Dk Kitila Mkumbo, anaeleza kuwa  ukitoa sababu za wanafunzi kuwa huru mno na kumiliki fedha, wazazi nao wanachangia kwa sababu  baadhi yao hawana utamaduni wa kuzungumza na watoto wao kwa minajili ya kuwaasa kuhusu maisha.

Anasema pamoja na vyuo vikuu vingi kuwa na ofisi za ushauri kwa wanafunzi, vitengo hivyo vimeshindwa kufanya kazi zake kwa kiwango cha kuridhisha kwa sababu ya kukosa nyenzo.

Hata hivyo, anasema  siyo kweli kuwa wanafunzi  wengi wanaharibika wakiwa vyuoni na kuwa mambo mengi wanayofanya kama kwenda katika kumbi za muziki yanatokana na  tabia za ujana.

“Wengi tabia zao ni nzuri tu na ndiyo maana hata taaluma zao siyo mbaya, kwenda disko na mambo mengine kama hayo ni mambo ya kawaida tu kwa vijana,” anasema Dk Mkumbo.

Mbinu za kuwasaidia
Mhadhiri mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na mtaalamu wa Saikolojia,  Profesa Mwajabu Posi anasema ili kukabiliana na tatizo la maadili vyuoni, ni vema  wazazi na walimu wakajenga tabia ya kukaa na vijana wao na kuwaeleza hali halisi ya maisha vyuoni.

“Wakati sisi tunasoma, ilikuwa ukifika darasa la nane, mwalimu anakwambia fulani wewe tabia yako siyo nzuri, fanya hivi ili ufanikiwe uko unakokwenda. Mzazi pia na yeye anakueleza yake,” anabainisha.

Kwa upande wake, mhadhiri mstaafu wa chuo hicho,  Profesa Ruth Meena anasema ni vema  kwa  wanafunzi wanaojiunga na vyuo vikuu kupata elimu ya kuyakabili mazingira ya chuo.

Elimu hiyo anaeleza kuwa ni muhimu kwa sababu maisha ya chuo yanatofautiana kwa kiasi kikubwa na maisha ya shule ambayo kwa kawaida  wanafunzi wanakuwa chini ya uangalizi wa karibu wa wazazi na walimu.

“Shuleni kila kitu kipo kwenye ratiba, lakini ukifika chuoni unapewa ratiba ya darasani tu, mengine yote inatakiwa ujipangie ratiba mwenyewe,” anasema na kuongeza: 

“Baada ya kuona  tatizo hili, mimi mwenyewe nilianzisha  darasa la kukutana angalau kwa wiki moja na kukaa na hawa wanaotarajia kujiunga na vyuo vikuu. Tunawaeleza   mazingira watakayokwenda kukutana nayo, jinsi ya kuyakabili na mambo mengine yatakayowajenga kisaikolojia.” 

Anasema kuwa mafunzo hayo  ni matokeo ya tafiti  zilizobaini  kuwapo kwa   mabadiliko makubwa ya  kijamii  na kiteknolojia  yanayotokea duniani na kuathiri    wanafunzi  wa vyuo vikuu ambao wengi hujiunga na vyuo bila ya kupata mbinu za kumudu maisha ya vyuo.

Profesa Meena anasema   pamoja na mambo mengine, mafunzo hayo yalilenga kujitambua, kujiwekea malengo, kutumia muda kwa ufanisi,  kuhimili  msukumo wa makundi, kuchagua marafiki bora, kukabili msongo wa mawazo  na mbinu za kufanikisha ndoto zao za  maisha.

 “Mwanafunzi anapobadilisha maisha kutoka ya  sekondari ambako  kuna  ulinzi wa shule na wazazi kwenda  chuo kikuu ambako  anajisimamia mwenyewe,  anapaswa  kupata maelekezo  sahihi  ili  aweze kujitambua na    kujipangia malengo  yake  na kuyatekeleza  kikamilifu,’’anaeleza.

Aidha, Profesa Meena anasema kuna  tafiti  zinazoonyesha kuwa  wanafunzi wengi  wanaojiunga vyuo vikuu, hushindwa  kutimiza ndoto zao kielimu  kutokana na  kutoandaliwa vyema kuhusu namna ya  kuzikabili  changamoto za  ujana na  masomo  wakiwa  vyuoni. 

Ni kwa sababu hii anasema wanafunzi wengi  hujikuta wakitumbukia  kwenye vishawishi  vya  makundi mabaya, starehe, uvivu,  uvutaji wa bangi, migomo isiyo ya lazima  na  uasherati.

Mbali ya mafunzo  na ushauri wa kisaikolojia, Mhadhiri msaidizi katika Shule ya Uandishi wa Habari na Mawasiliano ya Umma ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Abdallah Katunzi anasema ni vema wanafunzi wakashauriwa juu ya vile wanavyotaka kusoma wakifika vyuo vikuu.

Hii ni kwa sababu uzoefu unaonyesha wanafunzi wengi wamekuwa wakisoma kozi wasizo na uwezo nazo ama kuzipenda. 

Akitolea  mfano wa fani ya uandishi wa habari,  Katunzi anasema kumekuwa na dhana potofu kwa baadhi ya wanafunzi kudhani kila mtu anaweza kusomea uandishi wa habari na kozi nyingine zinazohusiana na fani hiyo.

"Tunahitaji wanafunzi bora kwa kila fani na siyo kila mtu anaweza kusomea uandishi wa habari au kozi nyingine kwa urahisi kama haelewi undani wake," anabainisha.
Share this article :

+ comments + 1 comments

November 11, 2017 at 6:50 AM

eToro is the #1 forex trading platform for newbie and professional traders.

Post a Comment

KARIBU KATIKA WEBSITE YA KIJANJA, KUPATA HABARI MBALIMBALI ZA NDANI NA NJE YA NCHI. PIA UTAPATA MAMBO YA ACADEMIC. KARIBU SANA
 
Support : Creating Website | Johny Template | Mas Template
Copyright © 2011. GetInformedTz - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Mas Template
Proudly powered by Blogger