Home » » Hofu ya bajeti kukwama yatanda

Hofu ya bajeti kukwama yatanda

Written By Koka Albert on Tuesday, June 12, 2012 | 1:23 AM

KAMATI YA UONGOZI YA BUNGE YAKUTANA NA WAZIRI WA FEDHA  
Waandishi Wetu
 HOFU imetanda mjini Dodoma juu ya kuwapo kwa uwezekano wa kukwama kwa Bajeti ya Serikali ya mwaka wa fedha 2012/13 inayotarajiwa kuwasilishwa Bungeni keshokutwa na Waziri wa Fedha, Dk William Mgimwa.

Dk Ngimwa atawasilisha bajeti ambayo alilazimika kuifumua upya baada ya kuteuliwa kuchukua nafasi hiyo baada ya mabadiliko ya Baraza la Mawaziri yaliyofanywa mapema mwezi uliopita na Rais Jakaya Kikwete na kumweka nje ya aliyekuwa akiongoza wizara hiyo, Mustafa Mkulo.

Waziri Mkuu, Mizengo Pinda jana alinukuliwa akizungumza katika kikao cha kutoa mwongozo kwa wabunge wote (briefing) kwamba Dk Mgimwa aliomba ridhaa ya Rais kufumua bajeti hiyo upya ili iweze kwenda sawa na mtizamo wake kama kiongozi wa wizara, hali iliyosababisha kuchelewa kwa vitabu vya bajeti kwani baadhi viliandaliwa upya.

Pinda alikuwa akijibu hoja za wabunge wa Serengeti (CCM) Dk Steven Kebwe, Mbunge wa Nzega (CCM), Dk Hamis Kigwangallah na Mbunge wa Viti Maalumu (Chadema), Pauline Gekul ambao kwa nyakati tofauti walihoji sababu ya kuchelewa kwa vitabu vya bajeti kinyume cha Kanuni za Bunge, hali iliyowanyima fursa ya kuijadili kwa kina.

Hata hivyo, jitihada hizo za Dk Mgimwa zinaonekana kutowaridhisha wabunge ambao katika vikao vya kamati waliyakataa mapendekezo ya bajeti nyingi kutokana na upungufu wa kutozingatiwa kwa vipaumbele.

“Kwamba bajeti itapata wakati mgumu hilo halina ubishi licha ya kwamba wabunge wa CCM tunabanwa na kanuni ya ‘three lines whip,’ si unajua ukikataa kuunga mkono bajeti unaweza kupoteza ubunge wako? Lakini kwa ujumla hali ni ngumu sana,” alisema mmoja wa wabunge wa CCM kutoka mikoa ya Kanda ya Magharibi.

Jana jioni Kamati ya Uongozi ya Bunge ikiongozwa na Spika wa Bunge, Anne Makinda; Waziri Mkuu, Pinda; Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Uhusiano na Uratibu), Steven Wassira na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi ilikuta na Mgimwa “kuweka mambo sawa” kabla ya bajeti kuwasilishwa Bungeni.

Habari kutoka ndani ya kikao hicho zinasema miongoni mwa ajenda kuu zilikuwa ni mjadala kuhusu bajeti zilizokataliwa na Kamati za Bunge ikiwamo Bajeti kuu ya Serikali ambayo ilikataliwa na Kamati ya Fedha na Uchumi kutokana na kutotengwa kwa fedha za kutosha kwa ajili ya shughuli za maendeleo.

Ratiba ya vikao vya Bunge la bajeti inaonyesha kuwa kamati za wabunge za vyama zinakutana leo baada ya kipiondi cha maswali na majibu. Masikio yote yataelekezwa ndani kamati ya CCM ambako kunatabiriwa kuwapo kwa mvutano kabla ya kuwa na msimamo wa pamoja wa kuunga mkono Bajeti.
Baadhi ya wabunge wakiwamo wa CCM nao wameonyesha msimamo wa kuikataa wakitilia shaka kama itakidhi mahitaji ya wananchi, hasa kupunguza makali ya maisha.

Walisema Bajeti hiyo ya Sh15 trilioni huenda isilete matumaini kutokana na ile ya mwaka 2011/12 kushindwa kuonyesha tija.

Mbunge wa Mwibara (CCM), Kangi Lugola alisema walitarajia bajeti ya mwaka huu itaongeza fedha katika kukabiliana na sekta za elimu, afya na kilimo lakini matokeo yake fedha zimeendelea kupunguzwa.

“Walimu bado wanadai mabilioni ya fedha, mikopo elimu ya juu bado ni tatizo, kilimo chetu hakikidhi na hivyo kukosekana uhakika wa chakula katika maeneo mengi sasa badala ya bajeti kuongezwa inapungua,” alisema Lugola.

Mbunge wa Ludewa (CCM), Deo Filikunjombe alisema Watanzania wasitegemee jipya katika Bajeti ijayo. Alisema Bunge litatenga fedha katika kila sekta lakini, tatizo ni kufika zilikotengwa na kusaidia maendeleo ya Watanzania na kukuza uchumi wa nchi.

Mbunge wa Arumeru Mashariki(Chadema), Joshua Nassari alisema Watanzania wasitegemee jipya katika Bajeti ijayo kwani ni ya madeni… “Bajeti hii mimi naiita ni ya madeni, kwani katika wizara kama ujenzi, kiasi kikubwa fedha kimetengwa kulipia miradi ambayo tayari imeanza.”
Share this article :

Post a Comment

KARIBU KATIKA WEBSITE YA KIJANJA, KUPATA HABARI MBALIMBALI ZA NDANI NA NJE YA NCHI. PIA UTAPATA MAMBO YA ACADEMIC. KARIBU SANA
 
Support : Creating Website | Johny Template | Mas Template
Copyright © 2011. GetInformedTz - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Mas Template
Proudly powered by Blogger