Home » » Mnyika kumkatia rufaa Naibu Spika

Mnyika kumkatia rufaa Naibu Spika

Written By Koka Albert on Monday, June 25, 2012 | 4:05 AM

Raymond Kaminyoge
MBUNGE wa Ubungo, John Mnyika amesema anakusudia kukata rufaa kwa Kamati ya Bunge ya Kanuni dhidi ya Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai kutokana na uamuzi wa kumtoa bungeni wiki iliyopita.

Wiki iliyopita Mnyika alitolewa bungeni baada ya kukataa kufuta kauli yake kuwa ‘Rais Jakaya Kikwete ni dhaifu’.

Jana, katika taarifa yake kwa vyombo vya habari, Mnyika alisema anakusudia kukata rufaa dhidi ya Ndugai, ili kuwe na mjadala mpana wa kibunge utakaoweka kumbukumbu sahihi.
 Alisema uamuzi huo wa kukata rufaa kwa Kamati ya Kanuni za Bunge, unalenga kupata haki. Mnyika alisema kutamka kuhusu udhaifu wa Rais, si kumtukana wala siyo kutumia jina lake kwa dhihaka.

“Pamekuwapo na propaganda za kudai kuwa kauli hiyo ni matusi, chanzo ni udhaifu wa Naibu Spika Ndugai, kwa kunihukumu kwa kutumia kanuni tofauti na tuhuma iliyotolewa,” alisema.

Alifafanua kwamba, “Naheshimu taasisi ya urais na umri, naamini pia katika matumizi ya lugha za kidiplomasia, hata hivyo, niliamua kuusema ukweli kwa lugha ya moja kwa moja ili ujumbe ufike kwa mamlaka zote.”
Alisema hata viongozi wa dini na taasisi mbalimbali, wamekuwa wakisema hadharani kuhusu udhaifu huo wa rais.

Kuhusu Bajeti, Mnyika alisema wabunge wamekuwa na udhaifu kutokana na Katiba kuweka nguvu kubwa kwa Rais, kwamba wasipopitisha Bajeti anaweza kulivunja Bunge.

“ Woga huo wa Rais kulivunja Bunge ndiyo maana wamekuwa wakipitisha Bajeti kwa kauli za `ndiyo’ kwa asilimia 100, hata kama kuna maeneo ambayo wanayapinga,” alisema Mnyika katika taarifa yake hiyo.

Mbali na kukata rufaa, aliongeza, “Bunge litakapokuwa likijadili utekelezaji wa bajeti katika Ofisi ya Rais 2012/13, nitaeleza hatua ambazo Rais anapaswa kuchukua kufanikisha ahadi alizozitoa kwa Watanzania.” 
Alisema anaamini, Rais Kikwete anayo fursa ya kurekebisha, ili kuongeza nguvu zake katika kupanua wigo wa mapato na hatimaye kuongeza kiwango cha fedha za maendeleo.

Share this article :

Post a Comment

KARIBU KATIKA WEBSITE YA KIJANJA, KUPATA HABARI MBALIMBALI ZA NDANI NA NJE YA NCHI. PIA UTAPATA MAMBO YA ACADEMIC. KARIBU SANA
 
Support : Creating Website | Johny Template | Mas Template
Copyright © 2011. GetInformedTz - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Mas Template
Proudly powered by Blogger