Home » » Chadema, CUF waungana kuikataa Bajeti

Chadema, CUF waungana kuikataa Bajeti

Written By Koka Albert on Sunday, June 17, 2012 | 2:23 AM

LIPUMBA  AAGIZA WABUNGE WAKE KUIPINGA KWA NGUVU,CHADEMA WASEMA HAIFAI  

 MWENYEKITI wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba ameungana na wenyeviti wa vyama vingine vya siasa vya upinzani kupinga Bajeti ya Serikali ya 2012/2013, akisisitiza kuwa kamwe chama chake na wabunge wake, hawataiunga mkono.

Lipumba aliiponda Serikali akisema kuwa nchi inahitaji uongozi wenye uwezo wa kusimamia rasilimali za nchi na matumizi ya fedha za umma.

Aliikosoa Serikali akisema imeshindwa kubuni vyanzo vipya vya mapato huku kukiwa na udhaifu mkubwa katika usimamizi wa matumizi ya fedha za umma zinazokusanywa kutoka katika vyanzo vya mapato vilivyopo.

Kwa kauli hiyo, Lipumba ameungana na wenyeviti wenzake wa vyama vya upinzani, Freeman Mbowe wa Chadema na James Mbatia wa NCCR-Mageuzi ambao pia waliiponda Bajeti hiyo wakisema haina jipya.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti baada ya kuwasilishwa kwa Bajeti hiyo Alhamisi usiku, wenyeviti hao walisema hakuna matumaini kwa Watanzania kupitia Bajeti hiyo kwani fedha nyingi zimelundikwa kuwanufaisha wachache huku umma ukiambulia patupu.

Kwa upande mwingine, wabunge wa CCM juzi walikutana kwa zaidi ya saa tano katika kikao ambacho waliibua hoja ya kutaka kuchunguzwa kwa Mfuko Mkuu wa Serikali kwa maelezo kwamba kuna dalili za kuwapo ufisadi.

Habari kutoka ndani ya kikao hicho  kilichoongozwa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda zinasema msingi wa hoja hiyo iliyotolewa na Mbunge wa Simanjiro, Christopher Ole Sendeka na kuungwa mkono na wabunge wengine, ni kutokuwapo kwa uwiano kati ya fedha zilizokusanywa na Mamlaka ya Mapato (TRA) pia kutoka kwa wahisani na zile zilizopelekwa katika wizara na idara za Serikali.

Prof Lipumba

Akizungumza na waandishi wa habari, Profesa Lipumba akizungumza na waandishi wa habari jana katika ukumbi wa mikutano wa Ofisi za Upinzani Bungeni, alisema CUF ina sababu za msingi kupinga Bajeti hiyo kwa sababu hailengi kumsaidia kabwela kuondokana na umaskini na gharama kubwa za maisha.

“Bajeti ya mwaka 2011/12 Serikali ilieleza kwamba inatambua changamoto zinazowakabili wananchi, lakini hadi sasa hali bado ni ngumu. Mfumuko wa bei umefikia asilimia 20, bei ya mafuta bado ipo juu. Mfumuko wa bei ya chakula umefikia asilimia 24 na sasa inasababisha asilimia 50 ya mapato ya Watanzania wengi kutumika kwa chakula,” alisema Prof Lipumba.

Profesa Lipumba alisema, Serikali imekuwa bingwa wa misamiati katika bajeti na kutangaza mambo mengi, bila kujali vipaumbele ambavyo imeshindwa kuvitekeleza.

“Tunasema sekta muhimu kama kilimo, katika jedwali namba 26 katika bajeti, la mgawo wa fedha, bado fedha zilizotengwa kwa kilimo ni kidogo tofauti hata na makubaliano na nchi za SADC ambayo yanapendekeza nchi kutenga walau asilimia 10 ya bajeti yake, ili kuhakikisha kilimo kinaongezwa na kuondoa tatizo la uhaba wa chakula,” alisema.

Alisema kuna miradi inayotengewa fedha kila wakati wa Bajeti, kama wa kuzalisha Megawati 61 za umeme wa Nyakato, Mwanza na ule wa Kinyerezi, lakini kwa miaka mitano sasa, hakuna kilichokamilika.

Matumizi hewa

Alisema katika Bajeti ya mwaka 2011/12 Serikali ilipanga kufanya sensa ya watumishi kulipwa mishahara madirishani ili kubaini wafanyakazi hewa, lakini katika Bajeti ya mwaka huu, mpango huo haujaelezwa kabisa, wala hatua iliyofikiwa mwaka uliopita.

Alisema tatizo kubwa linaloikabili Serikali ni ombwe la uongozi, hakuna nidhamu ya matumizi ya fedha za umma, viongozi wanajiamulia mambo bila kuulizwa zikiwamo safari za nje na kulipana posho bila kuwa na utaratibu.

Profesa Lipumba alisema inashangaza katika hesabu za Bajeti iliyopita, kuna fedha nyingi zimetajwa kukusanywa ndani na nje ya nchi, lakini bado kuna miradi iliyopewa fedha chini ya asilimia 30 ya mahitaji.

Alisema kukosekana ubunifu katika Bajeti, kumesababisha Serikali kuanzisha kodi ya wenye magari ambao watataka kuweka majina yao badala ya namba na kwamba makadirio yake ya Sh5 milioni zilizopangwa zitawezesha kupatikana kwa watu 10 tu badala ya kupunguza kodi hiyo ili kupata watu wengi zaidi.

“Hapa inaonyesha ni jinsi gani uandaaji wa Bajeti yetu una matatizo. Kama unaweza kupanga kodi ya Sh5 milioni na ukategemea kupata watu 10, kwa nini kodi hiyo isipunguzwe na kupata watu wengi zaidi, sidhani hata hawa wanaoandaa Bajeti kama hii wanaipitia vizuri,” alisema Profesa Lipumba.

Mfumo wa Bajeti

Profesa Lipumba alisema mfumo wa Bajeti ya Tanzania unakabiliwa na matatizo mengi, kwanza, kutoshirikisha wadau kwa muda mwafaka, kukosa mipango ya kupata vyanzo vipya vya kodi na kutopangwa kwa uwiano mzuri wa  makusanyo na matumizi na kuandaliwa kwa vipaumbele.

Alieleza kuwa inashangaza Serikali, katika Bajeti  kueleza mapato ya ndani kuwa taifa linatarajia kukusanya kiasi cha Sh8.7 trilioni lakini hapohapo matumizi ya kawaida yanakuwa Sh10.3 trilioni.

“Serikali inahitaji kukusanya fedha za ndani walau ziweze kutumika katika matumizi yote ya kawaida kabla ya kuomba misaada kwa wahisani,”alisema Lipumba.

Alisema kwa Serikali kuendelea kutenga fedha kidogo kwa mambo ya maendeleo kiasi cha Sh4.5 trilioni pekee ni tatizo kwani ni asilimia 30 tu ya fedha zote na kulingana na mipango ya Serikali na mahitaji yake inapaswa ifikie walau asilimia 40.

Alisema Bajeti hiyo inapishana sana na Mpango wa Serikali wa miaka mitano, Mpango wa Kupunguza Umaskini na Kukuza Uchumi Tanzania (Mkukuta) namba mbili na Malengo ya Milenia.

“Serikali inapaswa kuacha kuwa bingwa wa siasa kwa kutangaza mambo mengi bila kuwa na uwezo wa kuyatekeleza. Kama sasa katika taarifa ya hali ya uchumi iliyotolewa bungeni na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Uhusiano na Uratibu), Stephen Wassira kuwa Serikali ina mpango wa kuanza kutekeleza mpango wa ujenzi wa Reli ya Arusha- Musoma, Mtwara – Mbamba Bay, wakati reli muhimu kama ya kati bado inawashinda, kila siku inaelezwa utafanyika ukarabati mkubwa,” alisema Lupumba.

Mbowe na Mbatia

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alisema, “Hakuna mkakati wa makusudi wa kupunguza matumizi ya Serikali. Ahadi ya Serikali ya kupunguza matumizi kwa kupunguza posho zisizo na tija na matumizi mengine haikutekelezwa.”

Mbowe ambaye pia ni Kiongozi wa Upinzani Bungeni, alisema ameshangazwa na kutokuwapo nyongeza za mishahara kwa watumishi wa umma, badala yake fedha nyingi kulundikwa katika matumizi ya kawaida ya Serikali.

“Mfumo wa kodi kama mlivyosikia ni mbaya kabisa, hakuna kinachoashiria kwamba mkulima wa kawaida atapunguziwa mzigo na badala yake wanaendelea kuwanufaisha wafanyabiashara wa vyakula kwa kuwaruhusu kuagiza nje bila kodi, hiki naweza kusema ni kichekesho,” alisema Mbowe na kuongeza:

“Hakuna ubunifu kwenye kupanua wigo wa kodi. Tungeweza kusikia katika construction (ujenzi) ambayo inakua haraka na inachukua asilimia 18 ya pato la taifa kwamba tungetoza kodi huko, badala yake ni yaleyale ya siku zote, kodi kwenye sigara, vinywaji na bia.”

Naye Mwenyekiti wa NCCR- Mageuzi, James Mbatia alisema kwamba, lazima Serikali ijifunze kubadilika, kwani kilichotangazwa kwenye Bajeti yake ni marudio ya miaka yote.

“Huwezi kuchukua hela zote ukaulundikia utawala halafu ukawaacha wananchi bila kitu, hicho ndicho tulichokiona leo. Sh10 trilioni ni kwa ajili ya mishahara na watumishi na matumizi ya kawaida, maendeleo ambako ndiko wananchi waliko kumeachwa tena kutegemea fedha za wafadhili,” alisema Mbatia ambaye pia ni Mbunge wa kuteuliwa na Rais.

Alisema, hata fedha zilizotengwa kwa ajili ya kujenga reli ni kidogo kwani mahitaji ni Sh3 trilioni na Serikali imetenga Sh1 trilioni kwa ajili ya kugharimia sekta nzima ya miundombinu.
Share this article :

+ comments + 1 comments

October 16, 2017 at 10:50 PM

eToro is the ultimate forex broker for novice and pro traders.

Post a Comment

KARIBU KATIKA WEBSITE YA KIJANJA, KUPATA HABARI MBALIMBALI ZA NDANI NA NJE YA NCHI. PIA UTAPATA MAMBO YA ACADEMIC. KARIBU SANA
 
Support : Creating Website | Johny Template | Mas Template
Copyright © 2011. GetInformedTz - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Mas Template
Proudly powered by Blogger