Home » » Makada wa CCM watishia kuhamia Chadema

Makada wa CCM watishia kuhamia Chadema

Written By Koka Albert on Saturday, June 16, 2012 | 3:02 AM

BAADHI ya Wenyeviti wa Serikali za Vijiji, Viongozi wa kimila(Malwaiganani),Wajumbe wa Serikali za Vijiji  sanjari na viongozi wa CCM wilayani Simanjiro wametishia kuhamia Chadema endapo serikali ikishindwa kuwarudishia eneo la ekari 2000 wanayodai kuporwa na Mwenyekiti wa CCM wilayani humo,Brown Ole Suye.

Wakizungumza na Waandishi wa Habari jana viongozi hao  zaidi ya 100 ambao wamefunga safari ya kutoka wilayani Simanjiro hadi jijini Arusha  pia walimtaka Rais Jakaya Kikwete kuingilia kati mgogoro huo kwa kuwa wananchi wilayani humo wamepoteza imani ya serikali yao.

Olamayan Ole Langaa,ambaye ni mzee wa mila wilayani humo maarufu kama Laigwanani alisema kwamba yeye kama kada wa CCM na kiongozi wa kimila wilayani  humo amechoka kuona wananchi wakinyanyaswa kwenye ardhi yao.

Alisema kwamba amepoteza imani na serikali ya chama tawala kwa kumkumbatia Mwenyekiti wa CCM wilayani humo,Ole Suye ambaye alimtuhumu kwamba amepora ardhi ya ekari 2000 katika eneo la Lebosoit.

“Wananchi tumepoteza imani na serikali ya CCM haiwezekani  kiongozi wa chama ambaye tunamtegema apore ardhi yetu kubwa kiasi hiki”alisema Ole Langaa

Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Lebosoit A,Yohana Siriri na Mwenyekiti wa CCM Tawi la Lebosoit,Elisha Karua  walimshutumu mwenyekiti huyo wa CCM wilaya kwa madai kwamba amepora ardhi kubwa na kuwaacha wananchi wakihangaika kutafuta njia za kupita,maeneo ya malisho na kuokota kuni.

Walisema kwamba malalamiko dhidi ya uporaji wa ardhi hiyo walishayafikisha mbele ya uongozi wa chama, serikali pamoja na kwa mbunge wa jimbo hilo lakini hakuna jitihada zozote zilizofanyika kutatuliwa zaidi ya kulindana.

Walisema kwamba jumla ya watu 36 wameshtakiwa kwa kuingiza mifugo ndani ya eneo hilo kitendo ambacho ni unyanyasaji wa haki za wananchi dhidi ya ardhi yao.

Hatahivyo,walisema kwamba wamepoteza imani na serikali ya CCM kwa  madai kwamba imekuwa ikikumbatia watu wachache kwa maslahi yao binafsi na kuwatupa wanyonge.

“Wananchi na wanachama wa CCM wamepoteza imani na CCM na hivi karibuni wametuambia wako njiani kuhamia Chadema kwa kuwa wameona serikali yao imeshindwa kuwasaidia kuhusu tatizo hili la ardhi”walisema kwa nyakati tofauti

Nao Makada wa CCM,Marco Sangeti,Lenganasa Sipei ,Lengai Ole Makoo pamoja na Michael Lengara walisema kwamba wamechoka na tabia ya chama chao kuwakumbatia watu wachache kwa maslahi yao binafsi na kuwatupa wanyonge.

Walisema kwamba uamuzi wa wao kutishia kuhamia upinzani uko sahihi kwa kuwa wameona serikali ya chama chao imeshindwa kuwasikiliza pamoja na kuipa dhamana ya kuendesha dola.

Hatahivyo, Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Sukuro,Kaaya Mulelo alisema kwamba hivi karibuni aliletewa jumla ya kadi 650 na vijana wa Jumuiya ya Umoja wa Vijana ya CCM(Uvccm) wilayani humo wakitaka kuhamia upinzani kwa madai ya kuchoshwa na ukandamizaji ndani ya chama chao hatahivyo aliwazuia kwa kuwatuliza wasiondoke.

Alipotafutwa Mwenyekiti wa CCM wilayani humo,Ole Suye ili ajibu madai hayo alisema kwamba yeye hajapora ardhi ya mtu yoyote kwa kuwa ardhi inayolalamikiwa ya ukubwa wa ekari 2000 anaimiliki kihalali huku akiwataka wanaomlalamikia wafuate taratibu husika.

Akizungumzia kitendo cha makada wa CCM wanaotishia kuhamia upinzani Ole Suye alisema kwamba makada hao wanapaswa kufuata taratibu za chama za kuwasilisha malalamiko yao mbele ya vikao ili waweze kusikilizwa badala ya kufanya maamuzi yenye hasira.
Share this article :

Post a Comment

KARIBU KATIKA WEBSITE YA KIJANJA, KUPATA HABARI MBALIMBALI ZA NDANI NA NJE YA NCHI. PIA UTAPATA MAMBO YA ACADEMIC. KARIBU SANA
 
Support : Creating Website | Johny Template | Mas Template
Copyright © 2011. GetInformedTz - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Mas Template
Proudly powered by Blogger