Home » » Kukamatwa kwa mbunge kwaibua mapya

Kukamatwa kwa mbunge kwaibua mapya

Written By Koka Albert on Monday, June 4, 2012 | 1:28 AM

Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila
Raymond Kaminyoge
WAKATI Mbunge wa Bahi, Omar Badwel anatarajiwa kufikishwa mahakamani leo kwa tuhuma za kupokea rushwa, Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila ameilipua Kamati ya Bunge ya Serikali za Mitaa (LAAC) kuwa imekithiri kwa rushwa.

Kutokana na tuhuma hizo, Kafulila amemtaka Spika wa Bunge, Anne Makinda kuvunja kamati hiyo, vinginevyo yeye atajiondoa.

Pia mbunge huyo ameitaka Kamati ya Maadili kulitumia Bunge kumvua ubunge, Badwel, kutokana na tuhuma za kupokea rushwa zinazomkabili.

Kafulila alisema hayo jijini Dar es Salaam jana alipozungumza na waandishi wa habari huku akisisitiza kuwa, wananchi hawatakuwa na imani tena na kamati hiyo.

“Ikumbukwe Juni 13, 2011 nilieleza bungeni namna wabunge wa Kamati ya LAAC wanavyoomba rushwa kwa watumishi wa Serikali, huku nikimtaja kwa jina Mbunge wa Bahi, Omary Badwel kuwa ni miongoni mwao,” alisema Kafulila ambaye pia ni mjumbe wa kamati hiyo.

Mkurugenzi wa Idara ya Upelelezi ya Takukuru, Alex Mfungo alisema juzi kuwa mbunge huyo anatarajiwa kufikishwa mahakamani leo.

Hata hivyo, Spika wa Bunge, Anne Makinda alisema hana taarifa zozote za mbunge huyo kukamatwa.

“ Sina taarifa za mbunge kukamatwa na Takukuru, kama ni kweli tutaletewa taarifa rasmi ndipo ninaweza kuzungumzia suala hilo,” alisema Makinda kwa simu.

Awali, Kafulila alisema licha ya kutoa taarifa hiyo bungeni na kumwandikia Spika kuhusu vitendo vya rushwa vya baadhi ya wajumbe, hakuna hatua yoyote iliyochukuliwa.

“ Nilijitoa mhanga kwa kutaja majina ya wabunge wanaoomba rushwa kwa watumishi wa Serikali, lakini hatua hazikuchukuliwa, sasa leo Takukuru wamemtia mbaroni mmoja wao, bado hamuamini,” alisema Kafulila.

“ Sasa naomba niweke wazi kwamba kama Spika hataivunja kamati hii na kuunda nyingine nitajiondoa kwenye kamati kwa sababu itakuwa imepoteza imani kwa wananchi,” alisema Kafulila.

Alisema kamati hiyo imepoteza uhalali na sifa za kuendelea kuzikagua hesabu za serikali za mitaa kwa sababu wajumbe wake wanatuhumiwa kwa rushwa.

Kafulila alisema ni wajibu wa Spika kutafakari upya kuhusu hadhi ya kamati hii na kuipanga upya kwa kuzingatia masilahi ya umma.

Kamati hiyo inayoongozwa na Mbunge wa Vunjo, Augustine Mrema, ndiyo yenye jukumu la kusimamia hesabu za serikali za mitaa.

“Serikali legelege ni matokeo ya Bunge legelege kwa kuwa ni kazi ya Bunge kusimamia na kuidhibiti Serikali kikatiba,” alisema Kafulila.

Mbunge huyo wa Kigoma Kusini aliitaka Bunge kuweka azimio la kumvua ubunge Badwel kwa vitendo vyake vya rushwa.

“ Kamati ya Maadili ya Bunge ifanye hivyo ikiwa ni hatua za kinidhamu kuchukuliwa kwa mbunge huyo kwa tukio hilo la aibu,” alisema.

Kafulila alisema hata mabunge ya Jumuiya za Madola ambalo Tanzania ni miongoni mwao, huchukua hatua za kinidhamu za kuwavua wabunge wanaotuhumiwa kwa makosa ya aibu kabla ya mahakama hazijatoa uamuzi.

Kwa mujibu wa Kafulila, Bunge la Uingereza limeshachukua hatua za kuwavua ubunge watuhumiwa zaidi ya 59 ili kujenga imani ya wananchi kwa Bunge lao.

“Kwa hiyo nafahamu kwa kutumia azimio, Bunge lina uwezo wa kumvua madaraka mbunge yeyote ambaye amefanya vitendo vya aibu vya kuliaibisha Bunge,” alisema.

Kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ibara ya 71(1) (d) Mbunge anaweza kupoteza nafasi yake ikiwa itathibitishwa kwamba amevunja masharti ya Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma.

Mbunge huyo wa Bahi, Badwel, na Mbunge wa Mbozi Mashariki, Godfrey Zambi wote wa CCM ni miongoni mwa wabunge waliotajwa na Kafulila (NCCR-Mageuzi) katika Bunge la bajeti mwaka jana kwamba aliwakuta wakiomba rushwa kwa viongozi wa halmashauri ambayo hakuitaja.

Juzi saa 9.00 alasiri, Badwel alikamatwa na Takukuru akidaiwa kupokea rushwa kutoka kwa watumishi wa Serikali katika Hoteli ya Peacock jijini Dar es Salaam.
Share this article :

Post a Comment

KARIBU KATIKA WEBSITE YA KIJANJA, KUPATA HABARI MBALIMBALI ZA NDANI NA NJE YA NCHI. PIA UTAPATA MAMBO YA ACADEMIC. KARIBU SANA
 
Support : Creating Website | Johny Template | Mas Template
Copyright © 2011. GetInformedTz - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Mas Template
Proudly powered by Blogger