Home » » Samaki wanaovuliwa kwa mabomu wanasababisha saratani

Samaki wanaovuliwa kwa mabomu wanasababisha saratani

Written By Koka Albert on Monday, June 4, 2012 | 1:33 AM

 Hivi ndivyo vifaa vinavyotumika kutengeneza bomu, mbolea ya chumvi, dongo, utambi na kibati.
Mwandishi Wetu
JUMAMOSI iliyopita katika safu hii ya Mada ya Jumamosi, tulieleza kwa kina jinsi uvuvi haramu unavyofanyika kwatika maeneo ya karibu na fukwe za Bahari ya Hindi jijini Dar es Salaam.

Leo tunaendelea na sehemu ya pili ya makala haya tukiangaza athari za kimazingira zinazosababishwa na uvuvi huu wa kutumia baruti pia athari za kiafya wanazoweza kuzipata walazi wa samaki hawa.

Daktari bingwa katika Chuo Kikuu cha Sayasi za Tiba, Muhimbili, Henry Mwakyoma, anaweka wazi kuwa, samaki hao huweza kusababisha saratani na maradhi ya figo.

 
Dk Mwakyoma anasema, mwili wa samaki hufyonza sumu yote iliyoko katika bomu lile mara baada ya kupigwa na kwamba sumu hiyo huweza kupita aidha katika nyama au mapafu yake. “Sumu inayoingia mwilini mwa samaki inategemeana na mchanganyiko uliotumika kutengeneza bomu hilo,” anasema Dk Mwakyoma.

Kwa bomu lililotengenezwa kwa mbolea ya chumvichumvi, mafuta ya taa, baruti, na dongo au ‘waterexplosive gel, daktari anathibitisha kuwa  na sumu kali na husababisha maradhi ya saratani na figo.
“Endapo mtu atakula samaki wa aina hiyo mara kwa mara, anakuwa kwenye hatari kubwa ya kupata maradhi ya saratani na figo,” anasema mtaalamu huyo.

 Dk Mwakyoma anaongeza kuwa, bidhaa kama mbolea ya chumvichumvi na baruti ni sumu hatari kwa mwili wa mwanadamu hata kama samaki huyo atakuwa amepikwa.

“Kwa sababu samaki ana nyama laini, hupikwa kwa muda mfupi, na hivyo sumu ile hubaki katika nyama ikiwa na nguvu,” anafafanua Dk Mwakyoma.

Anasema, samaki wa aina hiyo anapoliwa huchukua muda mrefu kiasi kwa madhara yake kuanza kuonekana kwa binadamu kwa kuwa utengenezaji wa mabomu hayo ya kienyeji, wakati mwingine hutumia mbolea za viwandani na baruti.

Samaki wa mabomu
Wataalamu wa masuala ya uvuvi, wanasema, samaki aliyevuliwa kwa mabomu hutambulika kwa urahisi.
Mishipa ya damu iliyoko katika matamvua ya Samaki aliyevuliwa kwa mabomu hupasuka hivyo huvilia damu na kupata rangi nyekundu.

Dalili nyingine ni  utumbo  wake kusagika na kutawanyika, bandama kupasuka na mwili wa samaki huyo huacha tundu unapobonyezwa hata kwa kidole.
 
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, David Mathayo alikiri kuwepo kwa watu wanaonunua vifaa vya kutengeneza  mabomu kwa visingizo vya kulipulia miamba.
“Tukipata majina yao,watashughulikiwa mara moja, lakini ukiishutumu idara yote ya uvuvi, utakuwa umekosea,” alisema.

Athari za kimazingira
Watalaamu wa Mamlaka ya Uvuvi (Fisheries) wanasema kuwa, uvuvi wa kutumia mabomu unaathiri kwa kiasi kikubwa mazalia na malisho ya samaki ambayo kitaalamu yanaitwa ‘Coral Reef’.

Festo Mtanga ambaye ni Ofisa Uvuvi kutoka Idara ya Uvuvi ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi, anasema mabomu na baruti huathiri chanzo kikuu cha mazalia ya samaki. Anasema utengenezwaji wa mabomu haya kienyeji ndicho chanzo cha uharibifu  mkubwa wa mazali ya samaki kutokana na uwezo wa zana zinazotumika kutengeneza mabomu husika.

“Mabomu yanayotumika sasa ni yale yanayotumika vitani, kubomoa majengo ama madaraja, tofauti ni moja kwamba haya yanatengenzwa. Lakini yakipigwa kwenye matumbawe huharibu kabisa makazi ya samaki,” anasema.

 Mtaalamu huyu wa uvuvi, anazungumzia athari za uvuvi haramu kwamba baada ya mazalia ya samaki na viumbe hai kuteketezwa, huchukua miaka 70 hadi 100 kujijenga upya, hali ambayo hukaribisha ujwangwa baharini.

Anasema, mlipuko wa mabomu wakati wa uvuvi, huua viumbe hai vyote na mayai yake na kupoteza kizazi kikubwa cha samaki baharini, mmomonyoko wa fukwe unaosababisha kukosekana kwa vizuizi vya mawimbi, upotevu wa samaki wengi ambao mara nyingi ni vigumu kuwaondoa wote.

Makazi ya samaki
Samaki wanaotaga na dagaa hupendelea kujificha maeneo hayo kwa ajili ya kukwepa samaki wakubwa ambao huwafanya mlo.

Makazi haya mara nyingi huwa yamefunikwa kwa mawe madogo madogo na huwa na chakula cha kutosha na chenye virutubisho  kwa samaki.  Aidha, kuharibiwa kwa makazi ya samaki, huambatana na kupotea kwa mayai, samaki wadogo na makazi yao.

Hili huathiri kizazi cha samaki kwa kiasi kikubwa na kusababisha upungufu wa maliasili hii.  Uvuvi haramu ni ule unaofanyika bila kufuata Sheria na Kanuni za Uvuvi zinazosimamia raslimali za uvuvi kitaifa na kimataifa.

Uvuvi huu unajumuisha kuvua bila kuwa na leseni, kufanya shughuli za uvuvi katika maeneo yasiyoruhusiwa, kuvua kwa zana zisizokubalika kwa mfano kuvua kwa baruti na sumu,    Vilevile kuchakata mazao ambayo hayakuvuliwa kihalali na kufanya biashara ya mazao ya uvuvi ambayo yamevuliwa kwa kutozingatia taratibu zilizowekwa.

Pamoja na mabomu, zana nyingine ambazo hutumika kufanya uvuvi haramu ni nyavu zenye macho madogo, nyavu za timba, kokoro, sumu na baruti.
Share this article :

Post a Comment

KARIBU KATIKA WEBSITE YA KIJANJA, KUPATA HABARI MBALIMBALI ZA NDANI NA NJE YA NCHI. PIA UTAPATA MAMBO YA ACADEMIC. KARIBU SANA
 
Support : Creating Website | Johny Template | Mas Template
Copyright © 2011. GetInformedTz - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Mas Template
Proudly powered by Blogger