Home » » Ubaguzi wa rangi unavyoathiri michuano ya soka Ulaya 2012

Ubaguzi wa rangi unavyoathiri michuano ya soka Ulaya 2012

Written By Koka Albert on Monday, June 4, 2012 | 1:44 AM


MWEZI  huu  mashindano ya mpira wa mataifa ya Ulaya- Euro 2012- yatafanyika Poland na Ukraine.

Nchi hizi zilikuwa zamani sehemu ya kanda ya Ujamaa au Wasoshalisti chini ya Urusi. Kanda ilizaliwa baada ya vita kuu iliyokwisha mwaka 1945 baina ya Wazungu dhidi ya nduli Adolf Hitler wa Ujerumani.

Upande mmoja zilikuwa mataifa yaliyofuata siasa na uchumi wa kibepari zenye  muungano wa majeshi ya NATO. Mwaka jana muungano huu  ulichangia  kumpiga mabomu na kumuondoa (hatimaye kumuua ) Rais wa zamani wa Libya, marehemu Muammar Gaddafi. Ukanda uliotawaliwa na Warusi uliitwa WARSAW PACT –na hili jina linatokana na mji mkuu wa Poland yaani Warsaw, ambapo ni miongoni mwa miji itakayosimamia mashindano yatakayoanza Juni 8.

Ajabu kwamba ingawa nchi hizi za Ulaya Mashariki ambazo zilifuata siasa hii ya Ujamaa (na kibinadamu zaidi) ndiyo leo zinasemekana kuwa na ubaguzi mkubwa dhidi ya watu wanaotoka nchi masikini  (zisizo za Kizungu) Asia, Marekani ya Kusini na Afrika.

Mkondo wa siasa dhidi ya watu wasio Wazungu uling’ara baada ya kuvunjika kwa himaya mwaka 1989 hadi 1991. Kutokana na kuanguka huko paliibuka matatizo mengi ya uchumi, ukosefu wa kazi, elimu na nyumba. Vijana wengi wasiosoma ama kutokua na kazi ndiyo kiini kikubwa cha magenge katili yanayopiga hata kuua wageni.
Na je, nchi zipi?

Urusi yenyewe, Poland, Czechoslovakia, Ukraine, Belarus, Estonia, Serbia, Hungary, Romania, Montenegro Bosnia na Herzegovina (zilikuwa zamani sehemu ya Yugoslavia iliyoongozwa na kiongozi mashuhuri  Josip Tito aliyefariki 1980), Croatia, Albania, Kosovo, Macedonia.
Makundi mbalimbali yaliyoibuka jamii hizi dhidi ya wageni yamekuwa si tu yakitukuza fikra za weupe kuwa nchi zao bila wageni bali pia kujihamasisha  kwa kufanya mazoezi ya kupigana na mikutano ya siri inayotisha unaposikiliza katika mitandao kama You Tube na hata baadhi ya runinga za Majuu.

Kifikra siasa ya vikundi hivi inaongozwa na itikadi iitwayo “Neo-Nazism” – inayosifia, kutukuza ugali na damu ya Wanazi uliojengwa na kuimarishwa na hayati Adolf Hitler kichocheo cha vita vya 1939-1945.

Mwaka jana Anders Beivrik alipoua watoto na watu 77 nchini Norway alikuwa akitukuza itikadi hiyo. Tabia yake ya kunyoosha ngumi mbele anapoingia mahamakani ni moja ya kilelezo dhahiri cha jamaa hawa.
 Si nchi za Ulaya Mashariki tu zinazotukuza itikadi ya “Kineo-Nazi” bali pia  mataifa ya Ulaya Magharibi, Marekani, Brazil, Chile, Costa Rica na hata Israel yenyewe (kundi la Patrol 35 linaongozwa na vijana walishambulia wageni, watu weusi na mashoga mwaka 2008).

Makundi haya yote hufuata itikadi ya Adolf Hitler ya kutukuza Uzungu, utaifa na mashambulizi dhidi ya watu weusi, Wayahudi, vilema, wasenge na wageni ndani ya jumuiya.

Makundi ya Urusi yenye nguvu sana  yanafuata dhana inayotetea  “Urusi kwa ajili ya Warusi”- dhidi ya Wayahudi, Wazungu wa nchi  za Magharibi, Wahindi na Wachina, mashoga, Waislamu na Waroma (Wazungu wanaofanana na Wahindi ambao huwa na nywele nyeusi Waroma kiasilia ni raia masikini wanaorandaranda mitaa ya Ulaya wakiishi na familia zao majiani, wakifanya kazi za sulubu, wakiomba omba au kuiba na karne nyingi wamebaguliwa. Ingawa asili ya kabila hili ni Uhindini, huitwa “Wa-Gypsy” na huonekana pia Hispania, Ufaransa  na Marekani ya Kusini).

Baadhi ya vikundi pia vimeunda vyama dhahiri vyenye katiba na ofisi. Nchini Urusi kuna chama cha “Russian National Unity” (RNU) kilichoanzishwa na Alexander Barkashov aliyezaliwa1953. Huyu bwana alipomaliza shule mwaka 1971 alijiunga na jeshi kisha akafanya kazi kama fundi umeme na kujifunza Karate. Alianzisha pia klabu yake ya kupigana hiyo “karate” na mwaka 1991 akaunganisha baadhi ya wananchi wenzake waliokuwa na fikra za aina hiyo. Leo RNU inapigania maslahi ya fikra hizi kwa kutetea Ukristo, uzalendo, kuzuia ndoa kati ya Wazungu na wasio Wazungu, kupiga na kuondoa wageni wanaofanya kazi, nk.

Mkondo huu pia umezikumbuka nchi mbili zilizoteuliwa kuwa wenyeji wa mashindano ya mpira - Juni 8 hadi Julai mosi.

Tatizo la ubaguzi limefahamika baada ya wacheza mpira maarufu weusi hapa Uingereza kuanza kuongelea kwa uwazi adha iliyopo. Wanasoka maarufu wa Arsenal,  machotara  Theo Walcott na Alex Oxlade, Chamberlane walioko katika timu ya taifa ya Uingereza walitangaza kuwa ndugu zao hawatosafiri kuunga mkono msafara utakaokwenda Poland na Ukraine kutokana na woga wa magenge yaliyojitayarisha kushambulia watu weusi watakaohudhuria sherehe.

Habari hizo zilisikika kwa nguvu zaidi wakati mchezaji mashuhuri wa zamani wa taifa na Arsenal, Sol Campbell alipohojiwa na idhaa ya BBC, akawaasa washabiki wasio weupe “wakae nyumbani na kutazama mechi la sivyo watarudi  ndani ya jeneza.”

Kipindi maalumu kilichotolewa Jumatatu iliyopita na BBC ( “Panorama”) kilionyesha  magenge ya kibaguzi Ukraine na Poland yakiwasakama wachezaji weusi kwa sauti za milio ya nyani, wakishambulia wanafunzi toka Bara Asia wanaosoma mji wa Kharkiv- mmoja wa miji itakayokuwa na michuano Ukraine.Wakitetea eti hakuna ubaguzi baadhi ya wachezaji maarufu wa nchi hizi, walisema makundi ya kibaguzi ni madogo sana na si ukweli. Mshambuliaji wa zamani wa Chelsea, Andriy Schevshenko (mzawa wa Ukraine) alidai “hakuna la kuogopa.” Mchezaji mwingine aliyewahi kuichezea Arsenal Oleg Luzhny naye, alisema wapo wachezaji toka Nigeria na kwinginepo wanaosakata kabumbu “bila kubaguliwa.”

Licha ya maoni haya habari zimefufua suala la ubaguzi wa rangi na Sol Campbell alisema Ukraine na Poland “hazistahili kuwa wenyeji” wa kandanda iwapo hofu ya weusi imekita.

Habari hizi ni muhimu kwa vijana wengi Bongo wanaofikiria sana kwenda nchi za kigeni au wanaopelekwa kusoma Uzunguni. Ni muhimu kwao kuchunguza nchi gani wanakwenda na kuyajua mahusiano ya wenyeji na wageni.

Ukweli mataifa ambapo mambo ni afadhali na ubaguzi unapigwa vita ni yale yenye historia ya ukoloni kama Uingereza, Ufaransa na Uholanzi. Ukitathmini sana utagundua ni nchi hizi hizi zenye wachezaji wengi zaidi weusi  na hata vilabu vikubwa vya mpira.

Ingawa ubaguzi bado upo lakini si rahisi kukuta vikundi vikifanya mazoezi au kujifunza kuua wageni.Kijana yeyote wa Kibongo lazima awe macho na mtambuzi wa mambo kama haya.
Share this article :

Post a Comment

KARIBU KATIKA WEBSITE YA KIJANJA, KUPATA HABARI MBALIMBALI ZA NDANI NA NJE YA NCHI. PIA UTAPATA MAMBO YA ACADEMIC. KARIBU SANA
 
Support : Creating Website | Johny Template | Mas Template
Copyright © 2011. GetInformedTz - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Mas Template
Proudly powered by Blogger