Home » » Misamaha hii ya kodi isifumbiwe macho

Misamaha hii ya kodi isifumbiwe macho

Written By Koka Albert on Wednesday, June 13, 2012 | 1:57 AM

SIKU moja kabla ya Serikali kutangaza Bajeti yake ya mwaka wa fedha 2012/13, zimeibuka taarifa kwamba Tanzania inapoteza Dola za Marekani 1.7 bilioni (Sh1.7 trilioni) kila mwaka kutokana na misamaha ya kodi, ukwepaji kodi na utoroshaji wa fedha na rasilimali nyingine nje ya nchi.

Kiwango cha fedha kinachotajwa kupotea, kingeweza kusaidia Bajeti Kuu ya Serikali na kuondokana kabisa na utegemezi wa fedha za wahisani zenye masharti.

Utafiti wa Kamati ya Viongozi wa Dini ya masuala ya Uchumi na Haki za Binadamu (ISCJIC) umebainisha baadhi ya mambo yanayochangia upotevu huo kuwa ni sera mbovu za Serikali, uzembe katika kukusanya kodi na vitendo vya rushwa.

Mathalani, kati ya mambo ambayo ni ya ajabu, ni kwamba baadhi ya kampuni, zikiwamo za madini zinazofanya kazi hapa nchini hazitozwi kodi kulingana na uzalishaji, jambo linalofanya zaidi ya nusu ya kodi wanazolipa kuwa ni zile zinazotokana na mishahara ya wafanyakazi wao.

Hata hivyo, kilio hiki cha upotevu wa fedha kwa njia hii si jambo jipya na linaweza lisiwe la kushangaza masikioni mwa Watanzania kwa kuwa limekuwa likielezwa mara kwa mara na watu wa kada mbalimbali. Kinachoshangaza ni kuona Serikali imekaa kimya bila kutafuta suluhisho la tatizo hili.
Ukimya wa Serikali katika eneo hilo ambalo liko wazi kwa kupoteza fedha za walipa kodi, ndilo suala ambalo kila Mtanzania anatakiwa kujiuliza na kuwauliza viongozi wake. Hii ndiyo hatua ya kwanza ambayo tunapaswa kuchukua ili kuongeza mapato ya Serikali.

Itakumbukwa kuwa katika Bunge la Bajeti mwaka 2011/12, Kambi ya Upinzani Bungeni ilipaza sauti kuhusu jambo hili na kuitaka Serikali kuchukua hatua, lakini hatujaona lolote lililofanyika, badala yake kilio hicho kimeendelea kusikika tena mwaka huu.

Tayari wiki iliyopita, Waziri Kivuli wa Fedha, Zitto Kabwe alitaja vipaumbele katika bajeti yake mbadala, likiwamo suala la kupunguza upotevu wa fedha katika misamaha ya kodi kutoka asilimia tatu hadi asilimia moja.

Zitto alisema misamaha ya kodi inayotolewa kwa sasa ni mikubwa, sawa na misaada yote kutoka nchi wahisani ambayo ni Sh1.03 trilioni, kiwango ambacho kinawiana na utafiti wa viongozi hawa wa dini – kwamba tusipotoa misamaha hatutahitaji misaada kutoka nje.

Sisi hatuoni sababu ya Serikali kuendelea kuyapiga chenga maoni haya ya viongozi wa dini na kambi ya upinzani, hasa katika suala hili ambalo tunaamini ni muhimu kwa ustawi wa nchi yetu.

Tunaungana na wadau hawa kuona na kusisitiza haja ya kuwapo kwa mipango mizuri ya kukusanya kodi, kupanua wigo, kudhibiti kampuni za kihuni zinazokwepa kodi na kupunguza kwa kiwango kikubwa misamaha ya kodi kama si kuifuta kabisa.

Tutashangaa kama Serikali itaendelea kuikumbatia misamaha hiyo kama ambavyo imekuwa ikifanya siku zote hasa baada ya kuwepo kwa taarifa za kuaminika kuwa wengi wanaonufaika na misamaha hiyo wapo ndani ya Serikali na wengine wanaipigania kwa sababu za rushwa.

Katika orodha ya watu waliosamahewa kodi na Serikali katika mwaka wa fedha 2009/2010, yanaonekana majina ya baadhi ya mawaziri, wabunge na wakuu wa taasisi za Serikali kinyume cha taratibu.

Hata Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Ludovick Utouh katika ripoti yake alisema eneo hilo la misamaha ya kodi linapaswa kutazamwa ili kuepuka kuwa na makusanyo pungufu ya kodi.

Tunaungana na wadau wanaopigania suala hili kuishauri Serikali kutazama njia nyingine ya kuvutia wawekezaji badala ya kuwaumiza wananchi kwa kuweka misamaha ya kodi.
Share this article :

Post a Comment

KARIBU KATIKA WEBSITE YA KIJANJA, KUPATA HABARI MBALIMBALI ZA NDANI NA NJE YA NCHI. PIA UTAPATA MAMBO YA ACADEMIC. KARIBU SANA
 
Support : Creating Website | Johny Template | Mas Template
Copyright © 2011. GetInformedTz - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Mas Template
Proudly powered by Blogger