Home » » Vurugu zaibuka upya Zanzibar

Vurugu zaibuka upya Zanzibar

Written By Koka Albert on Monday, June 18, 2012 | 3:56 AM

MJI wa Zanzibar jana uligubikwa na vurugu mpya za kupinga Muungano na kuwalazimisha polisi kutumia mabomu ya machozi kuwatawanya wafuasi wa kikundi cha Uamsho waliokuwa wakiandamana.

Tukio hili lilitokea katika eneo la Mahonda Mkoa wa Kaskazini Ugunja, ambapo wafuasi hao walikuwa wakiandamana kuelekea katika mhadhara uliopangwa kufanyika katika eneo la Donge, nje kidogo ya Mji wa Unguja.

Awali, Jeshi la Polisi kupitia kwa Kamishna wake, Mussa Ali Mussa lilizuia  mhadhara huo, lakini viongozi wa kundi hilo walikaidi na kuwaamuru wafuasi wao kuandamana kuelekea katika eneo walikopanga kufanya mhadhara huo.

Masemaji wa Jeshi la Polisi Zanzibar, Mohammed Mahina aliithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kwamba watu kadhaa wamekamatwa kuhusiana na vurugu hizo.

Hata hivyo, alikataa kutoa maelezo zaidi kwa madia kuwa hajapata taarifa kamili kutoka katika eneo la tukio.

"Ni kweli tukio hilo limetokea na watu kadhaa tunawashikilia, lakini sina taarifa za ndani zaidi, sijawasiliana na Kamanda wa Polisi wa eneo hilo," alisema Mhina.

Vurugu hizo zilibuka mara baada ya kundi hilo kufika eneo la Mahonda karibu na Kituo cha Polisi, ambako askari polisi waliokuwepo eneo hilo waliwaamuru wafuasi hao kutawanyika, amri ambayo ilipingwa na kuwalazimisha polisi kutumia nguvu.

Polisi walilipua mabomu ya machozi ambayo yaliwafanya wafuasi hao wakiwemo wanawake na watoto kukimbia ovyo, baadhi yao wakikimbilia katika miskiti ya jirani, ambako walifuatwa na kutiwa mbaroni na wengine kujeruhiwa, kabla ya kukimbizwa hospitalini.

“Mabomu yamepigwa hadi ndani ya msikiti wa Mahonda walipokuwa wamekimbilia wafuasi hao,” alisema mkazi mmoja wa eneo hilo na kuongeza kuwa kuna watu walifuatwa hadi ndani ya msikiti na kupigwa kabla ya kukamatwa.

Vurugu hizo ambazo zilichukua zaidi ya saa moja, zilisababisha gari la Kiongozi wa kundi Maimam Zanzibar, Sheikh Farid Hadi Ahmed kuharibika baada ya kupata ajali wakati dereva wake alipokuwa anajaribu kuwakimbia polisi, lakini hata hivyo sheikh huyo hakuwamo ndani ya gari hilo.

Baada ya kutawanywa eneo la Mahonda wafuasi hao walirudi na kukusanyika eneo la Mjini katika Viwanja vya Msikiti wa Mbuyuni, kabla ya kujaribu kwenda tena katika mhadhara huo na kutawanywa tena na polisi.

Hata hivyo, baadaye Sheikh Farid alipozungumza na gazeti hili alisema maandamano hayo na mhadhara vilifuata utaratibu.

“Tulifuata taratibu zote za polisi, lakini cha ajabu kufika Mahonda tunatawanywa na kupigwa mabomu,” alisema na kuongeza kuwa kusudio lao la kutaka kuvunjwa kwa Muungano linabaki kama lilivyo na viongozi wote wa kundi hilo wapo salama.

Alisema polisi walichofanya sio sawa, kwani wamejeruhi watu na wengine kuwafuata msikitini na kuwapiga mabomu.

Imam Mselem alikiri kukutana na viongozi wa Jeshi la Polisi ambao waliwataka wasifanye maandamano na mhadhara huo.

Mwezi uliopita vurugu kubwa zilitokea mjini Zanzibar baada ya watu wasiofahamika kuchoma moto makanisa kadhaa, magari pamoja kupora mali mbalimbali kwa madai ya kupinga muugano.

Hoja ya Uamsho imewafanya pia wanasiasa mbalimbali kutoa kauli zao,  Rais wa Zaanzibar, Dk Ali Mohammed Shein hivi karibuni aliwata Wazanzibar wanaotaka kundolewa kwa kasoro katika Muugano wasubiri Tume ya Katiba.
Share this article :

Post a Comment

KARIBU KATIKA WEBSITE YA KIJANJA, KUPATA HABARI MBALIMBALI ZA NDANI NA NJE YA NCHI. PIA UTAPATA MAMBO YA ACADEMIC. KARIBU SANA
 
Support : Creating Website | Johny Template | Mas Template
Copyright © 2011. GetInformedTz - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Mas Template
Proudly powered by Blogger