Home » » Mgomo wa madaktari waanza rasmi

Mgomo wa madaktari waanza rasmi

Written By Koka Albert on Sunday, June 24, 2012 | 1:03 AM

Mgonjwa akihamishwa kutoka Wodi ya Kibasila katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), iliyopo Dar es Salaam jana, ili kupelekwa katika hospitali nyinyine kutokana na tihsio la kuwepo kwa mgomo wa madaktari, katika hospitali hiyo na nyingine za serikali sehemu mbali mbali nchini wanaodai stahiki zao mbali mbali, kwa madai ya serikali kushindwa kuzitekeleza. Picha na Emmanuel Herman
HUDUMA ZA KAWAIDA ZAZOROTA
Waandishi Wetu, Dar na Mikoani       
 MADAKTARI nchini wameanza mgomo katika baadhi ya hospitali nchini baada ya Serikali kushindwa kutekeleza madai yao waliyowasilisha katika Kamati ya Majadiliano iliyoundwa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.  Mgomo huo umetangazwa na Jumuiya ya Madaktari nchini huku ikifafanua kwamba kati ya madai kumi waliyotaka yatekelezwe na Serikali, hakuna hata moja lililofanyiwa kazi.  Hata hivyo,  jana madaktari hao ambao walikaa vikao vya majadiliano na Serikali kwa siku 90 baada ya kusitisha mgomo wao wa pili, wamesema katika madai yao kumi, hakuna hata moja lililotekelezwa na Serikali.  Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo, Dk Stephen Ulimboka jana aliwaeleza waandishi wa habari kwamba ili warejee kazini, Serikali inatakiwa kutekeleza madai yao yote na kusisitiza kwamba dai lao la kwanza ni kuitaka Serikali kuboresha huduma za msingi kwa wagonjwa.   
“Mgomo umeanza leo na hauna kikomo, lengo ni kuishinikiza Serikali kutekeleza madai yetu, hata zile huduma za dharura nazo kuanzia kesho (leo) zinaweza kusitishwa,” alisema Dk Ulimboka.  Wakati Ulimboka akieleza hayo, huduma katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) na Taasisi ya Mifupa (Moi) ilikuwa ikitolewa kwa kusuasua huku baadhi ya wafanyakazi wakisisitiza kuwa mgomo huo upo. 

Licha ya wafanyakazi hao kukiri kuwa siku za mwisho wa wiki idadi ya wagonjwa katika hospitali hizo huwa ndogo, lakini walisisitiza kuwapo kwa mgomo huo na kufafanua kuwa kwa mtu mgeni katika eneo hilo si rahisi kutambua hali hiyo.  Mwananchi Jumapili lilifika katika hospitali hiyo na kukuta huduma zikitolewa ‘kiaina’ huku baadhi ya wagonjwa wakieleza kwamba zimezorota, sio kama siku zilizopita.  

Tamko la Jumuiya      Akieleza kwa kina sababu za mgomo huo, Dk Ulimboka alisema katika madai waliyoyawasilisha, hakuna hata moja lililotekelezwa na kufafanua kwamba Serikali imeongeza dai ambalo wao hawakuliwasilisha.  Madai hayo ni pamoja na kupandishwa kwa ongezeko la mishahara, posho ya kuitwa kazini, posho za kufanya kazi katika mazingira magumu, bima ya afya, nyumba za kuishi, kukopeshwa magari kwa ajili ya usafiri, kuboreshwa kwa mazingira ya kufanyia kazi kwa kupeleka vifaa vya kazi, dawa na kuboresha miundombinu.  

“Serikali imesema imerekebisha viwango vinavyotumika kulipa posho ya uchunguzi wa maiti  kwa Sh 100,000 kwa uchunguzi wa madaktari na Sh50,000 kwa watumishi wengine, lakini hili halikuwa dai letu!” alisema Dk Ulimboka.   Naye Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Hussein Mwinyi aliwatahadharisha madaktari hao kuacha mgomo, akieleza kuwa ni batili na ni kinyume cha viapo vyao vya kazi.  Dk Mwinyi aliainisha mambo 10 ambayo madaktari walikuwa wamepanga kutekelezewa na kusema kuwa kwa sehemu, yametekelezwa na baadhi ya mambo yaliyobakia wanaweza kuyazungumza.

Mwanza
Madaktari zaidi ya 200 waliopo katika Hosptali ya Rufaa ya Bugando jana walianza mgomo rasmi baada ya Serikali kushindwa kutoa majibu ya kuridhisha kuhusu madai yao mbalimbali yaliyosababisha madaktari hao kugoma mapema mwaka huu.  Akizungumza na Mwananchi Jumapili, Mwakilishi wa Kamati ndogo ya kufuatilia madai madaktari hao, Dk Richard Kirita alisema kwamba madaktari wa kada zote katika hospitali hiyo wapo kwenye mgomo isipokuwa baadhi ya madaktari bingwa pamoja na wakuu wa idara.

 “Kwa kuwa leo sio siku ya kazi unaweza kudhani hakuna mgomo, lakini njoo Jumatatu (kesho) ndo utapata picha halisi ya mgomo kwa sababu wagonjwa watakuwa wengi, lakini hakutakuwa na huduma,”alisema 
Moshi

Hali ya utendaji wa madaktari mkoani Kilimanjaro imeonekana ya kusuasua huku baadhi ya madaktari katika Hospitali ya Rufaa ya KCMC wakisema hawaingii kazini na wengine wakisema bado wanasikilizia.

Katika Hospitali ya Mkoa ya Mawenzi, madaktari waliokuwa zamu walisema kwa leo huwezi kujua aliyeko kwenye mgomo na ambaye hayupo, kwani wengi hawako kazini leo hadi kesho.  

 Baadhi ya wagonjwa waliolazwa Hospitali ya KCMC katika wodi ya wanawake, walisema kuwa walitangaziwa kuwa kutakuwa na mgomo wa madaktari na kila mmoja aangalie cha kufanya na kuwa walifika wodini hapo asubuhi na hawakuzungumza na mgonjwa na kutoka.   Wagonjwa hao wamesema Ijumaa jioni wagonjwa wengi waliruhusiwa kuondoka hata kama hali zao hazijatengemaa ambapo walisema wanahofia afya zao kama madaktari watatekeleza msimamo wao.   Mbeya   Katika Hospitali ya Rufaa Mbeya madaktari 10  kati ya 80  ndiyo waliokubali jana kuendelea na  huduma ya kutibu wagonjwa ambapo wengine wameanza mgomo rasmi. 

Akizungumza na Mwananchi Jumapili kwa njia ya simu, Mkurugenzi wa Hospitali ya Rufaa Mbeya, Dk Eliuter Samky amethibitisha kuwapo na hali ya mgomo na kwamba ana uhakika wa madaktari 10 waliopo zamu kuendelea kazi.     

Awali Mwandishi wa gazeti hili alipofika  katika hospitali hiyo hakukuta daktari yeyote na ofisi za utawala zikiwa zimefungwa huku katika eneo la mapokezi likiwa na wagonjwa ambao wamekaa wakisubiria kupata huduma.  Katika kitengo cha wazazi Meta wanawake wanaokwenda kupata huduma  wamesema wameingiwa na hofu kubwa kwa kukosa huduma hiyo baada ya kuona matangazo yanayosema hakuna mgojwa atakayepatiwa matibabu.  

Wakizungumza hospitalini hapo wanawake hao ambao hawakutaka kuandikwa majina yao, walisema kuwa mbali na kuona tangazo hilo lakini pia waliambiwa na baadhi ya madaktari kuwa ni bora wakaenda sehemu nyingine kwa ajili ya matibabu kwa kile kilichoelezwa kuwa kuwa na wao wapo katika mgomo huo hivyo hakuta kuwa na huduma yeyote kwa mgonjwa.
Share this article :

Post a Comment

KARIBU KATIKA WEBSITE YA KIJANJA, KUPATA HABARI MBALIMBALI ZA NDANI NA NJE YA NCHI. PIA UTAPATA MAMBO YA ACADEMIC. KARIBU SANA
 
Support : Creating Website | Johny Template | Mas Template
Copyright © 2011. GetInformedTz - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Mas Template
Proudly powered by Blogger