Home » » Polisi atinga disko akiwa na SMG

Polisi atinga disko akiwa na SMG

Written By Koka Albert on Thursday, March 1, 2012 | 11:08 PM

POLISI mkoani Kilimanjaro wanamshikilia mmoja wa askari wake (jina tunalihifadhi kwa sasa) kwa tuhuma za kutoroka lindo, kisha kwenda klabu ya usiku mjini Moshi akiwa na bunduki aina ya Sub Machine Gun (SMG) usiku wa kuamkia jana.

Kitendo hicho kilisababisha mtafaruku katika klabu ya Pub Alberto baada ya meneja wa klabu hiyo kumkuta askari huyo akiingia ndani kupitia lango kubwa usiku wa manane, akiwa na silaha hiyo ya kivita.

Meneja wa ukumbi huo, Thadeus Kimaro alithibitisha tukio hilo na kusema alikutana na polisi huyo akiwa na bunduki hiyo aina ya SMG akitaka kuingia ukumbini humo kupitia lango kuu, kwa kuwa mlango wa kuingilia wateja tayari ulikuwa umefungwa.

“Wakati natokea Cool bar muda wa saa 9:00 usiku, nilikutana na mtu aliyetaka kuingia na bunduki huku akitweta na akisema kuna mtu amemuudhi ndani na alitaka kumuonyesha,”alisimulia  Kimaro.

Meneja huyo alisema wakati huo tayari muda wa kuingia wateja ulikuwa umepita na hivyo, mlango kufungwa na kuachwa lango kuu ili wateja waliobaki watoke.

Taarifa zaidi zilisema  askari huyo aliyekuwa katika lindo kwenye kituo kikuu cha mkoa, aliondoka lindoni akiwa na silaha hiyo iliyokuwa na risasi 30 ndani yake.

Inadaiwa kuwa awali polisi huyo alifika eneo la klabu hiyo akiwa kwenye gari binafsi na alikuwa ameongozana na wenzake watatu, lakini kabla ya kuingia ukumbini alibadili sare za kazi na kuziacha kwenye gari pamoja na silaha.

Muda kidogo baada ya kuingia ndani, alilikorofishana na mmoja wa watu waliokuwa ukumbini hapo, hivyo kuamua kwenda kwenye gari kuchukua silaha kwa malengo ambayo hayakufahamika mara moja, lakini alikutana na meneja huyo akiwa na walinzi ambao walimzuia asiingie ndani.

Meneja huyo alisema, akishirikiana na walinzi, walimsihi na kumwelewesha kuwa isingekuwa vyema kuingia na silaha kwa kuwa haziruhusiwi ndani ya ukumbi.  Aliridhika kwa shingo upande na kurudisha silaha kwenye gari.

"Kama angefanikiwa kuingia ndani ya ukumbi na silaha hiyo nahisi maafa yangekuwa ni makubwa, kwa kuwa kwa uelewa wangu SMG inabeba risasi 30," alisema Meneja huyo.

Kauli ya RPC
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Absalom Mwakyoma alisema askari huyo alikamatwa muda mfupi tu baada ya baada ya polisi kupewa taarifa hizo.

“Taarifa zilivyokuja kulikuwa na hisia kwamba inawezekana ni majambazi, kwa hiyo polisi walipofika pale na kuzingira lile gari ndipo tulipobaini kuwa ni askari, lakini wakati huo hakuwa katika sare zake, alikuwa amevaa kiraia,”alisema Mwakyoma.

Kamanda Mwakyoma alifafanua kwamba, baada ya polisi kupekua gari hilo walikuta sare za askari huyo na bunduki hiyo na kwamba alikuwa hajairudisha kwa vile bado alitakiwa kuwa lindoni.

“Tunaye hapa lock up (mahabusu) maana tulimkamata hiyo saa 9:00 usiku na mchakato wa kumfungulia mashitaka ya kijeshi unaendelea kwa sababu wakati huo, bado alipaswa awe lindo kituo cha kati, lakini akatoroka kwenda kucheza disko,”alisema Mwakyoma.

Mwaka 2007, wakili mmoja wa kujitegemea wa jijini Arusha aliwahi kuingia na bastola katika ukumbi huo na kufyatua risasi hali iliyoulazimu uongozi wa klabu hiyo kuweka mashine ya kukagua silaha kabla ya wateja kuingia ukumbini
Share this article :

Post a Comment

KARIBU KATIKA WEBSITE YA KIJANJA, KUPATA HABARI MBALIMBALI ZA NDANI NA NJE YA NCHI. PIA UTAPATA MAMBO YA ACADEMIC. KARIBU SANA
 
Support : Creating Website | Johny Template | Mas Template
Copyright © 2011. GetInformedTz - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Mas Template
Proudly powered by Blogger