Home » » Chuo Kikuu chatunuku shahada bandia watu maarufu

Chuo Kikuu chatunuku shahada bandia watu maarufu

Written By Koka Albert on Thursday, March 15, 2012 | 4:19 AM

Dotto Kahindi na Boniface Meena
TUME ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU), imekana kukitambua Chuo Kikuu cha Japan Bible Institute Graduate School of Theology kilichotoa Shahada ya heshima kwa mfanyabiashara maarufu nchini, kutokana na kutotambulika kisheria nchini.
Kwa mujibu wa taarifa ya TCU kwa umma iliyotolewa jana kwenye gazeti la moja la kila siku (siyo Mwananchi), chuo hicho kimekuwa kikitangaza kutoa kozi mbalimbali za uzamivu (PhD) kwenye nyanja za dini na jamii.
Taarifa ya TCU imekuja siku chache baada ya chuo hicho kuwatunuku Shahada ya heshima ya udaktari watu mbalimbali  akiwamo, Mwenyekiti Mtendaji wa Makampuni ya IPP.
Katika wasifu uliotolewa na chuo hicho kwa mwenyekiti huyo, ni kwamba hatua hiyo imefikiwa baada ya juhudi zake za kusaidia makundi mbalimbali ya watu wakiwamo walemavu, wajane na watu walioathirika na Ukimwi. Pia, kutambua mchango wake katika kutumikia kanisa.
Kwa mujibu wa taarifa ya TCU, chuo hicho kinatangaza kuwakilisha tawi la taasisi iliyopo nchini Marekani na kwamba, makao yake makuu kwa bara la Afrika yapo Dar es Salaam, huku eneo la ofisi likiwa halijulikani kilipo.
“Tume inachukua fursa hii kuuarifu umma kwamba chuo hiki hakitambuliki kwa mujibu wa sheria na kwamba wamiliki wa Japan Bible Institute Graduate School of Theology hawana kibali cha kutoa elimu ya chuo kikuu ambayo inatambuliwa hapa nchini,” inaeleza sehemu ya taarifa hiyo.
Tume hiyo ilitoa tahadhari kwa umma kuepuka ulaghai ambao unafanywa na watu eneo la elimu ya juu kwa kuwa vyeti vitakavyotolewa na chuo hicho havitatambulika na tume na haviwezi kutumika nchini.
 Tume ilitoa onyo kali kwa wamiliki wa chuo hicho , ikiwataka kuacha mara moja kutoa matangazo ya shahada za aina hiyo nchini, bila kufuata taratibu na kwamba hatua za kisheria zitachukuliwa kwa atakayekwenda kinyume cha sheria.
Hata hivyo, wakati wa sherehe za kutunukiwa kwa mwenyekiti huyo zilizofanyika viwanja vya Mnazi Mmoja mwishoni mwa wiki iliyopita, Mkurugenzi wa Taasisi hiyo Kanda ya Afrika, Askofu Dk Paul Shemshanga, alisema chuo chake kinatambuliwa na taasisi mbalimbali ulimwenguni na kuishukuru Serikali ya Tanzania kwa kuwapa ruhusu ya kutoa elimu hiyo nchini.
Msemaji wa Mwenyekiti Mtendaji wa IPP, Abdulhamid Njovu, alipoulizwa kuhusu suala hilo alisema anachokifahamu ni kuwa hakiingii kwenye mfumo wa TCU, kwa sababu kinahusiana na dini chenye misingi ya kikristo.
Njovu alisema TCU walitoa barua yenye kumbukumbu namba TCU/A60/25/ ya Machi 9, mwaka huu kuruhusu kufanyika kwa sherehe hizo za utoaji shahada za uzamivu (PhD).
”Huwa wanatoa shahada za heshima kwa watu wenye matendo ya kichungaji kwa kuwa, chuo chao ni cha masuala ya dini na wote waliokuwapo pale ni viongozi wa dini isipokuwa wale watunukiwa,” alisema Njovu na kuongeza: “Masuala hayo yote ni ya viongozi wa kidini.”
Share this article :

Post a Comment

KARIBU KATIKA WEBSITE YA KIJANJA, KUPATA HABARI MBALIMBALI ZA NDANI NA NJE YA NCHI. PIA UTAPATA MAMBO YA ACADEMIC. KARIBU SANA
 
Support : Creating Website | Johny Template | Mas Template
Copyright © 2011. GetInformedTz - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Mas Template
Proudly powered by Blogger