Home » » Watuhumiwa wa mauaji watoroka mahabusu

Watuhumiwa wa mauaji watoroka mahabusu

Written By Koka Albert on Friday, March 23, 2012 | 2:37 AM

Godfrey Kahango, Mbeya.
WATUHUMIWA wanne, wakiwamo watatu wa mauaji, wametoroka katika chumba cha mahabusu katika Kituo Kikuu cha Polisi mkoani Mbeya walikohifadhiwa kabla ya kufikishwa mahakamani. Kwa mujibu ya taarifa kutoka ndani ya Jeshi la Polisi mkoani hapa, watuhumiwa hao walitoroka baada ya kuvunja ukuta wa chumba cha mahabusu na kukimbilia kusikojulikana.

Mmoja kati ya mahabusu hao, anatuhumiwa kwa wizi. Tukio hilo lilitokea juzi kati ya saa 8 hadi saa 9 usiku katika kituo hicho cha polisi na Kamanda wa Polisi Mkoani wa Mbeya, Advocate Nyombi amethibitisha kuwapo kwa tukio hilo.
Kwa mujibu wa taarifa hizo, mahabusu hao waliamua kuchimba ukuta wa mahabusu ya kituo hicho na kutoroka huku askari polisi waliokuwa zamu wakiwa hawajui kilichokuwa kikiendelea.

Taarifa zaidi kutoka jeshi hilo mkoani hapa zilisema kwamba, baada ya mahabusu hao kufanikiwa kuchimba ukuta huo, wanne kati yao walifanikiwa kutoroka na wengine walikamatwa na polisi waliokuwa kwenye lindo baada ya kugundua tukio hilo.

Taarifa hizo zimeeleza kuwa askari watano waliokuwa zamu siku hiyo watupwa rumande kuhusiana na tukio hilo. Akizungumzia tukio hilo ofisini kwake, Kamanda Nyombi alisema askari waliokuwa zamu katika chumba cha mashtaka katika kituo hicho wakiwa katika ukaguzi wao wa kawaida wa kila baada ya saa moja waligundua kutoroka kwa watuhumiwa hao.
Kamanda Nyombi alisema watuhumiwa hao walichimba na kumwagilia maji ukuta wa chumba hicho kisha kuutoboa kwa kutumia vipande vya nondo.

Nyombi alisema askari hao waliokuwa zamu walipopita katika eneo hilo walikuta sehemu ya huo ikiwa na maji yanayotiririka kwa wingi huku kukiwa na tundu kubwa lenye upana wa futi mbili wa nchi 18.

Alidai kuwa katika eneo hilo kulikutwa na vipande viwili vya nondo ambavyo alidai kuwa huenda ndivyo vilivyotumiwa na watuhumiwa hao.

Kamanda Nyombi alisema baada ya kutolewa taarifa ya mahabusu hao kutoroka, msako mkali ulianza na walifanikiwa kumkamata mtuhumiwa mmoja ambaye ni mkazi wa eneo la Ilomba, jijini mbeya.
Alifahamisha kuwa mtuhumiwa mmoja ambaye alikuwa anatuhumiwa kwa kosa la kuiba betri tatu za gari alikamatwa na watuhumiwa wengine watatu wa mauaji hawajakamatwa na kudai kuwa ndani ya saa 24 watakuwa wametiwa mbaroni.
Share this article :

Post a Comment

KARIBU KATIKA WEBSITE YA KIJANJA, KUPATA HABARI MBALIMBALI ZA NDANI NA NJE YA NCHI. PIA UTAPATA MAMBO YA ACADEMIC. KARIBU SANA
 
Support : Creating Website | Johny Template | Mas Template
Copyright © 2011. GetInformedTz - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Mas Template
Proudly powered by Blogger