Home » » Wadau wapinga mfumo usahihishaji darasa la saba

Wadau wapinga mfumo usahihishaji darasa la saba

Written By Koka Albert on Saturday, March 31, 2012 | 11:15 PM

Ibrahim Yamola
WADAU wa elimu wamepinga mfumo mpya wa usahihishaji wa mitihani ya darasa la saba utakaoanza kutumika mwaka huu ambao unaojulikana kwa jina la Optical Mark Reader (OMR), wakisema hautawajenga wanafunzi kiuwezo, bali kuwalemaza.

Wakizungumza kwenye semina ya kujadili maendeleo ya elimu nchini iliyofanyika Dar es Salaam jana, wadau hao walisema utaratibu huo ambao Baraza la Mitihani la Taifa (Necta), walisema utaharakisha usahihishaji lakini utawalemaza wanafunzi kwa kuwa majibu yote yatakuwa ni ya kuchagua.

“Kipindi Necta wanabuni mpango huu hawakuwashirikisha wadau kama sisi ambao tungeweza kutoa maoni yetu juu ya kipi kifanyike. Tutegemee wanafunzi wengi wa kwanza kufeli,” alisema Mhadhiri wa Idara ya Lugha ya Isimu na Lugha za kigeni, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Michael Kadeghe na kuongeza:

“Hakukuwa na haja kwa Necta kubuni mfumo huu huku kukiwa na mfumo mpya wa ufundishaji wa kuwajenga wanafunzi kujieleza na kushirikishana wakati katika mitihani unamwambia unamletea wa kuchagua majibu A, B, C na D. Kweli tunajenga jamii ambayo haitaweza kujieleza mbele za watu!”

Dk Kadeghe alisema sababu zilizotolewa na Necta kwamba hatua hiyo itapunguza itapunguza muda na kuongeza ufanisi katika usahihishaji pamoja na kupungua kwa gharama za usahihishaji si za kweli kutokana akisema na kila halmashauri nchini inaweza kugharamia kusahihisha mitihani yao.

“Necta wanapenda kujibebesha mizigo ambayo si ya lazima. Kwa nini wasianzishe mfumo wa kusahihisha mitihani kwa kila kanda? Kwa mfano, kila kanda kusahihisha mitihani yao wenyewe kwa gharama zao na wao wasimamie tu?” alisema Dk Kadeghe.

Kwa upande wake, Mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Mzumbe, Dk Geoge Shumbusho alisema kutumika kwa mfumo huo mwaka huu hakutakuwa na matunda yoyote kutokana na wanafunzi kutopata muda wa kutosha kujiandaa na kuzoea kuutumia.

“Masharti ya karatasi  ya kujibia mtihani watatakiwa kutumia  penseli maalumu zijulikanazo  kwa jina la HB na hazitakiwi kukunjika wala kuchafua. Mtahiniwa asipofuata utaratibu, wakati wa usahihishaji kompyuta haitatambua mtihani wake,” alisema Dk Shumbusho.

Alisema mfumo huu utaendelea kurudisha nyuma kiwango cha elimu kwa baadhi ya wanafunzi watakaohitimu kutokuwa na uwezo wowote wa kujieleza kwani kitendo cha kujibu maswali kwa kuchagua hakina chachu ya kumfanya mwanafunzi kufikiria zaidi.

Mdau mwingine kutoka Mamlaka ya Elimu Tanzania (Tea), Juma Mkude alisema mfumo huo kwa mwaka huu utasumbua wanafunzi wengi na kushauri kuwa kabla ya kutumika, wanafunzi wangetakiwa kutumia karatasi hizo wakiwa angalau darasa la sita.

Alisema kufanya hivyo mapema kutawafanya wazizoee kabla ya kujibu mtihani wa darasa la saba… “Kwanza tunatakiwa kujua huu mfumo kwa vijijini utawafikia mapema na kuufanyia mazoezi ya kutosha? Tusije kujikuta tunazalisha watoto wengi watakaokuwa wa mitaani kwa kutofaulu na kushindwa waende wapi!”

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Selestine Gesimba aliutetea mfumo huu akisema ni mzuri na hauna tatizo na wanafunzi wanatakiwa kujiandaa kwa kufanya mazoezi ya kutosha.

“Wizara inawataka wadau wote kutambua kuwa mfumo huu ni bora na wanafunzi wanatakiwa kutambua wakati huu ni wakati wa kufanya mazoezi ya kutosha,” alisema Gesimba.
Share this article :

Post a Comment

KARIBU KATIKA WEBSITE YA KIJANJA, KUPATA HABARI MBALIMBALI ZA NDANI NA NJE YA NCHI. PIA UTAPATA MAMBO YA ACADEMIC. KARIBU SANA
 
Support : Creating Website | Johny Template | Mas Template
Copyright © 2011. GetInformedTz - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Mas Template
Proudly powered by Blogger