Home » » Profesa Lipumba: Hatujuti kuwafukuza kina Hamad

Profesa Lipumba: Hatujuti kuwafukuza kina Hamad

Written By Koka Albert on Tuesday, March 13, 2012 | 12:15 AM

Raymond Kaminyoge na Shakila Nyerere
MWENYEKITI wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba amesema chama hicho hakijutii kumfukuza kwenye chama hicho Mbunge wa Wawi, Hamad Rashid Mohammed na washirika wake kwa kuwa ni waasi na uamuzi huo umefanywa kulinda nidhamu ndani ya chama.

Uamuzi wa kuwavua uanachama Hamad Rashid na wajumbe wenzake watatu wa Baraza Kuu la CUF, Doyo Hamis Doyo, Juma Saanani na Shoka Khamis Juma, umekuwa ukitajwa kama sababu ya kuanza kuanguka kwa himaya ya kisiasa ya chama hicho kwa upande wa bara.

Lakini, jana, Profesa Lipumba akizungumzia mwelekeo wa chama hicho alipokutana na waandishi wa habari Dar es Salaam, alisema CUF ni chama imara hivyo lazima kifanye uamuzi kwa kufuata vikao na katiba yake.
“Uamuzi wa kuwafukuza uanachama hatuujutii, ulifanywa kwa umakini kwa kufuata taratibu za kufanya uamuzi kwa njia ya vikao na katiba. Nikiwa Marekani nilikuwa nawasiliana na viongozi wenzangu na uamuzi waliofikia ulikuwa na lengo la kukiimarisha chama,” alisema Profesa Lipumba.

Kuhusu wanachama kukihama chama hicho baada ya kuwafukuza kina Hamad, Profesa Lipumba alisema: “Watu wanaweza kuchapisha kadi nyingi na kusema ni za wanachama waliohama kumbe si kweli. Hatuwezi kuchapisha kadi kama zilivyo noti kwa kuwahofia wahalifu wanaozichapisha, jambo la msingi ni kuwafahamu wanachama wetu.”

“Kuna utata katika takwimu za watu wanaokihama chama, maeneo mengine idadi ya wanachama wanaohama inaelezwa kuwa ni kubwa kuliko idadi wanachama tuliowahi kuwa nao. Hizi ni mbinu zinazotumiwa kuonyesha kwamba chama kinaelekea kufa lakini, ukweli ni kwamba kipo imara na kitaendelea kuwepo.” Jana Hamad Rashid hakupatikana kutwa nzima kujibu tuhuma hizo. Lakini aliwahi kukaririwa akieleza kuwa uamuzi kumfukuza uanachama ulifanyika kwa mizengwe na chuki.

Alithibitisha madai yake hayo kwa kufungua kesi Mahakama Kuu kupinga uamuzi huo na kuiomba Mahakama imtake Katibu wa chama hicho, Maalim Seif Shariff Hamad na Baraza la Wadhamini la chama hicho kueleza kwa nini wasichukuliwe hatua kwa kukiuka amri iliyozuia mkutano wa kumfukuza.

Barua pepe
Akijibu tuhuma za Hamad Rashid kwamba aliwahi kunasa waraka wa barua pepe unaoonyesha mawasiliano kati yake na Maalim Seif, Profesa Lipumba alisema kitendo cha kuanika hadharani mawasiliano binafsi ni kosa la jinai... “Hili ni kosa la jinai mtu anatamba hadharani akionyesha mawasiliano ya barua pepe za watu kinyume na taratibu!”

Mwishoni mwa mwaka jana, Hamad Rashid wakati akiwa katika mvutano na uongozi wa juu wa chama chake, alitoa nakala kwa waandishi ukionyesha kile alichodai kuwa ni waraka wa mawasiliano ya barua pepe kati ya Profesa Lipumba na Maalim Seif ukitaja mbinu za kumng’oa katika CUF.
Share this article :

Post a Comment

KARIBU KATIKA WEBSITE YA KIJANJA, KUPATA HABARI MBALIMBALI ZA NDANI NA NJE YA NCHI. PIA UTAPATA MAMBO YA ACADEMIC. KARIBU SANA
 
Support : Creating Website | Johny Template | Mas Template
Copyright © 2011. GetInformedTz - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Mas Template
Proudly powered by Blogger