Home » » Tumuunge mkono Waziri Magufuli

Tumuunge mkono Waziri Magufuli

Written By Koka Albert on Thursday, March 15, 2012 | 2:36 AM

Agizo la Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli, kuwaondoa wafanyabiashara waliojenga katika hifadhi za barabara jijini Dar es Salaam limeanza kutekelezwa.

Operesheni hiyo inayotekelezwa na Wakala Barabara Tanzania ,(Tanroads) Mkoa wa Dar es Salaam, ilianza wiki hii katika barabara ya Morogoro.

Katika kutekeleza agizo hilo, wafanyabishara hao walionekana kuwa katika hekaheka za kuhamisha vitu vyao ili kuepuka operesheni hiyo ya safisha jiji, huku wengine wakiangua vilio kutokana na mali zao kuharibiwa.

Maofisa wa Tanroads wamekaririwa wakieleza kuwa hatua hiyo ya kuanza kubomoa nyumba za wafanyabiashara na watu waliojenga katika hifadhi za barabara, inatokana na kukaidi agizo la wakala huo, kuwataka wananchi hao kuhama kwa hiari kabla ya kubomolewa.

Zoezi hilo ni awamu ya kwanza ya utekelezaji wa agizo la Dk Magufuli ambapo linalenga kuwaondoa wafanyabiashara hao kuanzia Ubungo hadi Kiluvya.

Tayari waathirika wa bomoabomoa hiyo wamekaririwa wakisema kuwa pamoja na zoezi hilo kufanyika, hawako tayari kuondoka badala yake watarudi katika maeneo hayo baada tu ya operesheni hiyo kumaliziaka.
Baadhi ya wafanyabiashara hao wanasema kuwa wamepata hasara kubwa baada ya nyumba zao za biashara kuvunjwa huku  bado wakiwa na madeni makubwa waliyokopa benki.

Tunachukua nafasi hii kumpongeza Waziri Magufuli kwa hatua ambayo ameichukua kupitia Tanroads ya kusafisha maeneo ya hifadhi ya barabara za Jiji la Dar es Salaam.

Tunampongeza Waziri Magufuli kwa sababu tunajua kuwa amechukua hatua hiyo ili kutekeleza sheria za barabara zinazozuia watu kufanyabiashara kwenye maeneo hayo au kujenga nyumba za kuishi.
Tumeshuhudia katika sekta nyingi nchini Serikali imeshindwa kusimamia sheria zake na matokeo yake kila mtu anafanya analotaka, hali ambayo haikubaliki hata kidogo.

Ni kutokana na kukosekana usimamizi makini katika shughuli mbalimbali za kiserikali leo tunashuhudia baadhi ya watu wanajenga nyumba katika maeneo ya wazi, kandakando ya bahari na pengine kuziba barabara huku mamlaka zinazihusika zikiwaacha kama hazioni.

Leo tunaambiwa kuna mamia ya watu waliojenga juu ya bomba la maji la kutoka Ruvu Juu kuingia jijini Dar es Salaam, hali ambayo ni hatari kwa usalama wa maisha yao.

Tunajiuliza mamlaka zinazohusika zilikuwa wapi mpaka watu hawa wakajenga barabarani nyumba hizo? Kwa nini wasibomolewe wakati wanajenga?

Tunadhani anachofanya sasa Waziri Magufuli kinatakiwa kuigwa na watendaji wengine serikalini ili miji yetu iwe na mipangilio mizuri
Share this article :

Post a Comment

KARIBU KATIKA WEBSITE YA KIJANJA, KUPATA HABARI MBALIMBALI ZA NDANI NA NJE YA NCHI. PIA UTAPATA MAMBO YA ACADEMIC. KARIBU SANA
 
Support : Creating Website | Johny Template | Mas Template
Copyright © 2011. GetInformedTz - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Mas Template
Proudly powered by Blogger