Home » » Watatu Yanga kufungiwa miezi mitatu

Watatu Yanga kufungiwa miezi mitatu

Written By Koka Albert on Tuesday, March 13, 2012 | 12:29 AM

Waandishi Wetu
WACHEZAJI zaidi ya watatu wa Yanga, huenda wakafungiwa miezi mitatu kucheza soka kutoka na kitendo chao cha kumpiga mwamuzi, Israel Mujuni katika mechi yao dhidi ya Azam iliyopigwa  mwishoni mwa wiki kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Katika mchezo huo uliomalizika kwa Yanga kulala mabao 3-1, uliingia mushkeli dakika ya 13 baada ya Haruna Niyonzima kupewa kadi nyekundu kwa kile kilichoelezwa kuzozana na mwamuzi na kumtolea lugha chafu.

Wachezaji ambao rungu la Shirikisho la Soka Tanzania, TFF, ni dhahiri litawaangukia ni Nadir Haroub 'Cannavaro', Stephano Mwasika na Nurdin Bakari wakati Jerry Tegete huenda naye akaangukiwa na hilo baada ya kutaka kuingia ndani ya uwanja kwa nia ya kumdhuru mwamuzi. Hata hivyo alizuiwa na wachezaji wenzake wa akiba.

Haruna Niyonzima atakosa mechi tatu kama kanuni zinavyosema. Hata hivyo, Kamati ya Ligi ya TFF itakayokutana wiki hii, itaamua vinginevyo.

Nahodha wa Yanga, Shadrack Nsajigwa, Athumani Idd 'Chuji', Omega Seme na Hamisi Kiiza walifanya kazi ya ziada kuwazuia wachezaji hao pamoja na daktari wa timu, Juma Sufiani.

Wachezaji hao wanabanwa na Kanuni ya 25 ya udhibiti wa wachezaji kipengele (F) kifungu cha (iii) kinachosema, mchezaji yeyote atakayemshambulia mwamuzi au kiongozi yeyote kwa namna yoyote ile, iwe kwa matusi au kwa kumgusa, ataadhibiwa kwa kufungiwa kwa kipindi kisichopungua miezi mitatu hadi 12, kufungiwa kucheza michezo kadhaa, kupigwa faini kwa mujibu wa Kanuni ya 31 au vyote kwa pamoja.

TFF kupitia msemaji wake, Boniface Wambura alisema Kamati ya Ligi inakutana katikati ya wiki hii baada ya kupokea taarifa ya kamisaa wa mchezo huo.

Wambura alisema jana kuwa tayari wamepokea taarifa hiyo kutoka kwa kamisaa wa mchezo na tayari wameiwasilisha kwa Kamati ya Ligi.

"Tayari ripoti imefika kwetu na tulichokifanya sisi ni kuipeleka kwa wahusika wa mwisho ambao ni Kamati ya Ligi chini ya Wallace Karia pamoja Godfrey Nyange na wenzake ambapo wataipitia kwa makini kabla ya kuitolea maamuzi.

"Naamini yote yatakayofanyika yataenda sambamba na adhabu kwa watu waliohusika na vurugu zile ndani na hata nje ya uwanja," alisema Wambura.

Mbali na vurugu hizo, kulikuwepo na uharibifu wa mali za uwanja na baadhi ya mashabiki wa Yanga walikuwa wakirusha viti uwanjani ikiwa ni siku chache baada ya Serikali kuagiza Simba kulipa Shilingi5 milioni kwa kuvunja viti wakati wa pambano lao dhidi ya Kiyovu.

Ukiacha baadhi ya wachezaji hao kuadhibiwa, klabu ya Yanga italazimika kulipa gharama za uharibifu huo uliofanywa na mashabiki wake kwa kung'oa viti na miundombinu mingine.

Katika hatua nyingine, kiungo wa Yanga, Haruna Niyonzima amewaomba radhi mashabiki na wapenzi wa soka nchini kwa kitendo kilichotokea mwishoni mwa wiki walipocheza na timu ya Azam na kusababisha vurugu huku akidai hakumjibu lolote mwamuzi Israel Nkongo

"Nawaomba msamaha mashabiki na wadau wote wa soka hapa nchini kutokana na vitendo vya vurugu vilivyotokea kwenye mchezo ule na nawaahidi hakiwezi kutokea tena" alisema Niyonzima.

Aliongeza kusema kuwa mashabiki wasikate tamaa kwani wamekosa mchezo ule lakini bado wana michezo mingine na kikosi kipo vizuri hivyo watafanya vizuri kwenye mchezo ujao na kuhakikisha wanatete ubingwa wao
Share this article :

Post a Comment

KARIBU KATIKA WEBSITE YA KIJANJA, KUPATA HABARI MBALIMBALI ZA NDANI NA NJE YA NCHI. PIA UTAPATA MAMBO YA ACADEMIC. KARIBU SANA
 
Support : Creating Website | Johny Template | Mas Template
Copyright © 2011. GetInformedTz - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Mas Template
Proudly powered by Blogger