Home » » Serikali yatangaza waliochaguliwa kidato cha tano

Serikali yatangaza waliochaguliwa kidato cha tano

Written By Koka Albert on Wednesday, March 28, 2012 | 4:39 AM

Fredy Azzah
WIZARA ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, imetangaza majina ya wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na kidato cha tano mwaka huu, huku idadi yao ikishuka kwa asilimia 13.34 ikilinganishwa na mwaka jana.

Akitangaza majina hayo Dar es Salaam jana, Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Philipo Mulugo alisema kutokana na hatua hiyo, shule nyingi hasa zinazochukua wanafunzi wa mikondo ya sanaa na uchumi, zimekosa idadi ya wanafunzi kama ilivyotakiwa.

“Serikali ilikuwa imetenga nafasi 15,000 za wasichana, lakini waliopatikana ni 9,378 tu, nafasi zilizokuwa zimetengwa kwa wavulana ni 26,000, lakini waliopatikana ni 22,138,” alisema.

Alisema wanafunzi 142 waliobakia, ufaulu wao haukuweza kutengeneza maunganisho yoyote ya masomo, kwa hiyo hawakupangwa kuendelea na masomo ya kidato cha tano.

Mwaka 2010, wanafunzi 352,840 walifanya mtihani wa kidato cha nne, huku 40,388, sawa na asilimia 11.5 wakipata daraja la kwanza mpaka la tatu. Waliochaguliwa kuendelea na kidato cha tano na vyuo vya ufundi walikuwa 36,366.

Mulugo alisema mwaka 2011 wanafunzi waliofanya mtihani huo walikuwa 336,301, huku 33,577 sawa na asilimia 9.98 wakipata daraja la kwanza mpaka la tatu.

“Ufaulu huu umepunguza idadi ya waliochaguliwa kidato cha tano na vyuo vya ufundi kutoka wanafunzi 36,366 mwaka 2011 mpaka wanafunzi 31,516 mwaka 2012. Huu ni upungufu wa wanafunzi 4,850 sawa na asilimia 13.34,” alisema Mulugo.

Sayansi wajitutumua

Waziri Mulugo alisema idadi ya wanafunzi waliopangiwa kusoma masomo ya sayansi imeongezeka hadi kufikia asilimia 53.34 ya wanafunzi wote waliopangiwa kidato cha tano mwaka huu.

“Jumla ya wanafunzi waliopangiwa masomo ya sayansi ni 16,493 ambao ni asilimia 53.34 ya wanafunzi wote waliopangiwa kidato cha tano mwaka 2012. Idadi hii ni kubwa kuliko ya waliopangiwa kusoma masomo mengine,” alisema.

Sifa za kuchaguliwa
Pamoja na mambo mengine, Mulugo alisema sifa zilizozingatiwa katika kuwachagua wanafunzi hao ni pamoja na wote kutakiwa kuwa na umri wa chini ya miaka 25 na wawe wamefaulu kwa madaraja A, B, C, na D katika masomo yasiyopungua matano.

Alitaja sifa nyingine kuwa ni kila mwanafunzi kuwa na daraja la A, B, au C katika masomo matatu (credit) anayokwenda kuyasomea kidato cha tano.

Wanafunzi hao waliochaguliwa wamepangiwa kusoma kwenye shule 201, zikiwamo 61 za wasichana, 106 za wanafunzi wa kiume na 34 za mchanganyiko.

Kati ya hizo, shule 17 ni za masomo ya sayansi pekee, 64 ni za sanaa na uchumi, huku 120 zikiwa ni mchanganyiko wa mikondo ya sayansi na sanaa
Share this article :

Post a Comment

KARIBU KATIKA WEBSITE YA KIJANJA, KUPATA HABARI MBALIMBALI ZA NDANI NA NJE YA NCHI. PIA UTAPATA MAMBO YA ACADEMIC. KARIBU SANA
 
Support : Creating Website | Johny Template | Mas Template
Copyright © 2011. GetInformedTz - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Mas Template
Proudly powered by Blogger