Home » » Vurugu, utekaji vyazitikisa kampeni Arumeru Mashariki

Vurugu, utekaji vyazitikisa kampeni Arumeru Mashariki

Written By Koka Albert on Tuesday, March 20, 2012 | 12:18 AM


MATUKIO ya uhalifu yanayohusishwa na kampeni za uchaguzi mdogo katika jimbo la Arumeru Mashariki, mkoani Arusha yameanza kujitokeza huku polisi wakivionya vya vya siasa vinavyoshiriki kutojihusisha na vurugu kwa kuwa sheria zitachukua mkondo wake.
 
Wakati polisi wakitoa kauli hiyo, Chama Cha Mapinduzi (CCM) nacho kimetoa kauli kali kikitishia kuwaagiza vijana wake kuingia msituni ikiwa vitendo vya vurugu kinavyofanyiwa vitaendelea huku umoja wake wa vijana (UVCCM) nao ukilaani vurugu za wafuasi wa Chadema.
  
Juzi usiku gari la waandishi wa habari lililokuwa kwenye msafara wa mgombea wa chama hicho, Sioi Sumari ulishambuliwa na kundi la watu wanaodhaniwa kuwa wafuasi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) katika eneo la Maji ya Chai wakati ukirejea kutoka kwenye mkutano wa kampeni, uliofanyika kata ya Ngarenanyuki.Kwa upande wake, Chadema nacho kililalamika kwamba jana asubuhi Mwenyekiti wa tawi la Magadirisho, Kata la Usa River, Nuru Maeda (53) alitekwa na watu wanaodhaniwa kuwa ni makada wa CCM na kumpa kipigo kikali.

Mwenyekiti huyo alikutwa na mkasa huo alipokuwa akipita kuhakiki wanachama wa Chadema na alidai kwamba alitekwa  na kupelekwa katika kambi ya CCM iliyopo hoteli ya Gateways eneo la Liganga Usa River, ambako alipigwa.

Mkuu wa Oparesheni wa Polisi katika uchaguzi mdogo wa Arumeru Mashariki, Naibu Kamishna, Isaya Mngulu alivionya vyama vyote vinavyoshiriki kuhakikisha kwamba havijihusishi kwa namna yoyote na uhalifu ili kueupuka mkono wa sheria.  
 
DC Mngulu alisema mwenendo wa aina hiyo haufai kwani unaweza kuingiza uchaguzi huo mdogo kwenye fujo na vurugu, hivyo kuhatarisha hali ya amani na utulivu na kutia kasoro mwenendo wa uchaguzi mzima.

Alisema baadhi ya malalamiko yamewasilishwa katika Kamati ya Maadili inayoongozwa na Msimamizi wa Uchaguzi ili kuyafanyia kazi na kwamba kamati hiyo ilitarajiwa kukutana jana.Msimamizi wa Uchaguzi Jimboni Arumeru Mashariki, Trasias Kagenzi alithibitisha kuwapo kwa kikao cha kamati ya maadili ambacho kilitarajiwa kujadili mashauri yote na kutoa uamuzi ambao ni mwongozo wa kuwa na kampeni za kistaarabu.
 

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Thobias Andengenye alisema polisi wataendelea kushirikiana na vyama vya siasa vinavyoshiriki, ili kuhakikisha amani inatawala wakati wote wa kampeni na hata uchaguzi wenyewe.
Share this article :

Post a Comment

KARIBU KATIKA WEBSITE YA KIJANJA, KUPATA HABARI MBALIMBALI ZA NDANI NA NJE YA NCHI. PIA UTAPATA MAMBO YA ACADEMIC. KARIBU SANA
 
Support : Creating Website | Johny Template | Mas Template
Copyright © 2011. GetInformedTz - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Mas Template
Proudly powered by Blogger