Home » » Wabunge waibua ufisadi wa mabilioni D’Salaam

Wabunge waibua ufisadi wa mabilioni D’Salaam

Written By Koka Albert on Wednesday, March 28, 2012 | 11:12 PM

Patricia Kimelemeta na Ramadhan Semtawa
KAMATI ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC), imeibua tuhuma za ufisadi wa Sh2.7 bilioni katika mradi wa ujenzi wa machinjio ya kisasa Gongo la Mboto, Dares Salaam uliopaswa kufanywa na Kampuni ya East Africa Meat (EAMC).
Mradi huo ulipaswa kutekelezwa kati ya mwaka 2005/06 kwa ushirikiano wa jiji na Manispaa tatu za Dar es Salaam.

Akizungumza Dar es Salaam jana kwenye kikao kati ya kamati yake na watendaji wa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni, Mwenyekiti wa LAAC, Augustine Mrema alisema kampuni hiyo ya Malaysia ndiyo iliyoshinda zabuni ya ujenzi wa machinjio hayo.
Mrema alisema katika mradi huo, Halmashauri ya Jiji iliingia mkataba wa kughushi na EAMC, huku wakiwashawishi watendaji kushiriki kwenye ujenzi wa machinjio hayo yanayodaiwa kuwa ya kisasa.
Alisema kutokana na hali hiyo Halmashauri ya Kinondoni ilitoa Sh229milioni wakati ya Ilala ilitoa Sh364miloni, Temeke ilitoa Sh224milioni huku jiji likitoa Sh1.2bilioni.
Alisema kutokana na hali hiyo, fedha hizo zimepelekwa kwenye miradi huo ambao mpaka sasa haujatekelezeka jambo ambalo linaonyesha kuwa kuna baadhi ya wajanja ambao wamechukua fedha hizo.
“Tunajua kabisa kuwa kuna baadhi ya vigogo wameshiriki kuwarubuni watendaji wa halmashauri kwa ajili ya kutekeleza miradi hewa, hatutakubali na kila aliyeshiriki atachukuliwa hatua za kisheria,” alisema Mrema.
Alisema mbali na hilo, baadhi ya vigogo hao ndiyo walioshiriki kwenye kashfa ya Shirika la Usafiri Dar es Salaam (UDA), ambalo ripoti yake bado inasubiriwa ikabidhiwe serikalini kutoka kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).
Mrema alisema kutokana na hali hiyo, LAAC itawasilisha taarifa hizo kwa watendaji wakuu ili waweze kuangalia hatua stahiki za kurudishwa kwa fedha hizo katika halmashauri ikiwa ni pamoja na kuwafikisha mahakamani wahusika walioshiriki kwenye utapeli huo.
“Haiwezekani hata kidogo watu wachache wanufaike na rasilimali za taifa kwa manufaa yao, jambo ambalo limesababisha kuingia mikataba feki ambayo wanajua kabisa kuwa haiwanufaishi wananchi. Lazima fedha hizi zirudi,” alisema.

Meya: Kampuni imefilisika
Hata hivyo, Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Dk Didas Masaburi alisema kampuni hiyo imefilisika na kwamba hakuna mtu atakayeweza kulipa deni hilo. Kutokana na hali hiyo, alisema watakaa na halmashauri za manispaa ili kuangalia jinsi ya kutatua matatizo hayo.
“Kampuni yenyewe imefilisika, nani atalipa deni hilo? Hakuna kwa sababu hata jiji ni miongoni mwa watu waliotapeliwa japo tulikuwa tumeingia ubia lakini kilichofanyika ni kwamba mradi huo haujatekelezeka,” alisema Dk Masaburi.

Alisema machinjio hayo yalitakiwa kujengwa mwaka 2006, lakini mpaka sasa hayajengwa na wala hakuna eneo la ujenzi. Meya Masaburi alisema halmashauri hizo zilitoa fedha hizo na kudaiwa kuwa zimetumika kwenye upembuzi yakinifu na kuongeza kwamba, ilipofika mwaka 2009, madiwani wa jiji na manispaa walitaka ufafanuzi kuhusu suala hilo na kuitaka jiji kujiondoa kwenye mkataba huo jambo ambalo lilisababisha halmashauri hizo kudai fedha zao ambazo mpaka sasa hazijalipwa.
Alisema wakati hayo yakiendelea, tayari kampuni hiyo ilikuwa imefilisika na hakuna mtu mwenye uwezo wa kuendelea na mkataba au kurudisha fedha.
“Meneja wa kampuni hiyo ambaye ni raia wa Zimbabwe aliyejulikana kwa jina la Benjamin Chipazi ni miongoni mwa watu waliotapeliwa, anadai mafao yake ya zaidi ya Dola za Marekani 150,000, lakini ameshindwa kulipwa kwa sababu hakuna mtu aliyerithi madeni hayo,” alisema.
Alisema kutokana na hali hiyo, jiji haliwezi kurithi madeni ya kampuni hiyo na kwamba kila mmoja anapaswa kutambua kuwa katika mkataba huo wametapeliwa.
Iddi Simba Mwenyekiti

Alipoulizwa jana, Mwenyekiti wa EACM, Iddi Simba alikiri kuwa kampuni hiyo na ilikuwa ijenge mradi huo.
Alisema EACM ilikuwa ni kampuni iliyoanzishwa kwa kuhusisha jiji na Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam wakati huo alikuwa akiingia kwenye vikao akiwa mjumbe.
Alisema awali, jiji na manispaa zake tatu lilibuni mradi huo wa kujenga machinjio ya kisasa katika kiwanja chake cha Gongo la Mboto kilichokuwa na thamani ya Sh bilioni moja ambacho kilitumika kama sehemu ya mchango wa fedha katika hisa zake.
Alisema katika mkataba huo, Manispaa za Ilala, Temeke na Kinondoni kila moja ilipaswa kutoa Dola 500 za Marekani ikiwa ni mchango kwa hisa zake hivyo kufanya tahamani ya mtaji kufikia Dola 2.5milioni.
“Lakini, kilichotokea ni kwamba, fedha hizo za manispaa hazikutolewa katika kipindi ambacho mradi ulipaswa kuanza. Hivyo, kampuni ikafilisika kwa sababu hata watu wengine waliotaka kuwekeza fedha zao walisita baada ya kuona manispaa hizo zinasuasua,” alisema.

Alisema kampuni iliyofanya upembuzi yakinifu ilikuwa ya mhadhiri mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (jina tunalihifadhi kwa kuwa hakupatikana kujibu madai hayo jana).
Simba alisema hakuna fedha ambayo imeliwa na EACM kwani hata kiwanja hicho ambacho ni mali ya halmashauri ya jiji, bado kiliachwa mikononi mwa mamlaka hiyo.

Kuhusu ni kiasi gani cha fedha ambacho manispaa hizo tatu zilitoa hadi kampuni hiyo ilipokuwa ikikaribia kufilisika, Simba alijibu, “Sijui. Wewe umenikurupusha tu hapa sina nyaraka zozote.”
Lakini alisisitiza kwamba EACM haikuwahi kuuza kiwanja hicho kwani bado kiliachwa mikononi mwa jiji hilo hadi kampuni ilipofilisika.
Share this article :

Post a Comment

KARIBU KATIKA WEBSITE YA KIJANJA, KUPATA HABARI MBALIMBALI ZA NDANI NA NJE YA NCHI. PIA UTAPATA MAMBO YA ACADEMIC. KARIBU SANA
 
Support : Creating Website | Johny Template | Mas Template
Copyright © 2011. GetInformedTz - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Mas Template
Proudly powered by Blogger