Home » » Mwasika ajutia kumchapa mwamuzi

Mwasika ajutia kumchapa mwamuzi

Written By Koka Albert on Wednesday, March 14, 2012 | 1:46 AM

BEKI wa Yanga, Stephano Mwasika amewaomba radhi mashabiki wa Yanga kwa kitendo chake cha kumpiga ngumi mwamuzi Israel Nkongo kwenye mchezo wao dhidi ya Azam Jumamosi iliyopita.
Katika pambano hilo, Yanga ilijikuta ikimaliza mchezo huo na wachezaji nane baada ya Haruna Niyonzima na Nadir Haroub kupewa kadi nyekundu na kufungwa 3-1.

Kadi hizo mbili zilisababisha vurugu miongoni mwa wachezaji wa Yanga na mwamuzi Israel Nkongo, hali iliyosababisha Kamati ya Ligi kumfungia kucheza soka mwaka mzima mchezaji Mwasika.
Mwasika alisema amesikitishwa na adhabu iliyotolewa na Kamati ya Nidhamu, huku akikiri kutenda kosa hilo ingawa amedai adhabu ni kubwa ukilinganisha na kosa alilofanya.
Akizungumzia adhabu hii jana kwa simu, Mwasika alisema bado hajapata barua rasmi kuhusu adhabu yake, lakini hata kama nitaipata hatakata rufaa isipokuwa kuwaomba radhi viongozi wake.
"Dada yangu, habari za mimi kufungiwa ndiyo kwanza nakusikia wewe hivi sasa. Sifahamu lolote na wala barua sijapewa," alisema Mwasika kwa upole. "Kama uamuzi uliotolewa ndiyo huo, kweli sina pingamizi ingawa nimeumizwa sana, kwanza mashabiki wangu watalipokeaje? Nawaomba radhi kwa hili pamoja na benchi zima la ufundi kwa kipindi chote ambacho nitakua nje ya uwanja," alisema Mwasika kwa masikitiko.

Beki huyo aliongeza kuwa ni vigumu kueleza maisha yake kwa sasa atakapokua kifungoni kwa kipindi chote.
Naye, Jerryson Tegete aliyefungiwa mechi sita pamoja na adhabu ya faini ya sh.500,000 aliiambia Mwananchi jana kuwa adhabu hiyo hakuistahili kwani yeye aliingia uwanjani kwa lengo la kuwatuliza wachezaji wenzake na siyo kufanya vurugu kama walivyomuhukumu. "Nimeshangaa kama kweli na mimi nimeingizwa katika adhabu hiyo. Kama kweli, basi nakiri kusema nimeonewa sana. Sielewi hizo kanuni zilizotumika kunihukumu," alisema Tegete.

Aliongeza: "Niliingia uwanjani kuwatuliza wachezaji wenzangu na siyo kufanya vurugu kama wanavyosema. Nasubiri viongozi wangu watasema nini." Mbali na mchezaji huyo adhabu hiyo pia iliipita kwa Nadir Haroub, ambaye atakosa mechi sita pamoja na adhabu ya kulipa faini ya Sh500,000, huku Omega Seme na Nurdin Bakari wakikosa mechi tatu na kulipa faini ya Sh500,000.

Kwa upande wa msemaji wa Yanga, Luis Sendeu kwa niaba ya uongozi alisema, wamepata barua toka TFF, lakini hawajaridhishwa na uamuzi huo kwani haukuzingatia kanuni za uendeshaji ligi.
"Huku ni kuwakomoa wachezaji na kuwaharibia maisha. Kisheria walipaswa kufungiwa michezo mitatu, sasa unamfungia mchezaji mwaka mzima haya ni mambo ya kukomoana. Tutakata rufaa," alisema Sendeu.

Share this article :

Post a Comment

KARIBU KATIKA WEBSITE YA KIJANJA, KUPATA HABARI MBALIMBALI ZA NDANI NA NJE YA NCHI. PIA UTAPATA MAMBO YA ACADEMIC. KARIBU SANA
 
Support : Creating Website | Johny Template | Mas Template
Copyright © 2011. GetInformedTz - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Mas Template
Proudly powered by Blogger